KLABU
ya Mbeya City inatarajia kuanza kambi yake rasmi baada ya sikukuu ya
krismasi kuongeza makali yao kuelekea mzunguko wa pili wa ligi kuu soka
Tanzania bara unaotarajia kuanza kushika kasi mnamo januari 25 mwakani.
Akizungumza
leo hii, kocha mkuu wa klabu hiyo, Juma Mwambusi amesema kwasasa
wanaendelea na mazoezi ya kawaida ambapo vijana wake wanatokea kwao,
lakini baada ya sikukuu wataingia kambini rasmi.
“Tunafahamu
kuwa timu nyingi zinachukua tahadhari kubwa zaidi kwa ajili yetu. Hii
ni changamoto kubwa kwetu na ndio maana mikakati yetu ni kuwa na kambi
bora kuandaa vijana wetu kwa ajili ya kuwa na kasi zaidi mzunguko wa
pili”. Alisema Mwambusi.
Mwambusi aliongeza kuwa wachezaji wake wapo katika hali nzuri na kilichobaki ni kuanza programu ya mazoezi rasmi.
Kocha
huyo aliyejizolea umaarufu baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza bila
kufungwa mechi yoyote alisisitiza kuwa ana kikosi bora na ndio maana
hakufanya usajili katika dirisha dogo la usajili.
“Ninao
vijana wengi wenye kiwango cha juu, ni maamuzi yangu kumtumia yupi na
kumuacha yupi. Tutafanya vizuri kutokana na ubora wetu”. Aliongeza
Mwambusi.
Aidha Mwambusi amewaomba mashabiki wao Tanzania nzima kuendelea kuwa na ushirikiano mkubwa kama mzunguko wa kwanza.
“Mashabiki
ni mchezaji wa kumi na mbili. Nawashukuru sana kwa kuendelea kutuunga
mkono, lakini nawaomba waendelee kuwa nasisi katika harakati zetu.
Hatuna cha kuwalipa zaidi ya kuucheza mpira wenyewe kwa kiwango cha
juu”. Alisema Mwambusi.
Mbeya
City FC ilimaliza mzunguko wa kwanza katika nafasi ya tatu ikiwa na
pointi 27 sawa na Azam fc waliopo nafasi ya pili kwa pointi sawa na
klabu hiyo, lakini wana wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Vinara
wa ligi hiyo ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo, klabu ya Dar Young
Africans wenye pointi 28, huku watani zao wa jadi, Simba Sc wapo nafasi
ya nne kwa pointi zao 24.
No comments:
Post a Comment