“Unajua kuna ‘presha’ kubwa kwamba Rasimu ya Katiba inayopendekezwa iwe imetoka Septemba 21, sasa hiyo inaifanya kamati hiyo kufanya kazi hadi usiku,”.PICHA/MAKTABA.
Dodoma. Mzimu wa posho umeibuka upya katika Bunge la Katiba, safari hii wajumbe wake wa Kamati ya Uandishi wakiomba walipwe posho maalumu ya Sh500,000 kwa siku kutokana na kazi ya kuandika Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
Habari zilizolifikia Mwananchi na kuthibitishwa na uongozi wa Bunge zinasema kuwa tayari maoni ya wajumbe yamewasilishwa kwa uongozi kwa ajili ya uamuzi.
Wajumbe wa kamati hiyo kwa sasa wanalipwa posho maalumu ya Sh210,000 zaidi kwa siku, nje ya ile ya Sh300,000 kwa siku wanayolipwa wajumbe wote wa Bunge hilo.
Kamati hiyo inayoongozwa na Andrew Chenge ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi-CCM inahusisha baadhi ya vigogo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Vigogo hao ni pamoja Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose Migiro, Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema, Mwanasheria Mkuu wa SMZ, Othman Masoud Othman aliyejiuzulu ujumbe wa kamati hiyo hivi karibuni kwa sababu ambazo hazijaelezwa.
Katibu wa Bunge, Yahaya Khamis Hamad pamoja na kukiri kuwa kamati hiyo imeomba kuongezwa kiasi hicho cha posho, alisema Kamati ya Uongozi ambayo ndiyo huamua, haijayajadili maombi hayo na kuyatolea uamuzi.
Chenge hakupatikana jana kuzungumzia maombi hayo.
Gharama kuongezeka
Endapo Kamati ya Uongozi inayoongozwa na Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta itaridhia maombi hayo kwa wajumbe 24 wa kamati hiyo, Bunge hilo litatumia Sh12 milioni kwa siku.
Vyanzo vya habari vimedokeza kuwa iwapo nyongeza hiyo itaanza kulipwa, wajumbe wa kamati hiyo watakuwa wakizoa jumla ya Sh800,000 kwa siku.
“Msingi wa kuomba posho hiyo ya Sh500,000 kwa siku unatokana na wajumbe wa kamati kufanya kazi hadi usiku wa manane,” alidokeza mmoja wa wajumbe wa Bunge.
“Unajua kuna ‘presha’ kubwa kwamba Rasimu ya Katiba inayopendekezwa iwe imetoka Septemba 21, sasa hiyo inaifanya kamati hiyo kufanya kazi hadi usiku,” alifafanua mjumbe huyo.
Kwa sasa kamati hiyo imekuwa ikifanya kazi ya ziada kuingiza michango ya wajumbe wa Bunge hilo inayotokana na majadiliano baada ya kamati kumaliza kuwasilisha taarifa zake Septemba 8, mwaka huu.
Kamati hiyo inatarajiwa kuendelea na mchakamchaka huo hadi hatua ya Rasimu ya Katiba inayopendekezwa itakapopigiwa kura na wajumbe wa Bunge hilo kuanzia Septemba 26, mwaka huu.
Katibu aitetea
Katibu wa Bunge, Hamad aliitetea kamati hiyo akitaka Watanzania kufahamu kuwa wajumbe wake wamekuwa wakifanya kazi kubwa na wamekuwa wakitoka katika vikao saa 8.00 usiku.
“Hata jana (Jumamosi) mimi nilitoka pale saa 5.00 usiku niliwaacha ndiyo wanaletewa chakula cha usiku,” alisema Hamad.
Alisema hata baada ya wajumbe kukamilisha kazi yao, watendaji wamekuwa wakikesha ili kukamilisha kazi walizopewa na kamati hiyo.
Wakati Bunge hilo lilipoanza vikao Februari mwaka huu, baadhi ya wajumbe walitaka posho ya Sh300,000 wanayolipwa iongezwe wakisema ilikuwa haitoshelezi kuishi mjini hapa na kudai ifikie Sh500,000.MWANANCHI
No comments:
Post a Comment