WAHITIMU wa Kidato cha sita nchini wameaswa kuwa waadilifu na
wazalendo ili hatimaye taifa liweze kupata viongozi bora na raia wema
katika jamii.
Rai hiyo imetolewa na Kamishna wa Fedha na Utawala wa Magereza Gaston
Sanga akiongea kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza
nchini katika mahafali ya kwanza ya Kidato cha sita ya Shule ya Bwawani
Sekondari iliyopo Mkoani Pwani.
“Nadhani wote ni mashahidi kwa namna Serikali ya Awamu ya Tano
inavyowahudumia wananchi kwa kasi na kiwango cha kuridhisha. Hivyo
mkipata kazi nawasihi mkawajibike kwa kasi, uadilifu na mkawe wazalendo
kwa taifa”. Alisema Kamishna Sanga.
Kamishna Sanga ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wameunga
mkono kwa vitendo juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya
Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Aidha, Afande Sanga ameahidi kuwa Uongozi wa Jeshi la Magereza kwa
kushirikiana na Bodi ya shule hiyo utaendelea kuzitafutia ufumbuzi
changamoto mbalimbali zinazozikabili shule hiyo kadri uwezo wa kifedha
unavyopatikana.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari Bwawani, Kamishna Msaidizi
wa Magereza, Emmanuel Lwinga alipokuwa akitoa taarifa fupi kwa mgeni
rasmi katika mahafali hayo amesema kuwa shule yake ni miongoni mwa shule
bora nchini ambazo zinafanya vizuri kitaaluma na masuala mengineyo
yasiyoyakitaaluma.
Aliongeza kuwa katika mitihani mbalimbali waliyofanya wanafunzi hao
wa kidato cha sita wamekuwa na matokeo mazuri kutokana na mazingira
mazuri ya kujisomea, ushirikiano mzuri wa walimu pamoja na kuimarishwa
kwa miundombinu muhimu ya kujifunzia.
“Afande mgeni rasmi wanafunzi wahitimu 13 wa leo tuna hakika kuwa
watatuletea matunda mazuri kutokana na mwelekeo waliouonesha katika
mitihani ya ndani na nje ya shule waliyoifanya”. Alisema Mkuu wa Shule
Lwinga.
Shule ya Sekondari Bwawani inamilikiwa na Jeshi la Magereza,
ilianzishwa Mwaka 1978 kwa lengo la kutoa elimu ya Sekondari kwa
Watumishi wa Magereza ambapo hivi sasa shule hiyo inatoa elimu kwa
vijana wa kike na kiume kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini kuanzia
kidato cha kwanza hadi cha Sita.
No comments:
Post a Comment