Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima
Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima, amejikuta katika wakati mgumu baada ya wananchi wa jimbo lake kumshtaki kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kuwa hawatembelei jimboni.
Wananchi hao walimshtaki Malima ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha baada ya Kinana kuanzisha utaratibu mpya wa kuwataka wananchi waulize maswali magumu kwa viongozi wao ili wayajibu papo hapo aliouita ‘mahakama ya hadhara’.
Kinana alianzisha utaratibu huo juzi, katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kimanzichana, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 10 katika mkoa wa Pwani wa kukagua na kuhimiza utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2010/15.
“Hii ni mahakama ya hadhara, lazima kiongozi ajibu matatizo yanayolalamikiwa na wananchi, uongozi ni utumishi ya siyo utukufu, hivyo mnapaswa kuwatumikia wananchi waliowapatia fursa ya kuwa viongozi, lazima mjibu haya maswali ambayo wananchi wanayauliza. Kila mtu abebe msalaba wake,” alisema Kinana.
Mkazi wa kijiji hicho, Jamal Said, alisema kitendo cha Malima kutofika katika jimbo hilo kwa kipindi kirefu ndicho kinasababisha kero za wananchi zisitatuliwe.
“Katibu, Chama hiki ni kizuri ila watendaji wake ndiyo wanakiharibu, mbunge wetu hana utaratibu wa kuja huku mara kwa mara ndiyo maana unaona tunaeleza changamoto nyingi, hatuna pa kuzisema,” alisema.
Akijibu malalamiko hayo, Malima alikutana na zomea zomea ya wananchi, iliyoambatana na kauli za kebehi za ‘Utaachaje kuzomewa kama huji kutuona huku jimboni’, ‘huji jimboni mpaka udandie ziara ya wakubwa wako.’
Baada ya wananchi hao kuendelea kumzomea, Malima alidai kuwa anafahamu kuwa kelele hizo hazikukuwa za wana-CCM bali ni za vyama vya upinzani.
Aidha, alikiri kufahamu kero hizo zote na kusema kuwa zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi likiwamo la wananchi kurudishiwa eneo lao la bonde linalodaiwa kuuzwa.
Mbali na Malima, wengine waliokumbwa maswahiba hayo ya kujibu kero mbalimbali za wananchi walizouliza ni Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu na watendaji wenyeviti wa vijiji.
Akiuliza swali kwa niaba ya wanakijiji hao, Salum Lijonjo, mkulima wa mpunga, alisema viongozi wa serikali na chama walishirikiana kuuza eneo la kulima mpunga lililopo katika kijiji cha Lupondo na kijiji cha Mvule.
“Tunashukuru kwa ujio wako Katibu Mkuu kwa kuwa tunamini kilio chetu hiki kitapata majibu kwani tulikuwa tukilitegemea bonde hili kwa kilimo, lakini sasa limeuzwa hatuna pa kulima, tunaomba ubabaishaji huu uchukuliwe hatua,” alisema.
Akijibu malalamiko hayo, Katibu Tarafa ya Mkamba, Amini Mussa, alisema serikali imetoa agizo la kutotambua mauziano hayo na kwamba litaendelea kutumiwa wakulima.
“Wakulima endeleeni kulima kwa kuwa hatutambui kilichofanyika. Yeyote atakayedai kulinunua awabane waliomuuzia, kwa lugha rahisi imekula kwake aliyenunua,” alisema.
Jamal Said pia alimtaka Kinana awasaidie kuondokana na kero ya kulipa ushuru mkubwa katika vivuko vya mazao ya misitu.
Akijibu baadhi ya hoja hizo, Kinana aliahidi kulifikisha suala la ushuru wa mazao ya misitu kwa Waziri wa Maliasili na Utalii ili kupunguza ushuru huo ambao unawanyonya wananchi.
“Haiwezekani, ushuru wa serikali ni asilimia 18, lakini eti hapa , mnalipa asilimia 100,” alisema na kuongeza: “Nitazungumza na waziri ili tuone namna ya kupunguza ushuru huu.”
Wananchi hao wamekuwa wakilipa ushuru wa Sh. 120,000 kwa kitanda kimoja ambacho kinauzwa Sh. 120,000.
Kinana, ambaye amefuatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, yuko mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 30 katika mkoa huo, Tanga na Iringa ya kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2010/15 pamoja na kusikiliza kero za wananchi.
No comments:
Post a Comment