Posted: 02 Dec 2013 10:09 PM PST
- CHADEMA KIGOMA YASHTUKIA MCHEZO MCHAFU
- HOFU YA KUTOKEA VURUGU YATANDA MAJIMBONI
Na Mwajabu Kigaza, Kigoma
Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani Kigoma, kimesitisha ziara
ya Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa, Dkt. Wilbrod Slaa, ambayo
ilipangwa kufanyika mkoani humo kuanzia Desemba 5 hadi 13 mwaka huu,
kutokana na hofu ya usalama miongoni mwa wanachama wake.
Mwenyekiti
wa chama hicho mkoani humo, Jafari Kasisiko, aliyasema hayo jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa, usalama katika
baadhi ya majimbo mkoani humo ni mdogo sana.
Alisema
kutokana na hali hiyo, wameona ni bora ziara hiyo isitishwe kwanza ili
kuepusha machafuko yaliyoandaliwa na wanachama dhidi ya Dkt. Slaa kama
atafika mkoani humo.
“Uamuzi
wa kusitisha ziara hii umefikiwa katika Kikao cha Baraza la Uongozi
mkoani hapa kilichofanyika Desemba Mosi, mwaka huu na kushirikisha
viongozi wa majimbo mengine.
“Majimbo
haya ni Kigoma Mjini, Kaskazini na Kusini ambao kwa pamoja walielezea
uwepo wa njama za kuhujumu ziara hii ili kumdhalilisha Dkt. Slaa,”
alisema.
Aliyataja
majimbo yaliyodaiwa kuchafuka kisiasa kutokana na maamuzi ya Kamati Kuu
ya CHADEMA kumvua nyadhifa za uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa
chama hicho Bara, Bw. Zitto Kabwe kuwa ni Kigoma Mjini, Kaskazini na
Kusini, wakati ambapo majimbo ya Buhigwe, Kasulu, Muhambwe na Buyungu
pia hali ya usalama imedaiwa kuwa ya mashaka.
Akizungumzia
msimamo wa chama hicho mkoani humo kuhusu uamuzi wa Kamati Kuu kumvua
uongozi Bw. Kabwe kwa madai ya kutaka kukisaliti chama, alisema kikao
hicho kilikuwa halali.
“Hatua
zote za kumvua uongozi Bw. Kabwe na wenzake Dkt. Kitila Mkumbo na Bw.
Samson Mwigamba, zilifuatwa sasa kama anadhani ameonewa, ana haki ya
kukata rufaa Baraza Kuu.
“Ziara
ya Dkt. Slaa hapa Kigoma, haina uhusiano na maamuzi ya Kamati Kuu kwani
ilipangwa muda mrefu na kusitishwa kutokana na vikao vya Kamati Kuu,
lengo la ziara hii ni maandalizi ya uchaguzi ujao ngazi za chini,”
alisema.
Aliwataka
baadhi ya wanachama wanaoendesha vitendo vya vurugu na kuhujumu
miundombinu ya chama kuacha kufanya hivyo kwani ni kinyume cha maelekezo
ya chama kwani palipo na vurugu hakuna haki.
Baadhi
ya wanachama wa chama hicho kutoka majimbo yaliyotajwa kuwa na vurugu,
walikutana Mjini Kigoma katika moja ya kumbi za mikutano kupinga ujio wa
Dkt. Slaa, Desemba 5 mwaka huu.
Akisoma
tamko la wanachama hao, Fanuel Sindika alisema wameikataa ziara hiyo
kwa sababu CHADEMA kimekuwa kikiwaonea baadhi ya viongozi hasa kutoka
mikoa ya Magharibi na wapo tayari kufanya vurugu ili kumdhalilisha
kiongozi huyo.
Alisema hawakubaliani na maamuzi yaliyotolewa na Kamati Kuu dhidi ya Bw. Kabwe ambayo hayajazingatia haki kwa mujibu wa katiba.
Aliongeza
kuwa, kwa muda mrefu chama hicho kimekuwa na mgogoro unaotokana na hofu
ya madaraka katika nafasi ya Mwenyekiti wa chama ambayo inadaiwa
kuwaniwa na Bw. Kabwe akisaidiwa na rafiki zake kwenye kampeni ili
kuhakikisha anashinda kiti hicho.
Hivi
karibuni, baadhi ya vijana kutoka Tawi la Mwandiga, Jimbo la Kigoma
Kaskazini, walifanya maandamano ya pikipiki na kuburuza bendera
barabarani, kuchoma kadi, bendera na kuvunja bango la Tawi la Msingi
katika kijiji hicho
No comments:
Post a Comment