Na Eleuteri Mangi (MAELEZO)
Ni
siku chache tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete amuapishe Mheshimiwa Juma Nkamia kuitumika Serikali kama
Naibu Waziri katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Kwa
taaluma, Naibu Waziri Nkamia ni mwanahabari ambaye amesomea na kufanya
kazi ya habari kwa kipindi kirefu kabla ya kuingia katika Ubunge ambao
umemuwezesha kuteuliwa kuwa waziri.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili katika wizara hiyo,
Nkamia alisema anamshukuru Rais Kikwete kwa kumteua na kumpa dhamana
hiyo na kuahidi kuwa atasaidiana na Waziri wa wizara hiyo kutimiza
majuku ya wizara katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya nne.
“Kama
kiongozi mwenye mamlaka ndani ya wizara hii, nipo tayari kushirikiana
na viongozi wenzangu katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo kupitia Idara zote zinazounda wizara hiyo”, alisema.
Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inaundwa na idara kuu nne za
kisekta ambazo ni Idara ya Habari, Idara ya Vijana, Idara ya Maendeleo
ya Utamaduni na Idara ya Maendeleo ya Michezo.
Kwa
kuwa tasnia ya habari ni miongoni mwa idara zilizo chini ya wizara hii,
Nkamia alisema kuwa yupo tayari kushirikiana na wadau wa habari ikiwemo
kusimamia maslahi ya waandishi wa habari nchini.
“Ukitaka
kujua umuhimu wa vyombo vya habari na waandishi wa habari katika nchi
yeyote ile, jaribu kuvifanya vyombo hivyo kuanzia redio, televisheni na
magazeti visifanye kazi hata kwa muda wa saa moja tu uone ni hasara
kiasi gani na hatari kiasi gani zitatokea katika nchi ile” alisema
Nkamia.
Alisema
anaheshimu na anatambua umuhimu wa vyombo vya habari na waandishi wa
habari nchini na atafanya nao kazi vizuri kwa kipindi chote atakachokuwa
wizarani hapo.
Alisema
kuwa anatambua kuwa waandishi wa habari wanafanya kazi katika
mazingira magumu wakati wa kutekeleza majukumu yao ikiwemo tatizo la
“ukanjanja” na lugha mbalimbali zinozotolewa juu yao.
No comments:
Post a Comment