TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Thursday, May 17, 2012

Ajali nzima ya Patrick Mafisango na alivyo kufa


Patrick Mafisango (kwenye picha ndogo) enzi za uhai wake. Juu ni gari aliyopata nayo ajali. 
MCHEZAJI wa timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi) na timu ya Simba Patrick Mutesa Mafisango (32), amefariki dunia jana alfajiri kwa ajari ya gari.
Amepata ajali hiyo akitokea kwenye Ukumbi wa Starehe wa Club Maisha uliyopo Masaki. Akizungumza Dar es Salaam leo, Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba Geofrey Nyange Kaburu, alisema Mafisango alikubwa na mauti hayo eneo la Keko jirani na Chuo cha VETA jijini Dar es Salaam.
Alisema Mafisango amekufa kwa ajali ya gari, baada ya gari alilokuwa anaendesha kuacha njia na kugonga mti ulio pembezoni mwa barabara ya Chang’ombe majira ya saa kumi kasorobo alfajiri na kufariki papo hapo.
Kaburu ameongeza gari hilo ndani lilikuwa na abiria wengine wanne, lakini aliyekutwa na mauti baada ya ajali ni Mafisango pekee. Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tayari kwa kusafirishwa kwenda kwao Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako atazikwa.
Kaburu alisema ingawa alikuwa na uraia wa Rwanda na akiichezea timu ya taifa ya nchi hiyo (Amavubi), Mafisango alikuwa ni mzaliwa na raia wa DRC na uamuzi wa kuzikiwa huko ni wa familia yake. Msiba wa Mafisango uko katika eneo la Keko Toroli jirani na kituo cha Chang’ombe Maduka Mawili eneo la njia Panda ya Sigara.
Mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa kesho Ijumaa saa nne asubuhi katika viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam kabla ya mwili wake
kusafirishwa kwenda Kinshasa majira ya saa kumi jioni.
Mafisango alizaliwa Machi 30, 1980 huko Kinshasa Zaire wakati huo na ameacha mke na mtoto mmoja wa kiume, Chris Paul, mwenye umri wa miaka mitano.
Mafisango ameichezea Simba kwa msimu mmoja tu akitokea Azam ya Dar es Salaam lakini kabla ya hapo alichezea pia TP Mazembe ya DRC, APR ya Rwanda na pia aliwahi kuwa nahodha wa Amavubi kwa takribani miaka mitano.
Mara baada ya taarifa hiyo wanachama wa klabu ya Simba na wachezaji walipatwa na mshtuko mkubwa ikiwa ni pamoja na kuamua kwenda Muhimbili
kuhakikisha kama ni kweli mwenzao huyo amewatoka.
Miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa karibu na Marehemu kama marafiki ni Haruna Moshi Boban ambaye yupo kwenye kambi ya timu ya Taifa, Taifa Stars alishindwa hata kufanya mazoezi na kuomba apewe nafasi ya kwenda kushuhudia mwili wa mchezaji mwenzake katika chumba cha maiti.
Boban ambaye watu wamemzoea kumuona akiwa kimya alionekana mwenye uzuni nyingi kwa kulia moja kwa moja huku akiomba apewe nafasi ya kushuhudia mwili wa mpendwa wake huyo. Wengine ni haruna Niyonzima, ambaye anaichezea Yanga, Uhuru Suleman ambao walionekana wakishindwa kuvumilia.
Wakati huo huo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa Simba na timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), Patrick Mafisango kilichotokea jana alfajiri (Mei 17 mwaka huu) kwa ajali ya gari Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa jana na ofisa habari wa TFF Boniface Wambura, alisema kuwa msiba huo ni mkubwa kwa familia ya mpira wa miguu kwani Mafisango kwa kipindi chote alichocheza mpira hapa nchini akiwa na timu za Azam na baadaye Simba, aliifanya kazi yake (kucheza mpira) kwa bidii.
Kifo chake ni pigo kubwa si tu kwa familia yake na timu alizochezea, bali ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati ambapo changamoto zake zilikuwa dhahiri uwanjani. Wakati mauti inamkuta, Mafisango alikuwa ameitwa Amavubi kwa ajili ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika zinazochezwa mapema mwezi ujao.
TFF inatoa pole kwa familia ya Mafisango, klabu ya Simba, Shirikisho la Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Mafisango mahali pema peponi.
Habari hii ni kwahisani ya Gazeti la Jambo Leo.

No comments:

Post a Comment