JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAMKO LA MHE. UMMY MWALIMU (MB), WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUHUSU WANANCHI KUSHAMBULIA WATUMISHI WA AFYA HASA MADAKTARI NA WAUGUZI KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI, TAREHE 29 MACHI, 2016
Nachukua
fursa hii nikiwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya afya nchini, kutoa
tamko kuhusiana na matukio ya hivi karibuni yaliyoripotiwa kwenye
vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusiana na vitendo vya
kusikitisha wanavyofanyiwa watumishi wa sekta ya afya, wakiwemo
Madaktari kama vile kushambuliwa kwa maneno na vipigo. Pasi na shaka,
vitendo hivyo vitaathiri upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi
wanaopewa huduma hizo hususan wa kipato cha chini.
Matukio haya
yanajumuisha tukio lililotokea tarehe 27.03.2016 katika Hospitali ya
Mkoa wa Mtwara, Ligula, ambapo Dr Dickson Sahini alishambuliwa na ndugu
wa mgonjwa aliyepelekwa hapo kuhudumiwa.
Napenda kutamka kwamba
nimesikitishwa sana na tukio hilo, na ninalaani vikali matukio ya
watumishi wa afya kushambuliwa kwa maneno au kwa vitendo na wananchi
wanaopatiwa huduma. Jambo hili likiendelea litawavunja moyo watumishi wa
afya na hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Ningependa
kuwafahamisha kwamba kwa ujumla wake sekta ya afya inakabiliwa na
changamoto nyingi sana katika maeneo ya miundombinu, dawa na vifaa tiba,
watumishi wa kutosha, pamoja na kuwa na watumishi wasiozingatia
nidhamu, weledi na maadili katika kutimiza majukumu yao.
Ninatambua
kwamba changamoto hizi zipo siku nyingi, na zimekuwa zikitafutiwa
majawabu na Serikali za awamu zilizopita ikiwemo ile ya awamu ya nne.
Lakini sote ni mashahidi kwamba Serikali ya awamu ya tano, chini ya
uongozi wa Mheshimiwa Dr John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, inachukua hatua za makusudi katika kutatua
changamoto hizi, likiwemo pia suala zima la utendaji unaozingatia
uwajibikaji.
Kwa hiyo ninawasihi sana wanachi wanaopatiwa huduma
katika vituo vyetu vya afya kote nchini kuacha mara moja tabia ya
kujichukulia sheria mikononi na kufanya vitendo vinavyoweza kuwakwaza
watumishi wa afya. Kwa vile nchi yetu inafuata misingi ya utawala
unaozingatia sheria, ni vyema wananchi wakafuata taratibu zilizowekwa
wanapohisi kwamba hawakupatiwa huduma za afya wanavyostahili.
Aidha
nachukua fursa hii kuvitaka vyombo na mamlaka husika kutosita
kuwachukulia hatua wananchi wanaokwenda kinyume na matakwa ya sharia ili
kuwahakikishia watoa huduma za afya usalama na amani wakati wa utoaji
wa huduma hiyo.
Ninaagiza vile vile kwamba hospitali na vituo
vyote vya kutolea huduma za afya nchini ziweke utaratibu mwepesi wa
wananchi kufikisha malalamiko yao pindi wanapoona kwamba hawakupatiwa
huduma za afya kwa kiwango stahiki.
Napenda pia kuahidi kwamba
tutajitahidi kutatua changamoto za kimfumo zilizopo katika utoaji wa
huduma za afya nchini ili kuufanya utoaji wa huduma kuwa bora zaidi.
Ndugu Wananchi,
Ninatambua
kwamba sehemu kubwa ya watumishi katika sekta ya afya nchini wanafanya
kazi zao kwa ufanisi, upendo, uadilifu na kwa kuzingatia matakwa ya
weledi (professionalism) na miiko ya taaluma zao (ethics). Pia
ninatambua kwamba wengi wanafanya kazi katika mazingira magumu na
wanatumia muda wa ziada kuendelea kuwahudumia wagonjwa hadi wanapoona
wapo salama. Ninawapongeza kwa dhati watumishi hawa na ninawashukuru na
kuwatia moyo waendelee kuwa na tabia hiyo nzuri, kwa maslahi ya Taifa
letu.
Hata hivyo ninasikitishwa sana na tabia ya watumishi wa
afya wachache ambao wanafanya kazi kinyume na maadili na matakwa ya
weledi wa taaluma zao. Napenda kusisitiza kuwa Wizara yangu haitavumilia
matukio ambayo watumishi wa Sekta ya Afya watakwenda kinyume na matakwa
ya weledi na maadili ya taaluma zao katika vituo vya kutolea huduma za
afya nchini. Hivyo hatutasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa
Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo ili kudhibiti hali hii.
Nimeshaelekeza
vyombo vya kusimamia maadili ya watoa huduma za afya nchini, yaani
Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) na Baraza la Wauguzi na Wakunga
Tanzania (TNMC) kuchukua hatua mara moja, kwa mujibu wa Sheria na
Taratibu zao, juu ya watoa huduma wote wanaotuhumiwa kukiuka misingi ya
weledi na maadili ya taaluma zao. Endapo tuhuma zao zitathibitika, hatua
stahiki zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kufutiwa usajili au leseni zao
ikibidi.
Hivyo kwa tamko hili ninawaasa na kuwaagiza watoa
huduma wa afya wote nchini kufanya kazi zao kwa bidii, kwa nidhamu na
kwa kuzingatia weledi na maadili ya kitaaluma kama inavyoelekezwa.
Ndugu Wananchi,
Napenda
pia kukumbusha kwamba kazi hii ya usimamizi wa mahusiano mema kati ya
watoa huduma za afya na wananchi, na usimamizi wa weledi na maadili
katika vituo vya kazi, itafanikiwa kwa ushirikiano wa pamoja wa Wakuu wa
Mikoa na Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi, Kamati za Usimamiaji wa
Huduma za Afya za Mikoa na Wilaya, Kamati za Usimamiaji wa Huduma za
Afya za Hospitali, na Wananchi wote kwa ujumla katika kuwasimamia,
kuwaelekeza na kutambua mapungufu ya kimfumo au yale yanayohusu
watumishi wa afya yaliyopo na kuchukua hatua zinazostahili mara moja. Ni
lazima tuzingatie Sheria, Kanuni na Taratibu katika kutimiza jukumu
hili. Wizara ya Afya itaendelea kuvijengea uwezo Mabaraza ya kitaaluma
ya wataalamu wa afya ili kutimiza wajibu wao kikamilifu.
Tufanye kazi kwa pamoja ili kutekeleza kauli mbiu ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, inayosema ‘HAPA KAZI TU’.
Asanteni sana.
Imetolewa na:
Mhe. Ummy Mwalimu (Mb)
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mtwara – Tanzania
29 Machi 2016
No comments:
Post a Comment