TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Wednesday, January 18, 2012

Tanzia ya Maggid Mjengwa kwa marehemu Regia Mtema:Regia ameondoka, ametuachia daraja


Ndugu zangu, JUMATANO hii ya leo kuna kusanyiko kubwa la watu kule Ifakara. Ni WaTanzania wanaoshiriki kumsindikiza kwenye safari yake ya mwisho, ndugu yetu mpendwa, Regia Estelatus Mtema. Ni Jumatano hii ya leo, WaTanzania kwa mamilioni, nao, kwa kuelekeza fikra zao kwa Regia, wanashiriki kumsindikiza ndugu yetu Regia Mtema kwenye safari yake ya mwisho hapa duniani. Katika maisha kuna visivyoshikika,visivyogusika, lakini vipo. Hisia, kwa mfano, zipo na zinaishi. Jumatatu usiku ya wiki hii nilifika nyumbani kwa wazazi wa Regia pale Tabata- Chang’ombe. Nilikwenda kutoa pole kwa wafiwa. Regia alikuwa ni mmoja wa rafiki na dada zangu. Pale Tabata nilimwambia Remija, pacha wa Regia, kuwa niliongea kwa simu na Regia mara ya mwisho Jumapili iliyopita. Remija akanijibu; ” Nilikuwa nae wakati mkiongea!” Ndio, mazungumzo yangu ya mwisho na Regia yalihusu ombi langu la yeye Regia, kwenye siku ya kutoa tuzo ya washindi wa mchakato wa kumtafuta mbunge bora kijana kwa mwaka 2011, mchakato ulioendeshwa na mtandao wangu wa kijamii wa Mjengwablog. com, atoe mada ya nusu saa juu ya nafasi ya mwanamke katika kushiriki uongozi na changamoto zake. Kwamba mada hiyo ivuke mipaka ya siasa za vyama. Ilenge kwenye kuwajengea ari na moyo wa kujiamini wanawake vijana wa nchi hii. Regia alinikubalia ombi langu. Ni Regia Mtema ambaye pia alipendekezwa na wadau wa mtandao wangu wa kijamii kushiriki na hatimaye kushika nafasi ya pili katika mchakato husika. Ni kwenye kundi la wanawake akiwa nyuma ya Halima Mdee. Nafasi ya tatu ilishikwa na Esther Bulaya. Na hapa naungana na mwanasiasa kijana Nape Nnauye aliyesema; Regia Mtema alikuwa ni daraja kwa vijana bila kujali tofauti zao za kiitikadi. Ni kweli, Regia alikuwa ni daraja. Katika dunia hii ni nadra sana kukutana na wanadamu wengi wenye urafiki na watu wawili walio kwenye uadui huku watu hao walio kwenye uadui wakilifahamu hilo na wakaendelea na urafiki wao na mtu huyo. Nadharia iliyozoeleka ni ile ya ; rafiki wa adui yangu ni adui yangu. Kwa Regia Mtema nadharia hiyo haikufanya kazi. Regia ameweza kudhihirisha kinyume chake, kuwa adui yako anaweza kuwa rafiki wa Regia na wewe na Regia mkabaki kuwa marafiki. Ni watu wachache sana duniani waliojaliwa kuwa na sifa hizo. Na kifo cha Regia kinathibitisha hilo. Kimewakusanya pamoja hata mahasimu. Kimewaleta pamoja hata wagombanao. Hakika, kumuenzi Regia kuliko na maana, ni kuendelea kuliimarisha daraja alilotujengea. Tuache sasa siasa za ubaguzi. Wanadamu tunaweza kutofautiana katika hoja, lakini hatuna sababu za kuchukiana na kutakiana mabaya. Na kuna wanaotaka kuutumia msiba wa Regia kujijenga kisiasa au kuwabomoa wenzao kisiasa. Naamini, Regia asingependa msiba wake utumike kwa kuendeleza ajenda za siasa za uhasama; kupandikiza chuki, kuleta migongano na hila nyingine. Naam, katika maisha kuna visivyoshikika, visivyogusika, lakini vipo. Maana, jua laweza kuliangazia jiwe. Nalo jiwe likapata mwanga. Likapata joto pia. Lakini, jua laweza kuliangazia jicho lako, nalo likapata joto. Hata hivyo, kwa mwanadamu, kuna unachoweza kukifanya ambacho jiwe kamwe haliwezi kukifanya. Ndio, unaweza kulitazama jua kwa jicho lako. Jiwe huangaziwa mwanga wa jua, litapata joto, lakini jiwe haliwezi kulitazama jua. Juzi usiku pale Tabata nilipokaa na kuzungumza na Remija, pacha wa Rejia, kuna mwanga niliouona. Nilimwona Remija akiinamisha kichwa na kufikicha macho yake yaliyokuwa yakilengwa na machozi. Kisha nikamwuliza; wewe na Regia mlikuwa mkigombana utotoni? Na kwanini wewe hupendi siasa na mwenzako alipenda sana siasa? Remija akanitazama kwa macho yake makubwa na yenye mvuto. Kisha akaangua kicheko. Hapo nikamwona Regia. Wamefanana sana. Niliuona mwanga unaongazia jiwe, nalo jiwe likapata joto. Ni vile visivyoshikika, visivyogusika. Lakini, ni vyenye kuamsha hisia. Vyenye kuleta mwanga kunako giza. Vyenye kuleta matumaini katika hali ya kukata tamaa. Regia amewapigania wengi. Amewaletea matumaini walo wengi. Ni wale walio katika hali ya kukata tamaa. Mungu Amlaze Mahali Pema Peponi, Amen.

No comments:

Post a Comment