Abiria
37 waliokuwa wamesafaria ndege ya Shirika la Precision Air, akiwamo
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, jana walinusurika kifo, baada ya
magurudumu manne ya ndege hiyo kupasuka ilipokuwa ikitua katika Uwanja
wa Ndege wa Arusha.
………………………………………………………………………..
Arusha. Abiria
37 waliokuwa wamesafaria ndege ya Shirika la Precision Air, akiwamo
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, jana walinusurika kifo, baada ya
magurudumu manne ya ndege hiyo kupasuka ilipokuwa ikitua katika Uwanja
wa Ndege wa Arusha.
Tukio hilo la aina yake,
lilitokea saa 6:15 mchana, wakati ndege hiyo, ikitua kutoka jijini Dar
es Saalam, ikiwa na abiria hao 37, marubani wawili na wahudumu wawili.
Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza hakuna majeruhi aliyeripotiwa.
“Hadi sasa hali ni shwari, ndege
iliweza kusimama licha ya kupasuka magurudumu. Kiutaratibu uchunguzi
umeanza kufanywa na wataalamu husika,”alisema Kamanda Sabas.
Ofisa Mwendeshaji wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege nchini (TCAA), wa Uwanja wa Ndege Arusha, Roland
Mwalyambi, alisema kuwa katika tukio hilo, hakuna abiria aliyejeruhiwa
licha ya kupata mshtuko mkubwa.
“Uchunguzi wa ajali hii umeanza, lakini hakuna majeruhi, abiria wote walifanikiwa kushuka salama,”alisema Mwalyambi.
Alisema ndege hiyo, kama ingetua
salama ilitarajiwa kusafiri kurejea Dar es Salaam kupitia Zanzibar,
lakini abiria waliotarajia kusafiria ndege hiyo, walipelekwa Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro ili kuendelea na safari.
Katika ndege hiyo, pia kulikuwa
na maofisa mbalimbali wa Serikali na Jeshi la Wananchi, ambao leo
wanatarajia kuhudhuria sherehe ya kutolewa kamisheni kwa maofisa wa
jeshi katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli(TMA), ambapo Rais
Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Tukio hilo la ndege kupata ajali
katika uwanja huo ni la pili kutokea mwaka huu, kwani mapema mwaka huu,
mfanyabiashara maarufu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha, Babu Sambeki
alipata ajali pia katika uwanja huo, wakati akijiandaa kutua na ndege
yake.
Mfanyabiashara huyo, alifariki
papo hapo baada ya moja ya mabawa ya ndege kunasa katika matawi ya mti
jirani na uwanja huo. Hata hivyo, taarifa ya ajali hiyo hadi sasa
haijawekwa hadharani.
Kukosekana
kwa taa katika uwanja huo, ambao umekuwa ukitumiwa na ndege nyingi
ndogo hasa za watalii, imekuwa ni kero kubwa na mara kadhaa safari
zimeahirishwa kutokana na tatizo hilo.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment