TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Monday, May 14, 2012

Demokrasia ya Tanzania yapigiwa mfano duniani, na mtandao wa Gazeti la Majira


Posted: 11 May 2012 01:14 AM PDT

Wawekezaji wa madini wamponza mchimbaji
 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw.Diwani Athuman, alisema Bw. Magunila, alishambuliwa juzi mchana na kundi la wachimbaji wadogo wadogo katika machimbo ya dhahabu yaliyopo kijiji cha Mhandu kata ya Chela, wilayani Kahama.
Bw.Athuman alisema siku ya tukio hilo, Bw.Magunila alikuwa amefuatana na wawekezaji kutoka nje ya nchi na kwenda nao katika machimbo hayo bila kuwashirikisha, kitu walichomtuhumu anataka kuuza eneo hilo kwa maslahi yake binafsi, ndipo walipoanza kumshambulia kwa mawe na marungu.  
Akiongea kwa taabu na mwandishi wa habari hizi alikolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Bw. Magunila, alisema eneo hilo ni mali yao na Mkuu wa Wilaya Meja Matala kwa vile wameshalikatia leseni kutoka mwaka jana.

Bw.Magunila alisema eneo la machimbo ya dhahabu la Mhandu walishalikatia leseni ya majina mawili yeye na Meja Matala, ambapo wana viwanja sita.
Wachimbaji wadogo wadogo katika eneo hilo ambao hawakupenda majina yao yaandikwe gazetini waliwatuhumu Meja Matala na Magunila kutumia ujanja wa kulichukua eneo hilo bila wao kuwashirikisha.
Diwani wa Kata ya Chela Bw. Mibako Mabubu, alisema Bw.Magunila, alifanya kosa kwenda eneo hilo bila kushirikisha viongozi wa kata pamoja na kudai ana leseni ya viwanja sita.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama Meja Matala alipoulizwa alikiri kuwepo kwa tukio hilo ila akasema hawezi akalizungumzia suala hilo kama Bw.Magunila.
Ofisa Madini Mkazi wa Wilaya ya Kahama Bw.Tuna Badoma, alipotakiwa kuthibitisha kuhusu leseni ya Bw.Magunila na Meja Matala alisema yeye si msemaji
Posted: 11 May 2012 01:07 AM PDT

Na Godfrey Ismaely, Dar es Salaam

IMEBAINISHWA kuwa demokrasia iliyopo Tanzania ni moja wapo ya chachu inayowafanya watu wengi zikiwemo nchi zilizoendelea duniani kutamani kuwa nayo, lakini inashindikana kutokana na mifumo yao ya kiutawala.
Mbali na hayo Watanzania wamehimizwa kuendelea kuilinda, kuheshimu na kuitumia vyema demokrasia hiyo katika kujadili ikiwemo kuibua mambo ambayo hayana uchochezi ili kuharakisha maendeleo yao.
Changamoto hiyo ilitolewa juzi na Waziri Mkuu mstaafu wa Rwanda Bw. Faustine Twagiramungu ambaye kwa sasa anaishi mjini Brussels nchini Ubeligiji wakati akichangia mada kwenye kipindi cha Straight Talk Afrika ambacho huwa kinarushwa na Sauti ya Amerika (VOA) kutoka mjini Washington DC nchini Marekani.

Hata hivyo sababu kuu iliyomsukuma Waziri huyo mstaafu kutamka hivyo ni kutokana na mada ambayo iliwasilishwa katika kipindi hicho ambayo iliangazia tija ambayo inaweza kupatikana kwa Bara la Afrika baada ya Wafaransa kufanya uamuzi wa kidemokrasia na kumuingiza madarakani Bw. Francois Hollande.
"Huwezi kumpima mtu kwa matendo yake ila uamuzi na siasa safi hususan demokrasia zenye mantiki kwa Afrika ndizo kimbilio na ufunguo wa maendeleo kwa Afrika;
"Nikiwa huku nilipo (Ubeligiji) nchi ambazo ninaweza kujivunia kuwa na demokrasia ya kweli si kwetu Rwanda... ni Tanzania na ninaamini iwapo wataitukuza (Watanzania) demokrasia hiyo ni fundisho pekee na mfano wa kuigwa katika Bara la Afrika na hata nje ya bara letu," alisema Bw. Twagiramungu.
Hata hivyo baadhi ya wachangiaji wa mada hiyo kutoka sehemu mbalimbali duniani walisema kuwa, nchi za Afrika ikiwemo Tanzania haziwezi kutegemea wahisani kuziendesha ila umefika wakati sasa rasilimali zinazowazunguka kutumika vyema kwa manufaa ya Waafrika.
"Kuchaguliwa kwa Rais mpya nchini Ufarasa kwetu (Afrika) si tija, haijalishi sera zake zinajikita katika Ujamaa au la!...tutakachofanya ni kuendelea kudumisha umoja na ushirikiano, lakini masuala ya uwajibikaji kwa manufaa ya nchi zetu yanatuhusu wenyewe," alisema mmoja wa wachangiaji wa mada hiyo kutoka nchini Nigeria.
Hata hivyo tafiti zinaonesha kuwa mbali na changamoto za hapa na pale demokrasia iliyopo Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kutokana na Watanzania wenyewe kuwa na maamuzi yao pekee bila kulazimishwa na watu ya kuwachagua ikiwemo kuwakataa viongozi ambao wanaona hawawajibiki ipasavyo.
Posted: 11 May 2012 01:01 AM PDT

Posted: 11 May 2012 12:59 AM PDT

Na Jovin Mihambi, Mwanza

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Evarist Ndikillo, amewataka wafanyabiashara nchini kuagiza bidhaa kutoka nchi za nje zenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa na vinavyoendana na uchumi wa nchi ili kila mwananchi aweze kumudu kuvinunua na vitumike kwa muda mrefu.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Bw. Saidi Amanzi, katika hotuba yake aliyoitoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, wakati wa ufunguzi wa duka la kuuza pikipiki na bidhaa zingine zinazotengenezwa na kampuni ya Honda ambalo limefunguliwa na Kampuni ya QM Quality Motors Limited lenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara nchini wamekuwa wakiingiza bidhaa mbalimbali ambazo hazina ubora na nyingi kutoka China.
Alisema kufunguliwa kwa duka hilo la kuuza pikipiki za Honda pamoja na bidhaa zingine ambazo ni jenereta, pampu za kusukumia maji, injini za kuendeshea mitumbwi limekuwa ni mkombozi kwa wananchi wa kanda ya Ziwa na mikoa mingine ya jirani.
Naye Meneja mauzo na Masoko wa kampuni ya QM Quality Motors Limited, Bw.Sudhir Borgaonkar, alisema bidhaa za kampuni yake ikiwemo pikipiki za Honda ambazo alisema zinauzwa bei nafuu ikilinganishwa na zile za kutoka China.
Posted: 11 May 2012 12:58 AM PDT

Diwani wa Kata Vijibweni Bw.Selemani Methew akimpa pole mzazi aliyejifungua watoto mapacha Bi.Robi Wambura katika Hospitali ya Vijibweni Wilaya Temeke, Dar es Salaam juzi, (Picha na Heri Shaaban)
Posted: 11 May 2012 12:52 AM PDT

Na Mwali Ibrahim

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Zimbabwe Rosemary Mugdza amesema kikosi chake kipo kamili kukabiliana na timu ya Taifa ya wanawake 'Twiga Star' katika mchezo wake wa kirafiki wa kimataifa utakaochezwa kesho katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, kocha huyo alisema, walikuwa wakisaka timu ya kucheza nayo ikiwa ni kwa ajili ya maandalizi yao na mechi ya Nigeria ambapo waliamua kuichagua Tanzania kutokana na uwezo mkubwa waliokuwa nao.
"Twiga ni timu nzuri na yenye uwezo na ndio maana tuliona ni timu ya kuchuana nayo tukiwa katika maandalizi ya mchezo wetu huo kwani tunaimani tutapata mazoezi ya kutosha," alisema.
Aliongeza kuwa kwa upande wa maandalizi wamejiandaa vya kutosha hivyo wanaimani kubwa ya kufanya vizuri katika mchezo huo ili kujiweka katika nafasi nzuri katika mchezo wao ujao.
Kwa upande wake Ofisa Habari wa Shirikisho la soka nchini (TFF) Bonifance Wambura akizungumza kwa niaba ya kocha wa Twiga, Boniface Mkwasa alisema hata kwa upande wao mchezo huo utakuwa ni mchezo mmoja wa kimataifa ambao ni kwa ajili ya mechi ya maandalizi ya kuivaa Ethiopia Mei 26, mjini Adis Ababa.
"Huu ni mchezo wa kwanza  wa kimataifa wa kirafiki kwa ajili ya kujiweka sawa kwani timu hii itacheza mchezo mwingine wa kirafiki Mei 20 ambapo kwa sasa tunatafuta timu ya kucheza nayo," alisema.
Alisema, timu hiyo ilikuwa mkoani Mwanza ikimalizia ziara yake ya kucheza michezo mbalimbali ya kujipima nguvu ambapo sambamba na mkoa huo pia walicheza mchezo mmoja mkoani Dodoma.
Wambura alisema, kwa upande wao wako tayari kukabiliana na timu hiyo kwani wanaijua vizuri walishawahi kuchuana nayo katika mashindano ya All African Games mwaka jana.
Alitaja viingilio katika mchezo huo kuwa  VIP A ni sh. 10,000, VIP B sh. 5,000 na viti vingine vikiwa ni sh. 1,000 ambapo wanaimani mashabiki watajitokeza kwa wingi kuisapoti timu hiyo..
Posted: 11 May 2012 12:47 AM PDT


Na Stella Aron

WANANCHI wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima afya zao bure ili kuzuia na kutibu magonjwa mbalimbali yanayoangamiza jamii kwa asilimia kubwa.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Agakhan Bi. Loveluck Mwasha, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya siku ya uuguzi duniani, ambayo huadhimishwa Mei 12, kila mwaka.
Alisema katika kusherehekea siku hiyo uongozi wa hospitali hiyo umeazimia kutoa huduma ya upimaji bure kwa magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu kesho katika ukumbi wa Mlimani City.
"Tumechagua magonjwa hayo kutokana na watu wengi kupoteza maisha kwa kutofahamu dalili za magonjwa hayo kwa kushindwa kupata huduma za matibabu, " alisema Bi.Mwasha.
Bi.Mwasha alisema siku hiyo watatoa ushauri mbalimbali kwa watu warefu au wafupi na wenye uzito mkubwa namna ya kupunguza uzito ili kuepukana na ugonjwa wa shinikizo la damu na magonjwa mengine nyemelezi.
Alisema wananchi watakaogundulika kuwa na magonjwa hayo watatakiwa kwenda kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kupata huduma zaidi, ambapo hivi sasa kuna idadi kubwa ya watu wanaougua magonjwa hayo lakini hawajitambui.
"Kwa wastani wa mwezi Agakhan tunapokea wagonjwa 50 wa kisukari ambao hupata tiba na kurejea majumbani mbali ya wale wanaolazwa," alisema Bi. Mwasha.
Muuguzi huyo alisema kabla ya kusherehekea siku hiyo uongozi wa hospitali hiyo jana ulitoa mafunzo kwa wauguzi wake namna ya kufuata maadili ya kazi na utoaji wa chanjo.
"Tumetoa mafunzo kwa wauguzi wetu ili waweze kukumbuka na kufuata maadili ya kazi zao na utoaji wa ushauri kwa jamii kufahamu umuhimu wa chanjo, " alisema.
Posted: 11 May 2012 12:46 AM PDT
Diwani wa kata ya kilosa wiliya ya Nyasa Bw. Issa Mustapha (kulia) akimuekeza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Bw.Said Mwambungu (wa tatu kulia) nama ilivyonusurika kuuawa na wananchi wa kata hiyo baada ya kuwakatalia kushiriki kuongoza zoezi la kutoa uchawi kwa watu waliotuhumiwa kuhusika na vitendo vya kishirikina katika eneo hilo, wengine ni wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo.Picha na kassian Nyandindi
Posted: 11 May 2012 12:31 AM PDT


Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya kupatikana na simu gerezani inayomkabili  aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BoT), Bw. Amatus Liyumba, kutokana na hakimu anayesikiliza kesi hiyo kutokuwepo mahakamani.
Wakili wa Serikali Bi.Elizabert Kaganda, alisema jana mbele ya hakimu Bi.Devota Kisoka, wakati kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo. Alisema Bw.Suwart Sanga anaumwa hivyo ameshindwa kufika mahakamani.
Kutokana na hali hiyo kesi hiyo imepangwa kuendelea kusikilizwa Julai 2, mwaka huu. Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa, Julai 27, mwaka jana, Bw.Liyumba akiwa mfungwa kwenye gereza la Ukonga anadaiwa kukutwa na kifaa kilichozuiliwa kisheria ambacho ni simu aina ya Nokia, rangi nyeusi yenye laini namba 0653004662 na IMEI 356273/04/276170/3.
Posted: 11 May 2012 12:29 AM PDT

Posted: 11 May 2012 12:27 AM PDT


Na Elizabeth Mayemba

KAMPUNI ya Simu za mikononi ya Airtel jana ilizindua awamu ya pili ya mpango kabambe wa mpira wa miguu nchini Airtel Rising, ambao nia yake ni kutafuta na kukuza vipaji vya mchezo huo kutoka ngazi ya chini kabisa mpaka ya taifa.
Michuano ya Airtel Rising Stars iliyozinduliwa na mchezaji wa zamani wa Manchester United Quinton Fortune, itaanza kutimua vumbi Mei 24 mwaka huu, kutoka mikoa sita, fomu za usajili zinapatikana kwenye makao makuu ya ofisi za Airtel Lindi,Mbeya,Arusha,Kinondoni, Ilala na Temeke.
Awamu ya kwanza ya mpango huu ilifanyika mwaka jana na kupata mafanikio makubwa, lengo likiwa ni kuvipika vipaji vinavyochipukia chini ya umri wa miaka 17, nafasi ya kuonyesha vipaji vyao kwa makocha waliobobea pia kupata nafasi ya kuendeleza vipaji vyao.
Akizungumza Dar es Salaam jana kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Sam Elangallor alisema, mafanikio ya mwaka jana yanaonesha mpira wa miguu una uwezo wa kuunganisha makabila mbalimbali na pia kuleta hamasa kwa jamii ya chini hadi taifa.
"Mwaka jana zaidi ya timu 11,000 Afrika zilijiandikisha kushiriki kwenye michuano hii kuanzia kwenye mtoano na kuchagua wachezaji ambao waliunda timu zilizoshiriki kwenye ngazi ya mkoa, ushiriki huu mkubwa ulituonesha ya kwamba tuko kwenye njia sahihi, na ndio maana tuna hamasa kubwa na awamu hii ya pili kwa mwaka huu," alisema Elangallor

Alisema kama ilivyokuwa kwa mwaka jana, mpango huu utaanzia ngazi ya mkoa na taifa na kufuatiwa na kliniki ya soka ya kimataifa chini ya wakufunzi kutoka klabu ya Manchester United ya Uingereza, kwa mwaka huu kutakuwa na mashindano ya siku nne ya timu bingwa kutoka kila nchi itakayoshiriki kushindania taji jipya la Airtel Rising Stars African Champion.
Kwa mwaka huu michuano hii imezinduliwa na mchezaji wa zamani wa Manchester United Quinton Fortune, mchezaji aliyesajiliwa na kocha Sir Alex Ferguson mwaka 1999 akitokea klabu ya Atletico Madrid wakati huo akiisaidia timu yake kushinda vikombe vitatu.

Raia huyo wa Afrika kusini aliweza kuzoea haraka mazingira wa Uingereza na kuweza kupata namba ya kudumu kwenye kikosi cha Ferguson kama winga wa kulia,kiungo wa kati na mshambuliaji, akiwa Man U Fortune aliiwezesha timu yake kushinda taji la FA mwaka 2003.

Posted: 11 May 2012 12:25 AM PDT

Mchezaji wa zamani wa Klabu ya Manchester United ya Uingereza Quinton Fortune, akipiga mpira kuashiria uzinduzi rasmi wa michuano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya Airtel Rising Stars. Uzinduzi huo ulifanyika jana,  kwenye Hoteli ya Sea Clif, jijini Dar es Salaam.(Na Mpigapicha Wetu)

Posted: 11 May 2012 12:22 AM PDT

Na Heri Shaaban

UONGOZI wa Kata Vijibweni iliyopo Kigamboni wamemuagiza Mganga Mkuu Zahanati ya Vijibweni, Bi.Rukia Msumi, kuagiza walinzi wa zahanati hiyo kuacha geti wazi ili wagonjwa waweze kuingia baada ya kutokea tukio la mjamzito kujifungulia getini.

Agizo hilo lilitolewa juzi wakati wa ziara ya kushtukiza iliyofanywa na diwani huyo, Bw. Suleiman Methew akiongozana na wenyeviti wake. Alikemea vikali kitendo cha walinzi kukataa kufungua milango hadi mjamzito akajifungulia nje.
Bw. Methew alimtaka mganga mkuu awaagize walinzi wa hospitali hiyo kuruhusu magari kuingia ndani wakati wote.

Bw.Methew alisema baada ya kupata malalamiko ya makosa  yanayofanywa na walinzi wa zahanati hiyo kwa muda mrefu yeye kama kiongozi amekerwa.
"Wananchi wangu kufanyiwa vitendo vya aina hii sijaridhika navyo, kuanzia leo naomba magari yote ya wagonjwa yaingie ndani kama vituo vingine vya afya wanavyofanya pindi wanapopokea wagonjwa," alisema Bw.Methew.
Alimtaka mganga huyo kusimamia suala hilo ili vitendo vya aina hiyo visijirudie.
Kwa upande wake Mganga Mkuu, Bi.Rukia Msumi, alisema taarifa hizo zilimfikia na alitoa onyo lakini kampuni hiyo ya ulinzi ilipuuzia.
Posted: 11 May 2012 12:20 AM PDT

Askari wa doria wakikagua pikipiki baada ya kuzikamata kwenye makutano ya Barabara za Bibi Titi Mohamed na Uhuru, Dar es Salaam jana. (Picha na Charles Lucas)
Posted: 11 May 2012 12:17 AM PDT

Na Queen Lema, Arusha 


WAFANYAKAZI wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha wamedai afya zao zipo hatarini kutokana na kukosa choo na kusababisha mazingira ya ofisi hiyo kutapakaa maji machafu.

Suala hilo limekuwa likilalamikiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kupatiwa ufumbuzi huku wafanyakazi hao wakiendelea kukumbwa na adha ya harufu mbaya.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa sharti la kutonukuliwa majina yao kwenye vyombo vya habari, walisema adha hiyo imekuwa ikiwakumba zaidi watumishi waliopo chini ya jengo hilo la ofisi ya mkuu wa wilaya.

Mmoja wa watumishi hao alisema watumishi waliopo ghorofa ya juu wamekuwa wakimwaga maji na kusababisha choo cha chini kuzagaa uchafu.

"Kama mnavyoona hii hali inatisha kwani ni muda mrefu choo hiki kimeziba wenzetu wakimwaga maji huko juu, uchafu wote unatoka," alisema mtumishi huyo.

Wafanyakazi hao kutoka idara mbalimbali za serikali katika jengo hilo, walidai kuwa wamekuwa wakipata shida kutokana na kukosa sehemu ya kujisaidia na kulazimika kwenda umbali mrefu kutafuta huduma hiyo ya choo.

Alidai taarifa ya ubovu wa choo hicho walitoa kwa viongozi akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Bw.Raymond Mushi, bila kupatiwa ufumbuzi. Kukosekana kwa huduma ya choo katika jengo hilo kumewakumba watumishi wa idara mbalimbali za Serikali.

Akizungumzia hali hiyo Katibu Tawala wa Wilaya, Bw. Emi Lyimo, alikiri kupata taarifa juu ya ubovu wa choo hicho, lakini alidai kuwa suala hilo lipo juu yake na tayari taarifa walishazifikisha ofisi kunakohusika.

Alisema hali ya ubovu wa choo hicho ni ya siku nyingi hata Mkuu wa Wilaya anaifahamu.

Kwa upande wa Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Bw. Everin Itanisa, alipoulizwa kuhusu ubovu wa choo katika jengo hilo alidai kuwa taarifa hizo anazo na kilichokwamisha ukarabati ni ukosefu wa fedha.

Alisema ukarabati wa choo hicho unahitaji gharama kiasi cha sh.milioni 12 na ofisi yake haikuwa na fedha isipokuwa wamepata nusu baada ya kuamua kuchangishana katika idara zote za ofisi.
Posted: 11 May 2012 12:14 AM PDT

Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Homes Expo, inayojishughulisha na makazi, Bw. Zenno Ngowi, akisoma taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), Dar es Salaam jana, kuhusu Maonesho ya Sekta ya Nyumba yatakayofanyika, Dar es Salaam, mwezi juni, mwaka huu. kushoto ni Mratibu wa Matukio wa taasisi hiyo Bw. Richard Mvula na Meneja Masoko Bi. Nice Chande. (Picha na Charles Lucas)
Posted: 11 May 2012 12:10 AM PDT

Darlin Said na Radhia Adam

KAMPUNI ya Mobile Ticketing LTD imezindua huduma mpya ya kukata tiketi za usafiri wa mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani inayojulikana kwa jina la "Tiketi popote" kwa kutumia simu za mikononi ambapo mteja atapata huduma ya tiketi popote alipo.

Huduma hiyo inategemewa kutumika kwa mikoa yote ya Tanzania ambapo kwa sasa huduma hiyo itaanza kutolewa katika mikoa ya Dar es Salaam,  Mwanza, Arusha, Tabora, Mtwara, Kilimanjaro, Lindi, Morogoro pamoja na nchi za jirani.
Huduma hiyo imeanza kutumika rasmi mara baada ya kuzinduliwa na kwa sasa inahusisha huduma za M-pesa, Airtel money pamoja na Easypesa.

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bw.Abert Muchuruza, alisema wameanzisha kampuni hiyo kwa lengo la kuondoa usumbufu wanaoupata wasafiri pindi wanapoenda kukata tiketi ikiwemo kuuziwa tiketi bandia, kuzidishiwa nauli na wapiga debe na kuuziwa tiketi za magari yasiyo safiri.
Huduma hiyo inatoa taarifa zote za mteja ikiwemo namba ya gari, namba ya siti pamoja na jina la gari atakalosafiri nalo abiria na ikitokea tatizo, msafiri anajulishwa.
Mbali na huduma ya tiketi kwa mabasi kampuni inatarajia kutoa huduma kwa vyombo vingine vya usafiri kama treni na meli.
Posted: 11 May 2012 12:08 AM PDT

Askari wa usalama Barabarani, akimuamuru dereva wa daladala namba T 225 BRD, kuegesha gari hilo kando ya barabara ya Azikiwe, Posta Dar es Salaam jana, baada ya kukiuka kanuni za usalama barabarani. (Picha na Charles Lucas)
Posted: 11 May 2012 12:04 AM PDT


Na Elizabeth Mayemmba

TIMU ya soka ya Simba imewasili salama jijini Khartoum, Sudan, jana usiku majira ya saa 5:49 ikitokea jijini Nairobi, nchini Kenya tayari kwa pambano lake la Kombe la Shirikisho (CAF) dhidi ya Al Ahly Shendi, ambapo walipokelewa na uongozi wa Chama cha Soka cha Sudan (SFA) lakini
Hata hivyo timu hiyo ilikiona cha moto kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoumbaada baada ya kutua kwa kuwekwa uwanjani hapo kuanzia saa sita usiku hadi saa saba na nusu usiku kwa kisingizio cha kumalizia taratibu za kiulinzi na kiusalama uwanjani hapo.

Kiongozi  wa SFA alipoulizwa kwanini wachezaji wanazidi kuwekwa uwanjani hapo wakati ni usiku wa manane , kiongozi huyo alijibu kwa mkato kuwa"Hata kwenu pia mlifanya hivihivi.”

Simba walitakiwa kuingia Sudan saa mbili usiku lakini walichelewa kufika kutokana na hitilafu iliyokuwepo katika ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) iliyopaswa iwachukue kutoka Nairobi.

Msafara huo wa Simba wa wachezaji 19 na viongozi wanane ulifikia katika Hoteli ya Shariqa lakini jana timu hiyo ilitakiwa kusafirishwa kwenda katika mji wa Shendi uliopo umbali wa Kilomita 150 kutoka Khartoum. Mechi ya Shendi na Simba itapigwa Jumapili saa mbili usiku katika Uwanja wa Shendi wenye uwezo wa kuchukua washabiki 10,000.

Kocha Mkuu wa Simba, Profesa Milovan Cirkovic alisema jana asubuhi kikosi chake hakikufanya mazoezi ya aina yoyote lakini jioni walifanya kama kawaida.

"Kuna uwezekano mkubwa wa mazoezi ya leo (jana) yakafanyika usiku muda ambao timu tutacheza ili wachezaji wazoee hali hiyo," alisema Milovan

Timu zote mbili, Simba na Shendi zinaweza kucheza kwa mara ya kwanza katika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la CAF. Simba iliweza kufika fainali ya michuano hii mwaka 1992 lakini wakati huo mfumo wa sasa wa hatua ya makundi katika hatua ya nane bora ulikuwa haujaanza kutumika.
Posted: 11 May 2012 12:02 AM PDT
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Robin Goetzsche (kulia) na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Leodgar Tenga (kushoto) wakisalimiana baada ya kusaini mkataba wa kuiwezesha TBL kuwa mdhamini mkuu wa Timu ya Taifa-Taifa Stars kwa miaka mitano ijayo kupitia Bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager. Katikati ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro premium Lager, George Kavishe. (Na Mpigapicha Wetu)
Posted: 10 May 2012 11:59 PM PDT


Na Elizabeth Mayemba

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro imeingia mkataba wa kuidhamini timu ya taifa, Taifa Stars kwa kipindi cha miaka mitano wenye thamani ya sh.bilioni 23 ambazo zitatumika katika kuimarisha timu hiyo ambayo inapeperusha bendera ya Taifa.

Uzinduzi huo ulifanyika katika hoteli ya Kempinski, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wote wakuu wa TFF, TBL na wadau mbalimbali.

Awali Stars tangu mwaka 2006 ilikuwa ikidhaminiwa na kampuni ya Serengeti (SBL).

Akizungumza katika hafla hiyo ya kutiliana saini, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Robin Goetzsche alisema udhamini huo utafungua mwanga mpya katika medani ya soka nchini Tanzania.

“Tunasaini mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya dola za Marekani milioni 10 sawa na sh.bilioni 23 za Tanzania utalifikisha soka letu Katika Kilele cha Mafanikio na kutupa kila sababu ya kujivunia kilicho chetuTuna matarajio makubwa sana na timu ya taifa kwani tunaamini kuwa ina uwezo wa kufanya maajabu, na kama nilivyosema awali, hili ni pambazuko la kuelekea mafanikio.

"Uwekezaji wetu umelenga katika kuhakikisha kambi za mazoezi zinaimarishwa, wachezaji watalala katika hoteli zenye ubora wa juu zenye zaidi ya ngazi tatu zilizo na bwawa la kuogelea na vifaa vya mazoezi, vifaa vinaboreshwa na pia vijana watapata fursa za kucheza mechi nyingi za kirafiki ili wajipime nguvu na kupata uzoefu zaidi na timu zinapata basi jipya la kisasa," alisema

Alisema udhamini wao utasaidia katika ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kisasa vya michezo, mafunzo kwa wafanyakazi wa TFF ndani na nje ya nchi, uendeshaji wa tovuti ya TFF, Semina na mikutano ya utawala bora.

Alisema wanaamini kabisa juhudi madhubuti zikiwekwa kwa kushirikiana na TFF na wadau wengine, malengo ya kuifanya Timu ya Taifa ishinde mechi zake zote yatatimia.
Goetzsche alisema TFF peke yake au mdhamini peke yake hawezi kuifanya timu ishinde lazima tujivunie kuwa na timu bora na kuimba nyimbo za ushindi kila wakati.

No comments:

Post a Comment