DODOMA/DAR ES SALAAM.
BAADHI ya wabunge wameanzisha mkakati wa kumwondoa madarakani, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kile wanachodai kuwa hawaridhishwi na utendaji wake serikalini.
Hiyo ni dalili kwamba kung’oka kwa mawaziri wanne
kutokana na matokeo ya ripoti ya utekelezaji wa Operesheni Tokomeza
Ujangili hakujamnusuru Pinda, kwani baadhi ya wabunge wanaendelea na
msimamo kwamba naye ajiuzulu kwa kushindwa kuwasimamia wenzake.
Mawaziri waliong’oka baada ya Rais Jakaya Kikwete
kutengua uteuzi wao kutokana na ripoti iliyowasilishwa na Kamati ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ni Mawaziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk
Emmanuel Nchimbi, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo
na Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki.
Hatua hiyo ya Rais Kikwete inatafsiriwa na wengi
kama njia ya kuwapoza wabunge na kumwokoa Pinda ambaye ikiwa atang’oka
itamaanisha kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri.
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili jana
zinasema wabunge 26 wametia saini fomu maalumu ya kutaka Bunge litumie
mamlaka yake ya kikatiba kumng’oa Pinda kwa kumpigia kura ya kutokuwa na
imani naye.
Kwa mujibu wa Ibara ya 53 A(1) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Bunge linaweza kupitisha azimio
la kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu, endapo itatolewa hoja
kupendekeza hivyo.
Kwa mujibu wa Ibara hiyo, hoja ya kumpigia kura ya
kutokuwa na imani na waziri mkuu inapaswa kuungwa mkono na wabunge
wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses
Machali alisema hili jana kuwa ukusanyaji saini za wabunge aliouanzisha
Ijumaa jioni unakwenda vizuri.
“Kung’oka kwa mawaziri wale wanne inatosha
kuthibitisha kuwa Pinda amepoteza uhalali wa kuwa Waziri Mkuu kutokana
na kushindwa kuwasimamia walio chini yake,” alisema Machali.
“Rais tunaweza kumuacha, lakini Pinda ndiye
mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali. Kama wapo mawaziri wameboronga ni
wazi na yeye anaingia moja kwa moja katika hilo kapu,” alisema na
kuongeza:
“Kama kweli tunataka taifa lisonge mbele kutoka
hapa tulipo ni lazima tumuondoe Pinda…….. amekuwa mpole mno, mzito
kufanya uamuzi na analea matatizo.”
Hata hivyo, alisema wabunge waliosaini fomu hiyo,
wote wanatoka kambi ya upinzani na kusema wabunge wengi wa CCM
aliowafuata kuwaomba watie saini wanaogopa au wanasita kufanya hivyo. MWANANCHI
No comments:
Post a Comment