Wananchi
wa Afrika ya Kusini wakishuhudia mwili wa rais Mstaafu Hayati Mzee
Nelson Mandela ulipokuwa ukitoka Ikulu. Picha na mpigapicha wetu
……………………………………………………………………………..
Pretoria. Maelfu
ya wananchi wa Afrika Kusini wameshindwa kutoa heshima za mwisho kwa
mwili wa Rais wa Kwanza mzalendo wa nchi hiyo, Nelson Mandela kutokana
na muda uliopangwa kumalizika.
Kuanzia Jumatano wiki hii hadi
jana, mwili wa Mandela aliyefariki dunia Desemba 4 mwaka huu, ulikuwa
ukiwekwa katika Ikulu ya Pretoria, iliyopo ndani ya Majengo ya Umoja
(Union Buildings), kila asubuhi kwa ajili ya wananchi kutoa heshima za
mwisho.
Jana ilikuwa siku ya mwisho ya
utoaji wa heshima hizo na hadi muda uliowekwa ulipokwisha saa 11:30
jioni, kulikuwa na maelfu ya watu waliokosa fursa ya kumuaga mpendwa wao
huyo.
Dalili za idadi kubwa ya watu
kukosa nafasi hiyo adhimu zilianza kuonekana Jumatano na baadaye juzi
Alhamisi kwani hadi muda wa kufunga ulipofika jioni, maelfu ya watu
walirejea nyumbani bila kupata fursa ya kuaga.
Jana mchana, Serikali ilitoa
taarifa kwamba kwa kuzingatia idadi ya watu waliojitokeza kutoa heshima
zao za mwisho, ilikuwa vigumu kwa watu wote kufikiwa.
“Hatuwezi kuahidi kwamba kila
mtu ambaye amejipanga hivi sasa kwenye mstari atapata nafasi ya kufika
katika Majengo ya Umoja, tunawaomba wananchi wasiende tena huko,”
ilisema taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya
Serikali (GICS) jana na kuongeza:
“Tunawashukuru sana wananchi kwa
kujitokeza, lakini sasa tunawaomba wale ambao hawakuweza kupata fursa
ya kutoa heshima zao za mwisho, wafanye hivyo kwa kutumia njia zao
wenyewe.”
Waziri katika Ofisi ya Rais,
Collins Chabane, alisema kuwa hakuna jinsi ya kuwasaidia watu
watakaokosa fursa ya kuaga na kwamba Serikali pamoja na familia
wamejitahidi kiasi cha kutosha.
Serikali ilisitisha utaratibu wa
usafiri kwa watu waliokuwa wakienda kuaga kuanza saa 8:00 mchana hali
iliyozua mvutano baina ya maelfu ya waombolezaji na vyombo vya usalama.
Wengine waliokuwa wameishapanda
kwenye mabasi na kufika Ikulu waliambiwa kwamba hawataweza kufikiwa hali
iliyozidisha manung’uniko.
Ulinzi ni mkali na Rais Jacob
Zuma jana aliliarifu Bunge kwamba amewaajiri kwa siku 15 Askari 11,894
kutoka Jeshi la Afrika Kusini (SANDF), ili wasaidiane na polisi katika
ulinzi na usalama wakati wa maombolezo na mazishi ya Mandela.
Wakesha viwanjani
Maelfu
ya wananchi walikuwa katika makutano ya barabara za kuelekea Ikulu
kuanzia saa 10 alfajiri na wengine walisema walilala jirani na eneo hilo
ili waweze kupata fursa ya kumuaga Mandela.
Miongoni mwa waliotoa heshima za
mwisho ni ujumbe kutoka Venezuela, ambao ulimzawadia Mandela upanga wa
dhahabu na kumkabidhi mjukuu wake wa kwanza, Mandla.
Mandla kwa siku tatu mfululizo
amekuwa akiketi pembeni mwa jeneza la babu yake, wakati waombolezaji
wakiaga na wakati wote ameonekana mwenye mawazo mengi na huzuni kubwa.
Ndani ya kibanda ambamo mwili wa
Mandela uliwekwa kulikuwa na ukimya, ambao mara kadhaa ulivunjwa na
kelele za vilio na majonzi kutoka kwa watu walioshindwa kujizuia.
Polisi na wasaidizi mara kadhaa
walikuwa wakiwasaidia wale waliozidiwa au wale walioanguka baada ya
kuona sura ya marehemu Mandela.
Mapema asubuhi, wengi
walijipanga pembezoni mwa barabara kutoka Hospitali ya Jeshi hadi Ikulu,
wakiimba nyimbo za kumsifu Mandela na wakati msafara uliokuwa
ukisindikiza mwili wake ulipokuwa ukipita, wengine walisikika wakisema;
“Siyabinga Tata Madiba…” (wakimaanisha ahsante Baba Madiba).
Wengine walionekana wakiwa
wamekwea juu ya miti ili kuweza kuuona vizuri msafara huo wa magari
zaidi ya 40, huku baadhi ya watu waliokuwa kazini wakionekana kutoka na
kupungia msafara huo.
Wakati
huo helikopta za SANDF na polisi zilikuwa zikizunguka katika anga la
Jiji la Tswane ndani ya Pretoria na wakati mwili wa Mandela ulipoingizwa
Ikulu zilizunguka eneo hilo kwa zaidi ya nusu saa kabla ya kuondoka.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment