Mwanaharakati
toka Shirika la Kutetea Haki za Wanawake la KIVULINI la jijini Mwanza,
Bi. Khadija Liganga ametoa mafunzo ya siku moja kuhusu Unyanyasaji wa
kijinsia na ukatili Dhidi ya watoto kwa vijana takribani 100 wa jiji la
Mwanza ikiwa ni hatua za kuwajenga vijana katika misingi ya kuachana na
mila, tamaduni na dhana potofu zinazowakandamiza wanawake na watoto
katika jamii.
Semina
hiyo iliyoandaliwa na Teen Club Mwanza, ililenga Kujenga uwezo wa
kutambua ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, kuelewesha na kutoa njia za
namna ya kuripoti unyanyasaji na ukatili na kuwasihi vijana
kutoendeleza tabia za unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake na
watoto.
Akizungumza
mara baada ya kutoa mafunzo hayo Bi. Khadija Liganga alisema ni lazima
jamii ichukue jukumu la makusudi kukomesha vitendo vyote
vinavyowakandamiza na kuwanyanyasa wanawake na watoto kwani ni moja ya
sehemu inayochangia kwa kiasi kikubwa kuleta umasikini na kurudisha
nyuma gurudumu la maendeleo kwa haraka sana.
“Mwanamke
akipigwa au kutukanwa hatoweza kufanyakazi zake, mtoto akiteswa na
kunyanyaswa hatoweza kusoma vizuri shuleni, huwezi pata maendeleo. Ili
vijana waweze kupeleka ujumbe sahihi wa masuala ya ukatili wa kijinsia
wanatakiwa kujua na kufahamu masuala yanayohusiana na tofauti za
kijinsia, kulingana na suala la ukatili wa kijinsia (GBV) na namna ya
kuzikemea tabia hizo” alisema Bi. Khadija.
Kwa
mujibu wa ripoti ya UNICEF ‘Watoto na Wanawake Tanzania’ ya mwaka 2010
inasema kuwa kuwekeza kwa watoto na wanawake ni moja ya njia bora kabisa
kwa maendeleo ya Tanzania. Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012
inaonesha Zaidi ya asilimia 50 ni watoto, ubunifu wao na umahiri wao
katika kuzalisha ndio msingi mkubwa wa kufikia malengo ya Tanzania 2025.
Bi.
Khadija aliendelea kusema kuwa bado katika jamii nyingi watoto hukatazwa
kusema hadharani kwamba wananyanyaswa, mila nyengine watoto hawastahili
kuzizungumzia, hivyo hivyo mwanamke anaona aibu au anaogopa kuzungumzia
suala la ukatili wakati mwanaume anaweza kufanya kisema mbele za watu
na wakati mwingine kwa kujidai /kujigamba amempiga mkewe. Hivyo basi
ushiriki wa wa vijana ni muhimu sana kuelimishwa ili kujenga familia na
jamii salama isiyo na ukatili Dhidi ya wanawake na watoto.
“Ni
swali la kujiuliza kama sisi watu wazima tumeshindwa kujenga miji iliyo
salama, kwanini tusiwekeza nguvu nyingi kwa hawa vijana, waswahili
husema ‘ashakum si matusi’ni ngumu kumfundisha mbwa mzee mbinu mpya,
hivyo naomba serikali, vyombo vya habari, mashirika ya kijamii, wazazi,
pamoja na wanaharakati kuwekeza katika kuwapa kundi hili la vijana elimu
ya ukatili wa kijinsia na haki za watoto ili kujenga kizazi bora”
alimalizia kwa kusema Bi. Khadija.
Ripoti
ya “Ukatili Dhidi ya Watoto Tanzania” ya UNICEF 2011, inasema kuwa
karibu wasichana 3 kati ya 10 na mvulana 1 kati ya 7 wameripoti
kutendewa walau tukio moja la ukatiliwa kijinsia kabla ya kutimiza umri
wa miaka 18. Huku karibu asilimia 6 ya wasichana wamelazimishwa
kujamiiana kabla hawajatimiza miaka 18. Marafiki, majirani, na watu
wasiowafahamu walitajwa na wasichana na wavulana kama wakosaji wa
ukatili wa kijinsia.
Kundi
la vijana Zaidi ya 100 toka katika klabu ya Vijana (Teen Club) jijini
Mwanza wakisikiliza kwa makini mafunzo toka kwa Bi. Khadija Liganga ya
jinsi gani wanaweza kukabiliana na Unyanyasaji na Ukatili wa kijinsia
lakini pia jinsi ya kuripoti matukio mbalimbali ya ukatili katika vyombo
husika.
Bi.
Khadija Liganga, Mwanaharakati wa kupigania Haki za Wanawake wa Shirika
la Kutetea Haki za Wanawake KIVULINI akitoa semina ya siku moja kuhusu
unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto kwa vijana Zaidi ya
100 kutoka klabu ya vijana (Teen Club) ya jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment