TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Friday, May 18, 2012

WAZIRI WA HABARI AONGOZA MAMIA YA WATANZANIA KUAGA MWILI WA MAFISANGO

Na Ismail Ngayonga

Maelezo

Dar es Salaam

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara ameungana na mamia ya Watanzania katika kuaga mwili wa aliyekuwa Mchezaji wa Klabu ya Simba Partick Mafisango aliyefariki katika ajali ya gari usiku wa kuamkia juzi katika eneo la chang’ombe Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa misa ya kuaga mwili wa Marehemu iliyofanyika katika viwanja vya Sigara, Dk. Mukangara alisema Serikali imepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mchezaji huyo kwani msiba huo ni pigo kubwa kwa wanajumuiya wa klabu ya Simba, familia na taifa kwa ujumla.

Dk. Mukangara alisema Mafisango atakumbukwa na wengi kwa kuwa alikuwa ni kijana wa mfano wa kuigwa na aliyejitolea kwa hali na mali katika kuisaidia klabu yake ya Simba katika michuano mbalimbali ya kitaifa na ile ya kimataifa.

“Mafisango alikuwa ni kijana maalum kwani alivuka mipaka na kuja nchini kuichezea Simba, na  historia yake inaonyesha kuwa aliichezea TP Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, APR ya Rwanda, pia alikuwa Nahodha wa Timu ya Taifa ya Rwanda, na alichezea klabu ya Azamu ya Jijini Dar es Salaam”.

Aidha Dk. Mukangara aliwataka wapenzi, mashabiki, wananchama na Viongozi wa Simba kutokata tamaa kutokana na msiba huo na badala yake klabu hiyo iendelee na nafasi yake ya ushindi katika michuano mbalimbali inayowakabili.

Waziri Mukangara pia alivitaka vyama vya michezo nchini kuwa na mipango endelevu ili kupata vijana wengi zaidi ili kuendeleza tasnia ya michezo nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage alisema Uongozi wa Klabu hiyo umepokea kwa masikitiko taarifa za msiba wa Mafisango kwani mchezaji huyo alikuwa mcheshi na aliyependwa na kila mtu klabuni hapo.

Rage alisema tukio la kifo cha Mchezaji huyo litakumbukwa kwa miaka mingi ijayo kwani kwa mara ya kwanza klabu hiyo kupata msiba wa mchezaji ilikuwa ni mwaka 1978, ambapo Simba iliondokewa na aliyekuwa mchezaji wake Hussein Tindwa.

Aidha Rage alisema kuwa klabu hiyo imeamua kutoitumia milele jezi namba 30 aliyokuwa akitumia Marehemu Mafisango, ikiwa ni hatua ya kuenzi mchango wa mchezaji wakati akiitumikia klabu hiyo.

Kwa mujibu wa Rage alisema katika michuano ya Ligi ya Tanzania Bara iliyomalizika hivi karibuni, mchezaji huyo alifunga magoli 11, hatua iliyomfanya kuwa mchezaji aliyeongoza  kwa idadi ya magoli iliyofungwa na wachezaji wa nafasi ya Kiungo kuliko wote katika ligi hiyo.

Naye Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, Celestine Musigwa alisema kifo cha mchezaji si pigo kwa klabu ya Simba  pekee bali pia kwa wapenda mpira wa miguu, kwani Mafisango alikuwa ni mmoja wa wachezaji hodari vijana katika medali ya mchezo wa soka nchini.  

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema shirikisho hilo limeshtushwa na taarifa za kifo cha mchezaji huyo, kwani kifo chake ni pigo kwa familia nzima ya wapenzi na mashabiki wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.

Wakati huohuo,mwili wa Maehemu Patrick Mafisango unatarajiwa kusafirishwa leo (jana) nchini kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ambapo ndipo alipozaliwa marehemu kwa ajili ya shughuli za mazishi.

Afisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema msafara wa wachezaji na Viongozi wa Simba unarajia kuongozwa na Joseph Itang’are na mwili wa Marehemu unatajia kusafirishwa kwa ndege katika uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment