Na Willbroad Mathias
ILI
Tanzania iwe na maendeleo endelevu lazima kujenga utamaduni wa
kujiendeleza kimasomo hasa katika fani za biashara na ujasiriamali.
Kwa
kufanya hivyo, watakuwa wamejirahisishia mazingira ya kumudu ushindani
unaolikabili soko la ajira ndani na nje ya nchi. Hakuna njia ya mkato
zaidi ya watu kuwekeza katika sekta ya elimu.
Changamoto hiyo ndiyo imewafanya watanzania wengi kuwekeza katika elimu.
Mkuu
wa Chuo Cha Biashara cha Aseki cha mkoani Dodoma, Bw. Omari
Kiputiputi, wakati akizungumzia maendeleo ya elimu na changamoto
mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo pamoja na umuhimu wa ujasiriamali.
Bw.
Kiputiputi anasema ni mhitimu wa Shahada ya Elimu ya Chuo kikuu cha Dar
es Salaam mwaka 1979 na pia ana Shahada ya pili ya usimamizi wa
biashara akiwa amebobea zaidi upande wa masoko MBA aliyopata mwaka 1998.
Anasema
baada ya kuhitimu shahada ya ualimu wa masomo ya sayansi mwaka 1979
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliajiriwa na Chuo cha Biashara Dar
es Salaam CBE na kufanya kazi katika chuo hicho kwa miaka 31 ambapo
alistaafu kwa mujibu wa sheria mwaka 2010.
Anasema, miaka 10 ya
mwisho licha ya kuendelea na kazi ya ufundishaji alipewa dhamana ya kuwa
Makamu Mkuu wa Chuo cha CBE Dodoma.
Bw.Kiputiputi anasema, akiwa
katika nafasi hiyo alikikuta kikiwa na wanafunzi 183, lakini hadi
anaondoka aliacha wanafunzi zaidi ya 4,000.
"Uwezo wa kampasi ile ni wanafunzi 200 tu, lakini tuliweza kufanya yote haya kutokana na stadi za kijasiriamali," anasema.
"Nilipokea
kampasi ile ikiwa inaendesha programu moja tu ya stashada katika fani
tatu tu yaani uhasibu, uendeshaji biashara na uboharia, lakini nimeiacha
kampasi ikiwa inaendesha programe tatu, cheti, stashahada na shahada
katika fani tano za uhasibu, uendeshaji biashara, masoko, uboharia na
TETAMA yaani Teknolojia ya Taarifa na Mawasiliano," anasema.
Anasema
kwa kuwa alifanya kazi kwa bidii, utiifu, ubunifu na uadilifu mkubwa,
alipostaafu mwajiri wake alimpa zawadi nyingi, ikiwemo cheti cha
utumishi uliotukuka hivyo anawahimiza watanzania kujituma zaidi katika
kufanya kazi.
Bw.Kiputiputi anasema, hata hivyo akiwa bado yupo
kazini wazo lake kubwa lilikuwa ni kuanzisha chuo chake binafsi ili
aweze kuwasaidia watanzania kufaidi matunda ya elimu yake.
Anasema
kuwa hata hivyo ndoto zake zilikamilika mwaka jana baada ya kufanikiwa
kuanzisha chuo chake binafsi cha Biashara cha Aseki cha mkoani Dodoma,
ambapo anaahidi kutoa wahitimu bora wanaoweza kujiajiri wenyewe au hata
kuajiriwa kila pembe ya dunia.
Anasema kozi zinazofundishwa
kuwa ni pamoja na cheti cha uhasibu, cheti cha uendeshaji wa biashara na
cheti cha manunuzi na ugavi.
Bw. Kiputiputi anasema kwa upande
wa stashahada wanatoa katika uendeshaji wa biashara, stashahada katika
uhasibu na stashahada ya manunuzi na ugavi.
Anaongeza kuwa
mwanafunzi yeyote aliyemaliza kozi ya cheti NTA 4 inayoendana na fani
hizo kutoka kwenye chuo chochote kilichosajiliwa na NACTE au aliyemaliza
kidato cha sita na kupata angalau 'pass' moja au 'subsidiary' pass
mbili anaweza kujiunga na kozi ya stashahada.
“Tunajitahidi
chuo hiki kiwe cha kipekee hapa nchini kwa kutoa wahitimu bora katika
menejimenti, ujasiriamali na ujuzi kupitia mafunzo, utafiti, utumishi wa
umma na huduma za kijamii katika kanda hii na hata nje ya mipaka
ifikapo mwaka 2020,” anasema.
Anasema chuo kitahakikisha
kinawaandaa wanafunzi katika misingi bora ya uendeshaji bora wa biashara
wenye mafanikio makubwa kwa kuwatumia wanataaluma waliobobea katika
gani husika.
Bw. Kiputiputi anasema chuo kimepata usajili kamili
kutoka NACTE na hiyo inamaanisha kwamba mtu yeyote atakayesoma kwenye
chuo hicho na kufanikiwa kupata cheti kitatambuliwa rasmi nchini na
duniani kote.
Anasema ili kufikia malengo hayo wamedhamiria kutoa
elimu ya kiwango cha juu na kwa gharama ambazo watanzania wengi
wataweza kuzimudu katika kozi za usimamizi wa biashara, uhasibu na
fedha, masoko, ugavi na manunuzi, masomo ya kompyuta na kozi zingine
zinazoendana na masomo hayo.
Anafafanua kuwa, iwapo wahitimu
watapata mafunzo ya kiwango cha hali ya juu itarahisisha kupata
maendeleo endelevu, kwani nchi itakuwa na wataalamu wa kutosha katika
fani mbalimbali kama zinazotolewa na chuo hicho.
Ili Aseki ifikie
malengo hayo, anasema wamepanga kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu
moja, kwa kuzingatia weledi wa taaluma, uadilifu, ubunifu, huduma kwa
wateja na uwajibikaji wa pamoja.
Bw. Kiputiputi anawaomba
watanzania kuchangamkia fursa ya kuanzishwa kwa chuo hicho kwa kuwa
elimu ni ufunguo wa maisha pia hazina pekee kwa urithi wa baadaye.
Anasema
wazazi au walezi ambao wana vijana waliomaliza kidato cha nne na kukosa
sifa ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano wasikate tamaa ili mradi
tu wawe wamefaulu na kupata angalau alama tatu za D, hivyo wanaweza
kujiunga na chuo hicho.
“Akija hapa sisi licha ya kumpa stadi
muhimu za maisha tutampa pia sifa za kuweza kujiunga na chuo kikuu
chochote nchini ndani ya miaka mitatu, tutampa stadi za kuweza kujiajiri
yeye mwenyewe au kuajiriwa baada miaka hiyo mitatu ya kwanza endapo
atashindwa au ataamua kutoendelea na masomo zaidi,” anasema, Bw.
Kiputiputi.
Anasisitiza kuwa, “Tumepania kuwa kituo
kilichotukuka, yaani kituo bora kwa kutoa elimu, mafunzo na stadi katika
nyanja za biashara, uendeshaji na ujasiliamali kupitia mafunzo,
utafiti, huduma kwa umma na shughuli za nje ya chuo katika kanda hadi
kufikia mwaka 2020.”
Bw. Kiputiputi anasema walimu wote wa chuo
hicho wana angalau shahada ya kwanza na stashahada ya juu, hivyo
wahitimu wa chuo hicho wanakuwa na viwango vya elimu inayokubalika
katika fani mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Baraza la Chuo hicho, Dkt. Richard Mushi, anawahimiza watanzania kuwa na
utamaduni wa kuanzisha miradi kwa ubia kwani ndiyo njia pekee ya
kuanzisha miradi mkubwa.
Anasema wengi hawapendi kuanzisha miradi
ya ubia kwa kutoaminiana, lakini aliwatoa hofu kuwa walioanzisha chuo
cha ASEKI kwa ubia wamefanikiwa na chuo kinazidi kusonga mbele siku hadi
siku.
“Waanzilishi wa chuo hiki wanastahili pongezi. Baraza
linaona fahari kuongoza chuo hiki kwani licha ya kuanzishwa na watu
binafsi, chuo kimetimiza masharti yote ya msingi ya kuandikishwa
yaliyowekwa na Baraza la Vyuo vya Elimu ya Ufundi NACTE na ndiyo maana
kimepata usajili kamili,” anasema Dkt. Mushi.
Anasema baraza la
chuo limedhamiria kuona wakufunzi wa chuo hicho wanapata elimu ya ngazi
ya juu zaidi ili waweze kumudu majukumu yao ipasavyo na wawe na viwango
vinavyokubalika popote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la
Mitihani, Bw. Balozi Job Lusinde anasema Baraza lake limepania
kuhakikisha linasimamia viwango vya juu vya taalum ili wahitimu
watakaotoka Aseki wawe watu wa kupigiwa mfano.
No comments:
Post a Comment