Mkurugenzi
wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw.
Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya mfumuko wa bei nchini kwa mwezi
Agosti, 2014 leo jijini Dar es salaam.
Na Aron Msigwa-MAELEZO.
Mfumuko
wa Bei wa Taifa kwa mwezi Agosti, 2014 umeongezeka hadi kufikia
asilimia 6.7 kutoka asilimia 6.5 iliyokuwepo mwezi Julai kutokana na
kuendelea kupanda kwa bei ya baadhi ya bidhaa na huduma katika maeneo
mbalimbali nchini.
Mkurugenzi
wa Sensa na Takwimu za Jamii Bw. Ephraim Kwesigabo akitoa taarifa ya
ongezeko hilo leo jijini Dar es salaam, amesema kuwa bidhaa zisizo za
vyakula zikiwemo Bia, Sare za shule, mkaa, samani za nyumbani na bidhaa
za vitambaa kwa matumizi ya nyumbani zimechangia kuwepo kwa ongezeko
dogo la mfumuko wa bei nchini.
Ameongeza
kuwa kuwepo kwa ongezeko la gharama kwenye huduma ya meno, huduma za
vyakula kwenye migahawa na zile za kulala hotelini katika maeneo
mbalimbali nchini pia zime kumechangia mfumuko wa bei.
Aidha,
Bw. Kwesigabo amebainisha kuwa kuongezeka kwa Fahirisi za bei kwa maana
ya kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma
mbalimbali zinazotumiwa na sampuli wakilishi ya kaya binafsi nchini hadi
149.31 kwa mwezi Agosti 2014 kutoka 149.16 za mwezi Julai kumechangiwa
na kupanda kwa gharama ya bidhaa zisizo za vyakula.
Kuhusu
mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi kwa mwezi Agosti amesema
kuwa umeongezeka kwa asilimia 0.1 huku uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania
katika kununua bidhaa na huduma za jamii kwa mwezi Agosti, 2014
ukipungua na kufikia shilingi 66 na senti 97.
“
Kuongezeka kwa bei ya baadhi ya bidhaa na huduma katika maeneo
mbalimbali kuna athari kwa fedha yetu, hii inamaanisha kwamba, uwezo wa
fedha yetu katika kununua huduma na bidhaa za mlaji unapungua, mfumuko
wa bei unapopanda thamani ya shilingi nayo inashuka”
Kwa
upande wa ulinganifu wa mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za
Afrika Mashariki Bw. Kwesigabo ameeleza kuwa una mwelekeo unaofanana na
kuongeza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya kwa mwezi Agosti umefikia
asilimia 8.36 ikilinganishwa na 7.67 za mwezi Julai huku Uganda ikiwa na
mfumuko wa bei wa asilimia 2.8 mwezi Agosti ikilinganishwa na asilimia
4.3 za mwezi Julai.
No comments:
Post a Comment