Posted: 30 May 2012 01:29 AM PDT
Meya
wa Manispaa ya Iringa, Aman Mamwingi akimkabidhi kombe nahodha wa timu
ya St. Agustine, Jimmy Nicas baada ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya
Safari Higher Learning Pool Competition 2012 yaliyomalizika mkoani
Iringa mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Pool
Tanzania (TAPA) Fred Mushi. Na Michael Machella
|
Posted: 30 May 2012 01:26 AM PDT
Na Godfrey Ismaely, Dar es Salaam ZIKIWA
zimebakia siku chache kabla ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kuingia katika vikao vya Bajeti, mwaka wa fedha 2012 na 2013 baadhi ya
wanaharakati wamedai kusikitishwa na uwajibikaji mdogo wa Serikali hasa
kuchelewa kutoa vitabu vya makadirio hayo. Kwa
mujibu wa Ibara ya 96 ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la mwaka
2007) wabunge wanapaswa kupokea vitabu vya makadirio ya bajeti ya
Serikali angalau siku 21 kabla ya kikao cha Bunge la bajeti kuanza. Pamoja
na kwamba kikao cha bajeti kinatarajia kuanza Juni 12, mwaka huu hadi
Mei 29, 2012 tafiti zinaonesha bado wabunge walikuwa hawajapokea nyaraka
hizo muhimu na haijulikani ni lini watazipokea. Kwa mujibu wa
taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Taasisi ya Sikika na
kusainiwa na Mkurugenzi wake Bw. Irenei Kiria ilieleza kwamba hatua hiyo
inatia wasiwasi katika utendaji. "Tumesikitishwa na hatua ya
Serikali kushindwa kutoa vitabu vya makadirio ya bajeti ya mwaka wa
fedha 2012/2013, siku 21 kabla ya kikao cha Bunge la Bajeti kuanza,
jambo ambalo ni ukiukwaji wa Kanuni za Kudumu za Bunge. "Hii ni
kinyume na kanuni na maazimio mbalimbali yaliyoridhiwa na serikali
likiwemo, Tamko la Dar es Salaam la mwaka 2011 lililotolewa na wananchi
na Azaki karibu 100 kutoka nchi mbalimbali duniani na mashirika 12 ya
Kimataifa," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo. Hata hivyo, tamko
hilo linasisitiza uwazi katika bajeti, uwajibikaji na ushirikishwaji kwa
kuzitaka Serikali Kuu na serikali za mitaa kutengeneza na kujadili
waziwazi katika muda mwafaka angalau nyaraka nane muhimu za bajeti
ambapo kati ya nyaraka hizo mojawapo ni makadirio ya bajeti. Pia
kutolewa kwa wakati kwa vitabu vya makadirio ya bajeti vya mwaka wa
fedha unaofuata kwa wabunge na umma kwa ujumla ni hatua muhimu katika
kuongeza uwazi, ubora wa bajeti na ufanisi wa ushiriki wa wabunge katika
kikao cha kujadili na kuidhinisha bajeti. Taasisi ya Sikika,
ilibaini kuwa ni kawaida kwa wabunge kupokea vitabu vya bajeti kwa
kuchelewa na wakati mwingine huvipata baada ya kikao cha bajeti kuanza. "Hali
hiyo pia inaweza kusababisha wabunge kupitisha bajeti bila kufahamu
undani wa kile wanachokijadili au kupitisha bajeti isiyo na tija wala
kipaumbele kwa taifa," iliongeza taarifa hiyo. Pamoja na
kuchelewa kupatiwa vitabu vya makadirio ya bajeti, Sikika pia imebaini
kuwa wabunge hupatiwa vitabu vya makadirio ya bajeti toleo la I-IV
ambavyo kwa kawaida huwasilisha jumla kuu za vifungu bila maelezo ya
kina. "Na huwa hawapatiwi kabisa Vitabu vya Muundo wa Matumizi
vya Muda wa Kati ya Bajeti (MTEF) kwa kila Wizara, Idara na Mashirika
mbalimbali ambavyo ndivyo hubeba maelezo ya bajeti na shughuli
zitakazotekelezwa," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo. "Sikika
imekuwa ikipitia tovuti ya Wizara ya Fedha, Bunge na kubaini kuwa hadi
leo (jana) tarehe 29, Mei 2012 vitabu vya bajeti kwa mwaka wa fedha
2012/13 havijawekwa kwenye tovuti hizi mbili," iliongeza taarifa hiyo. Aidha,
tafiti zinaonesha kuwa hali hiyo inawanyima wabunge pamoja na wananchi
fursa ya kushiriki kikamilifu katika mjadala wa kuichambua bajeti kabla
ya kuidhinishwa na Bunge. Pia tatizo hilo lilijidhihirisha mwaka jana (2011) ambapo wabunge hawakupata vitabu hivyo kwa wakati mwafaka. "Sikika
inatoa rai kwa Serikali kuhakikisha inatoa vitabu vya bajeti, mwaka wa
fedha 2012/13 toleo la I-IV na vitabu vya Muundo wa Matumizi ya Muda wa
Kati (MTEF) kwa kila Wizara, Idara na mashirika mbalimbali kwa wabunge
kabla ya kuanza kwa kikao cha bajeti. Hii itawapa wabunge muda wa
kufanya uchambuzi wa kina na kushiriki kikamilifu katika mjadala na
hatimaye kuidhinisha bajeti yenye manufaa kwa wananchi," ilifafanua
taarifa hiyo.
|
Posted: 30 May 2012 01:24 AM PDT
Mchezaji
wa mpira wa kikapu anyechezea Ligi ya NBA ya Marekani, Hasheem Thabeet
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kliniki ya
vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya Sprite itakayofanyika katika
viwanja vya Don Bosco Upanga, Dar es Salaam kuanzia keshokutwa. Na
Mpigapicha Wetu
|
Posted: 30 May 2012 01:21 AM PDT
Na Said Hauni, Lindi MKAZI
wa Kata ya Wailes katika Manispaa ya Lindi Bw. Mwanzaga Mbowi
amefikishwa Mahakama ya Mkoa wa Lindi akikabiliwa na shitaka la
kumjeruhi mkewe kwa kumchoma na moto wa pasi. Bw. Mboi ambaye ni
Mhasibu katika Manispaa hiyo alipandishwa kizimbani Mei 28, mwaka huu na
kusomewa shitaka lake na Mwanasheria wa Serikali, Bi. Mwahija Ahamadi. Akisomewa
shitaka lake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Bw. Dustan
Ndunguru, Mwanasheria wa Serikali alidai kuwa mshitakiwa alitendo kosa
hilo Mei 27, mwaka huu, saa 1:30 asubuhi. Bi. Mwahija alidai kuwa
siku hiyo ya tukio huko Wailes iliyopo katika Manispaa ya Lindi
mshitakiwa alimjeruhi mke wake wa ndoa Bi. Olifoncia Chembekwa kwa
kumchoma na moto wa pasi. Aliiambia mahakama hiyo kwamba siku na
wakati huo mshitakiwa na mke wake kwa pamoja walikuwepo nyumbani kwao
na mara kukatokea kidogo mifarakano ambayo ilipelekea mshitakiwa kumpiga
na hatimaye kuchukua pasi ya moto na kumuunguza mlalamikaji mkono wake
wa kulia na sehemu nyingine. Mwendesha mashitaka huyo alidai
kutokana na kitendo hicho, mshitakiwa alimsababishia mlalamikaji maumivu
makali kwenye mwili wake. Bi. Mwahija aliiambia Mahakama hiyo
kwamba kutokana na kitendo hicho mshitakiwa amefanya kosa chini ya
kifungu cha 225 Kanuni ya Adhabu Sura ya 16. Hata hivyo
Mshitakiwa alikana kosa linalomkabili na kupelekwa rumande baada ya
upande wa mashitaka kupinga dhamana kwa mshitakiwa kutokana na kutopata
taarifa ya maendeleo ya mlalamikaji huku kesi hiyo namba
49/2012,itatajwa tena Juni 11, mwaka huu.
|
Posted: 30 May 2012 01:19 AM PDT
Viongozi
wa Kamati inayofuatilia madai ya waliokuwa wafanyakazi wa iliyokuwa
Jumuiya ya Afrika Mashariki kabla ya kuvunjika kwaka 1977, wakitoa
taarifa ya kuungana katika madai yao, wakati wa mkutano na waandishi wa
habari kwenye Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (HLRC) Dar es Salaam
jana. Kushoto ni Bw Ahmed Kabunga na Alfred Kinondo. (Picha na Charles
Lucas)
|
Posted: 30 May 2012 01:16 AM PDT
Na Pamela Mollel, Arusha IMEELEZWA
kuwa bajeti nyingi za nchi za Afrika zimekuwa tegemezi kwa wahisani
jambo ambalo linachangia uwepo wa matumizi mabaya ya rasilimali za nchi
kwa maslahi ya wahisani husika. Pia Serikali imetakiwa kutumia
utawala bora wa fedha kwa wananchi wake na matumizi sahihi ya mali asili
ili ziweze kuwa na tija kwa vizazi vijavyo na kuitumia demokrasia
katika kukuza pato la wananchi. Changamoto
hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Elimu Mafunzo ya Amali kutoka Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Ally Juma Shamuhuna wakati akizungumza na
waandishi wa habari jijini Arusha kwenye mkutano wa Benki ya Maendeleo
ya Afrika (AfDB). "Tumekuja kujifunza suala zima la demokrasia
inavyoweza kukuza uchumi wa nchi yeyote sanjari na utawala bora wa
matumizi ya fedha za serikali na kuwa tunaelekea kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2012-13 ambapo tayari tutakuwa na tumepata uzoefu," alisema Waziri huyo. Alisema
kuwa, Serikali yeyote itakayofuata mambo matatu na kuyajali kwa maslahi
ya wananchi wake hususan utawala bora wa fedha, matumizi sahihi ya demokrasia sanjari na matumizi ya mali asili zitaifanya serikali kutokuwa tegemezi kwa wahisani. “Mashirika
haya ya fedha ulimwenguni hayatoi fedha bure, lazima watangulize
maslahi yao hali inayopelekea nchi zilizofadhiliwa 'kubaka' demokrasia
na wananchi wake kuendelea kuwa maskini,” alisema Bw. Shamuhuna
|
Posted: 30 May 2012 01:14 AM PDT
|
Posted: 30 May 2012 01:12 AM PDT
Na Sangalwise Abia, Dar es Salaam SHIRIKA la Posta Tanzania limefungua biashara ya kuuza na kununua fedha za kigeni (Bureau de change) katika ofisi zake zilizopo Posta Mpya Mtaa wa Azikiwe jijini Dar es Salaam. Hatua
hiyo ni kati ya mikakati ya shirika hilo ambayo inalenga kuhakikisha
linawapatia wateja wake nchini kote huduma mbalimbali zenye tija na
ufanisi, kibiashara zikiwa mahali pamoja ili kuwapunguzia kutumia muda
mwingi wa kuzitafuta mbali. Meneja Masoko wa shirika hilo Bw.
David George aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na gazeti hili juu
ya mipango mikakati ya shirika ambayo inalenga kuboresha huduma zake
nchini kote. Alisema, walifikia hatua hiyo baada ya kupewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania hivi karibuni. "Lengo
la kuanzisha huduma hii ni kwamba tunahitaji kuhakikisha Watanzania
wanapata huduma mahali pamoja badala ya wateja kuhangaika huku na kule
wakitafuta huduma. Kwa hali hiyo sisi posta tukaliona hilo...hivyo
tukaamua kuanzisha huduma hiyo," "Lengo letu ni kwamba mteja
anapoingia katika Ofisi za Posta basi ategemee kupata huduma mbalimbali,
hatua hiyo itawasaidia wateja kutopoteza muda mwingi kwa kutafuta mahitaji,” alisema Bw. George. Alisema, kwa sasa Shirika la Posta limeshaanzisha huduma nyingi zikiwepo huduma za Posta Cash, EMS Courier, EMS Cargo, Post Cargo City urgent mail (pCUM), huduma ya Internent Cafe na sasa huduma ya kuuza na kununua fedha. "Hayo
yote yakiwa ni malengo ya kusogeza huduma za kibiashara karibu zaidi na
jamii ili huduma hizo zipatikane kwa urahisi na mahali pamoja badala ya
kutafuta huduma sehemu mbalimbali," aliongeza. Bw. George alitoa
mwito kwa wateja kuhakikisha wanatembelea katika Ofisi ya Posta ili
wajipatie huduma ya Posta Bureau de Change sambamba na huduma nyinginezo za shirika hilo kwa kuwa zinatolewa kwa ufanisi wa hali ya juuikiwemo gharama nafuu zaidi.
|
Posted: 30 May 2012 01:09 AM PDT
Mkuu
wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishina Augustino Nanyaro kwa niaba ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akimvisha Nishani ya Mwenge wa
Uhuru Daraja la Nne, Mkaguzi Msaidizi wa Magereza, Bi. Mariam Kamangu.
wakati utoaji nishani hizo, Dar es Salaam jana. (Picha na Peter Twite)
|
Posted: 30 May 2012 01:03 AM PDT
Na Mwali Ibrahim WANYANGE
wanaotaka kushiriki katika mashindano madogo ya kumsaka mwakilishi wa
Tanzania katika mashindano ya Dunia (Miss World 2012) wameombwa
kuendelea kuchukua fomu za kuingia katika kinyang’anyiro hicho na
kuzirudisha kabla ya Juni 4 mwaka huu. Akizungumza
Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Lino International Agency ambayo
inaandaa mashindano hayo, Hashim Lundenga alisema wanatarajia kufanya
mchujo wa washiriki Juni 5, mwaka huu kwa ajili ya kubakiza warembo 10
watakaowania nafasi ya kushiriki mashindano ya Dunia. Mashindano
hayo ya Dunia yamepangwa kufanyika Agosti 18, mwaka huu kwenye Ukumbi wa
Dongsheng Fitness Center, mjini Ordos, Inner Mongolia, China. Lundenga
alisema utaratibu huo ulisimamishwa kutokana na zuio la serikali na
wakati huo, jumla ya warembo 12 walikuwa wamekwishachukua fomu za
ushiriki. Alisema muda wa kufanya mashindano hayo, umekaribia na wanatarajia kuitangaza tarehe mpya hivi karibuni. Mkurugenzi
huyo alisema amefurahishwa na kasi ya uchukuaji na kurejesha fomu, hata
hivyo wanahitaji warembo wengi zaidi ili kupata wigo mpana kwa ajili ya
kumsaka mrembo atakayewania taji la Dunia, ambalo kwa sasa lina
mikononi mwa mrembo kutoka Venezuela, Ivian Sarcos. “Tunakaribia
kufanya mashindano madogo hivi karibuni, hivyo ni wajibu wetu
kuwakumbusha warembo wanaotaka kuwania taji hilo kufanya hivyo kabla ya
Juni 4, mwaka huu ili kuweza kuingia katika mchakato wa mchujo,” alisema
Lundenga. Alisema mpaka sasa jumla ya nchi 84, zimekwishapata
wawakilishi wao kwa ajili ya mashindano hayo. Nchi 32 pamoja na Tanzania
bado hazijachagua wawakilishi wao katika mashindano hayo. Lundenga
alisema fomu za kuomba kushiriki zinapatikana katika ofisi za Miss
Tanzania za jijini na mawakala wote wa mashindano hayo katika mikoa ya
Tanzania Bara.
|
Posted: 30 May 2012 01:00 AM PDT
Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Under The Same Sun, Bw. Peter Ash (aliyeinua kofia),
akiwahimiza watoto wenye ulemavu wa ngozi (Albino), kuvaa kofia ili
kujikinga na jua, alipotembelea kituo chao kilichoko Shule ya Msingi
Jumuishi ya Buhangija, mkoani Shinyanga hivi karibuni. (picha na David
John)
|
Posted: 30 May 2012 12:18 AM PDT
Na Mashaka Mhando, Tanga MADIWANI
wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wamesema idara za
polisi na mahakama zina wajibu mkubwa wa kumaliza tatizo la utoro na
mimba shuleni badala ya kuwatupia lawama watendaji wa vijiji na kata. Wakizungumza
katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika jana kwenye ukumbi
wa halmashauri hiyo, madiwani hao walisema idara hizo zimekuwa kikwazo
kikubwa cha tatizo la mimba katika vijiji vingi wilayani hapa hatua
ambayo inachangia kuongezeka siku hadi siku. Diwani wa Kata ya
Ndolwa Bw. Joel Mabula alisema wananchi wakishirikiana na watendaji wa
vijiji wamekuwa wakiwakamata wahalifu wanaosababisha mimba kwa
wanafunzi, lakini wanapofikishwa katika vyombo vya sheria, kesi hizo
zimekuwa zikimalizika bila hatua zozote. “Serikali za vijiji zina
makosa gani jamani? Hadi tuwekeane nao mikataba…Mwenyekiti ningeomba
sasa badala ya kuwabana viongozi wa vijiji Serikali Kuu ingetusaidia
kuvibana hivi vyombo vya dola watu wakikamatwa wakifikishwa polisi na
baadaye mahakamani, washitakiwa wanaachiwa,” alisema Bw. Mabula. Diwani
wa Kata ya Komkonga Bw. Ramadhani Kisatu alitoa mfano wa mtu mmoja
(jina tunalo) kuwa alimpa ujauzito mtoto wa shule na kisha kwenda kuishi
naye katika Mji wa Kitumbi. "Walipomkamata na kumfikisha katika
Kituo cha Polisi Kabuku, mshitakiwa huyo hakuchukuliwa hatua zozote na
matokeo yake yupo huru hadi leo," alidai. Mkurugenzi wa
halmashauri hiyo Bw. Hassain Mwachibuzi akifafanua juu ya muswada
uliowasilishwa na mwanasheria wa halmashauri hiyo Bw. Mohamed Msemo
alisema kuwa mkataba baina ya halmashauri na watendaji utakuwa na
manufaa ya ufuatiliaji kwa kuwa watendaji hao watakuwa wakiitisha
mikutano shuleni itakayokuwa ikifuatilia mienendo ya wanafunzi.
|
Posted: 30 May 2012 12:13 AM PDT
Na Eliasa Ally, Iringa MBUNGE
wa Jimbo la Kilolo mkoani Iringa Prof. Peter Msolla amekabidhi msaada
wa kompyuta tatu na vitabu vya kiada, msaada wenye thamani ya shilingi
milioni tisa uliotolewa na Kampuni ya Simu Airtel Tanzania katika shule
tatu za sekondari jimboni humo. Akikabidhi
msaada huo katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya shule ya
Sekondari Mazombe jana Prof. Msolla alisema kuwa msaada huo ni sehemu ya
utekelezaji wa ahadi zake katika kuendeleza elimu kwa wananchi wake. Prof.
Msolla alisema kuwa mbali ya kuwa shule hiyo ya Sekondari Mazombe haina
umeme ila ametanguliza kompyuta hizo kama njia ya kuanza mkakati wa
kuisaidia shule hiyo kupata umeme wa mionzi ya jua. Alisema kuwa,
shule hiyo ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la kompyuta na kupelekea
walimu kushindwa kuchapa mitihani ama kuandaa masomo yao kwa kutumia
kompyuta na kuishia kuandaa mitihani na vipindi mbalimbali kwa kuandika
kwa mkono jambo ambalo lilikuwa likikwamisha shughuli nyingine. "Napenda
kuipongeza sana...Kampuni ya Simu ya Airtel Tanzania kwa kusaidia
maendeleo ya elimu katika jimbo langu, ndugu zangu wanafunzi na wazazi
moja kati ya vipaumbele vyangu vilikuwa ni elimu na wakati nikiingia
madarakani mwaka 2005 Kilolo ilikuwa na shule za sekondari tatu ila sasa
tumepiga hatua na kuwa na shule zaidi ya 20, napenda kuwahakikishieni
kuwa tutaendelea kupiga hatua katika maendeleo ya elimu," alisema. Pia
aliwataka wanafunzi kutumia vizuri nafasi hiyo waliyoipata kwa
kuendelea kusoma kwa juhudi kubwa na kuwa katika dunia ya sasa elimu
ndio kila kitu na bila elimu ni vigumu kuweza kufanikiwa
|
Posted: 29 May 2012 11:54 PM PDT
Na Suleiman Abeid, Shinyanga IMEELEZWA
kuwa maendeleo na mafanikio ya uchumi wa nchi yoyote duniani hutokana
na wananchi wake kuwa na afya bora zinazowawezesha kufanya kazi za
uzalishali mali pasipo matatizo. Hali hiyo ilibainishwa juzi na
Bw. Billie Edmott ambaye ni Ofisa wa Uchumi na Uzalishaji Mali mkoani
Shinyanga katika uzinduzi wa duka namba 103 la Kampuni ya TIENS
inayojishughulisha na usambazaji wa virutubisho vya mwili wa binadamu. Bw.
Edmott ambaye katika uzinduzi huo alikuwa amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga Bw. Ally Rufunga alisema maendeleo ya nchi yoyote ile
yanaletwa na wananchi wenye afya na kwamba wakiwa na afya zenye mgogoro
haitokuwa rahisi kwao kufanya kazi kwa ufanisi. Alisema,
Watanzania wengi hufanya kazi zao katika mazingira magumu, lakini hata
hivyo baada ya kazi hizo huwa hawapimi afya zao ili kuweza kubaini jinsi
gani viungo vyao vimetumika ili viweze kuboreshwa kwa kupatiwa
virutubisho. “Uchumi wa nchi yetu hutegemea sana kilimo na
asilimia 85 ya Watanzania ni wakulima ambao wapo vijijini, kwenye maeneo
ya uzalishaji wa mazao mbalimbali. Sasa ili maendeleo yapatikane
inatakiwa wakulima hawa wa vijijini wapate huduma ya kupima afya zao
kila wakati ili waweze kuwa na afya bora,” alisema Bw. Edmott.
|
Posted: 29 May 2012 11:44 PM PDT
Na Zahoro Mlanzi BENDI
ya muziki wa dansi ya Mashujaa, imetangaza rasmi kumnasa Meneja wa
African Stars (Twanga Pepeta), Matrin Sospeter kujiunga na bendi hiyo. Akizungumza
Dar es Salaam jana, Rais wa bendi hiyo, Charles Gabriel 'Chalz Baba'
alisema ana furaha kuona kiongozi huyo amejiunga nao na ana imani
itazidi kufanya vizuri katika anga ya muziki wa dansi. Alisema
amefanya kazi na kiongozi huyo kwa miaka sita akiwa Twanga Pepeta,
hivyo anamfahamu vizuri kutokana na kujituma kwake kazini na hata nje ya
kazi. "Nina furaha kubwa kukutana tena na Sospeter katika kazi,
nina imani tutaisukuma vizuri bendi yetu kutoka hapa ilipo na kusogea
mbali zaidi ili kuzidi kuliteka soko la muziki wa dansi," alisema Chaz
Baba. Naye Sospeter alisema ameondoka Twanga kwa ridhaa yake bila
kushawishiwa na mtu na kwamba anaishukuru familia ya Asha Baraka
(Mkurugenzi wa Twanga Pepeta) kwa muda wa miaka 14 aliokaa nao katika
bendi hiyo. Alisema ameondoka Twanga si kwa lengo la kuipa wakati
mgumu bendi hiyo, ila kwa ajili ya maendeleo ya muziki wa dansi ili
kuongeza ushindani zaidi miongoni mwa bendi za muziki huo. Meneja
huyo alisema hana kinyongo na Asha, kwani ndiye aliyemfanya afike hapo
na kwamba anawaomba mashabiki wa Mashujaa kumpa ushirikiano. Wakati
huohuo, Chaz Baba pia alizungumzia ujio wa nyimbo zao mpya ambazo ni
Risasi Kidole, Dunia ya mola, Thamani ya mtu na Usidharau sifuri kwamba
zitakuwa ni moto wa kuotea mbali hivyo mashabiki wao wakae mkao wa kula.
|
Posted: 29 May 2012 11:40 PM PDT
Na Salma Mrisho, Geita IMEELEZWA
kuwa mazingira magumu ya kazi yanayowakabili wauguzi hususan upungufu
wa watumishi wa kada hiyo na malipo kidogo ni mojawapo ya changamoto
zinazowafanya kutowajibika ipasavyo katika kazi zao. Hayo
yalibainishwa hivi karibuni kwenye kongamano la siku mbili na mkutano wa
12 wa Chama cha Wauguzi (TANNA) Mkoa wa Shinyanga ulioenda sambamba na
kuwaaga baadhi ya wauguzi waliohamishiwa mikoa ya Geita na Simiyu. Mgeni
rasmi katika kongamano hilo Bi. Liliani Matinga ambaye ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Bukombe aliwaomba wauguzi hao waendelee na
umoja wao pamoja na baadhi ya wilaya kugeuzwa mikoa mipya. "Ni
vyema sasa kila mmoja akafanye kazi huko anakoenda kwa kuwajibika na
kuwa kitu kimoja, ili kuepusha jamii kuwalalamikia kuwa hamfanyi kazi
ipasavyo ingawa changamoto ya kufanya kazi katika mazingira magumu bado
ipo," alisema Bi. Matinga. Alisema, anatambua kazi ya uuguzi kuwa
ni ngumu, lakini aliwapongeza na kusema baadhi ya uharibu muonekano
mzuri wa fani hiyo kwa kuwatukana wateja wao na kuomba rushwa jambo
ambalo limekuwa likilalamikiwa kila siku na wananchi wanoenda kupata
huduma.
|
Posted: 29 May 2012 11:39 PM PDT
Na Mwandishi Wetu, Mtwara CHAMA cha NCCR-Mageuzi mkoani Mtwara kimevuna wanachama wapya 2,517 katika Jimbo la Mtwara Mjini. Takwimu
hizo zilitolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri ya chama hicho Bw. Danda
Juju alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa. Alisema
kuwa, idadi hiyo imepatikana kuanzia Machi hadi Mei mwaka huu kutokana
na jitihada za uhamasishaji ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi wa
kitaifa na wa jimbo hilo. “Chama kinazidi kushika kasi, tumekuwa
tukivuna wanachama kila kunapokucha kwa sababu wananchi wanajua
NCCR-Mageuzi ndicho chama makini kitakachoweza kuwakomboa. “Nasema
hivyo kwa sababu tangu Machi mwaka huu tulipofanya ziara ya kitaifa
mjini hapa, tumeshaingiza wanachama 2,517 na idadi hii itazidi kushika
kasi kwa sababu wananchi wa Mtwara wameshaamka, wananchi wa Mtwara
wanataka mageuzi kutokana na kuichoka CCM,” alisema Bw. Juju. Kwa
mujibu wa Juju ambaye pia ni Msaidizi Mkuu wa Mwenyekiti wa chama hicho
Bw. James Mbatia alisema wanachama wanaojiunga na chama chao wanatoka
Chama cha Wananchi (CUF), wengine Chama cha Mapinduzi (CCM) na CHADEMA. “Hatutaki
mzaha wakati huu, lengo letu ni kuhakikisha tunaifukuza CCM, tunataka
Mtwara Mjini na Mtwara kwa ujumla wake, iwe ngome ya NCCR-Mageuzi kwani
tunaamini hilo litawezekana kutokana na kasi tuliyonayo. “Kama
tuliweza kuibadilisha Kigoma na kuwa ngome ya NCCR-Mageuzi, kwa nini
Mtwara na Mkoa wa Lindi ishindikane? Hilo haliwezekani, lazima tupambane
hadi dakika ya mwisho na mbinu tulizotumia kuikomboa Kigoma ndizo hizo
hizo tutakazotumia kulikomboa Jimbo la Mtwara Mjini, Mkoa wa Mtwara na
Lindi.
|
Posted: 29 May 2012 11:36 PM PDT
Na Allan Ntana, Tabora KATIBU
Mwenezi wa CHADEMA Bw. Ali Mwakilima amewataka wananchi kutobweteka na
ulaghai wa CCM pindi unapokuja uchaguzi kwa kuwahadaa kwa fulana, kofia
na kanga. Kauli hiyo aliitoa juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Igunda Kata ya Ifucha, Manispaa ya Tabora ambako kulikuwa na mkutano wa CHADEMA. Bw.
Mwakilima alisema inashangaza kuona wananchi wanafikia wanafikia hatua
wanadanganyika na vitu hivyo na baada ya ghiliba hiyo wanatamka CCM
imewalea. ”Mkitaka kujiridhisha na hilo kuwa watendaji na mabalozi nao hawaijui Katiba...ni
pale mtendaji anapohojiwa juu ya haki za msingi za raia na kuwa mkali.
Hiyo ni kiashirio tosha kwamba nao Katiba ya nchi hawaijui,” aliongeza. Aliwataka wananchi kuwa makini na michango isiyo ya lazima na kusema kwamba michango inakuwa mingi, lakini huduma zinakuwa mbovu. Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA Bw. Saimon Lameck
aliwaomba wananchi kwenye mkutano huo waichague CHADEMA kwani ni chama
kitakachoweza kuleta mageuzi na huduma za kweli. ”Ukitaka kujua
hali sasa ni tete na ngumu angalia kijana wa miaka 30 utadhani ana umri
wa miaka 70, hiyo ni kutokana na gharama za maisha kupanda kila kukicha
halafu ndugu zangu mnajitapa kuwa CCM imewalea, badilikeni,” alisema.
|
Posted: 29 May 2012 11:34 PM PDT
Na David John, Aliyekuwa Mwanza IMEELEZWA
kuwa jamii ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini Albino wana uwezo
mkubwa wa kufanya kazi katika sekta mbalimbali iwapo watawezeshwa ili
kuhaakisha maendeleo. Hayo yalielezwa hivi karibuni mkoani Mwanza
na Bi.Vicky Ntetema ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Under
The Same Sun hapa nchini, baada ya kutembelea mikoa ya Kanda ya Ziwa ili
kujionea changamoto zinazowakabili watu hao. Alisema,
kuna haja kupinga mawazo ama fikra potofu ambazo zimejengeka katika
vichwa vya Watanzania kwamba watu wenye ulemvu wa ngozi hawana uwezo wa
kufanya kazi na kupelekea kunyimwa fursa katika maeneo mbalimbali
wanayokwenda kuomba kazi. "Kuna changamoto kubwa, kwa watu wenye
ulemavu wa ngozi kuweza kukubalika katika jamii na hasa pindi
wanapokwenda kuomba kazi katika maeneo tofauti ambapo wanakutana na
vikwazo vingi hasa kuonekana kama hawana uwezo mbali na elimu waliyokuwa
nayo," alisema. Alisema, moja ya changamoto zinazowakabili
walemavu wa ngozi ni kutokukubalika vema na kuonekana kama wao ni watu
watofauti ambao hawawezi kufanya lolote katika jamii kitu ambacho
kinawakosesha amani na kuonekana wanatengwa katika nchi yao. Kwa
upande wa elimu darasani alisema, walimu wanapaswa kuwa karibu na watu
hao ikiwa pamoja na kuonesha upendo wa hali ya juu pia kuepuka kutoa
adhabu ambayo inatokana na kufanya vibaya kwa mwanafunzi mlemavu
darasani. "Najua kuna taasisi nyingi hapa nchini na zinasaidia
katika maeneo mengi, lakini binafsi naomba tujikite zaidi katika
kuwasaidia watu hawa," alisema.
|
Posted: 29 May 2012 11:31 PM PDT
Na Suleiman Mbuguni BAADA
ya wanachama wa Yanga, kushinda vita ya kumwondoa Mwenyekiti wa klabu
hiyo madarakani na kutakiwa kufanya uchaguzi mdogo Mwenyekiti
aliyeondoka kabla ya uongozi huu, Imani Madega amesema ili klabu hiyo
kongwe ifanikiwe ni lazima kufanyike marekebisho ya katiba. Akizungumza
Dar es Salaam jana, Madega alisema katiba hiyo mpya ndiyo itakuwa
suluhisho lililobaki pekee na ili klabu hiyo ifanikiwe ni lazima idadi
ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ipungue kutoka 13 hadi kufikia sita na
Mwenyenyekiti atatakiwa kuwa na kura ya veto. Alisema katika
idadi ya wajumbe hao italazimika watatu wawe wa kuchaguliwa na
wanachama, na mmoja ateuliwe na Mwenyekiti ambaye atakuwa na mamlaka
kutokana na kuwa kura ya veto. "Kwa hiyo baada ya marekebisho
hayo wanachama watatakiwa kuwachagua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti,
wajumbe watatu na mjumbe mmoja atateuliwa na Mwenyekiti ambaye atakuwa
na kura ya veto. "Kwa kufanya hivyo itakuwa imepunguza idadi
kubwa ya wajumbe ambao wengine mara nyingi wanakuwa hawana kazi ya
kufanya, isipokuwa wanasubiri mikutano ya klabu pekee litu ambacho
kinaleta majungu wenyewe kwa wenyewe," alisema Madega. Alisema
baada ya mchakato huo, viongozi hao watatakiwa kulipwa kwa mujibu wa
sheria za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), ambalo
hulipa viongozi wake akiwemo Rais Sepp Blatter. Madega alisema
hatua hiyo ya kuwalipa viongozi mishahara itaongeza uwajibikaji na
kuondoa majungu, kwani haiwezekani mchezaji akawa wa kulipwa alafu
kiongozi wa ridhaa. "Haiwezekani hata kidogo kiongozi akawa wa
kujitolea, alafu anahaha kumtafutia mchezaji mshahara wa sh. milioni 5,
wakati nyumbani kwake hajaacha kitu hivyo ni lazima mfumo huu ubadilike
kama kweli tunataka klabu zetu zipige hatua hatuwezi kuwa na mifumo
miwili tofauti ndani ya klabu moja," alisema Madega. Alisema
hatua hiyo ya kuwalipa mishahara viongozi, itawaletea heshima kwa
wanachama kwani hivi sasa kiongozi akiendesha gari anaonekana amelipata
kupitia klabu, lakini kwa mfumo huu utaondoa dhana hiyo. Kiongozi
huyo alisema hatua nyingine muhimu ni kupunguza idadi ya wanachama wa
kuingia katika mikutano ya klabu kwani sasa Yanga inakadiriwa kuwa na
wanachama zaidi ya 10,000, ambao ni tatizo kama wakifika wote katika
Mkutano Mkuu. Madega alisema hakuna ulazima wa kuwakutanisha
wanachama wote katika mikutano kwa kuwa si wote wanaochangia hoja, bali
wengine hufuata mkumbo na kuanzisha majungu yasiyokuwa na maana. "Si
lazima wanachama wote wakaingia katika mikutano, wanaweza wakachaguliwa
wawakilishi watatu kutoka kila tawi. Kwa mfano akawemo Mwenyekiti,
Katibu na Mjumbe mmoja wa kuchaguliwa katika tawi husika. Mfumo
huo hautakuwa tofauti na vyama vya siasa ambavyo hutumia wajumbe maalumu
kuingia katika mikutano yao kujadili mambo yao, kwani kama vingeamua
kutumia wanachama wake wote ingekuwa ni tatizo kutokana na wingi wao
nchi nzima," alisema. Klabu hiyo inatarajia kufanya uchaguzi
mdogo Julai 15, mwaka huu kutokana na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya
Utendaji kujiuzulu pamoja na Mwenyekiti wake Nchunga.
|
Posted: 29 May 2012 11:21 PM PDT
Na Zahoro Mlanzi KOCHA
Mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen amesema uwezo binafsi
wa wachezaji Didier Drogba na Yahya Toure wa Ivory Coast utawapa wakati
mgumu katika mechi ya Jumamosi itakayopigwa jijini Abidjan. Mbali
na hilo, Kim ameahidi kufa au kupona pindi watakapokutana nao licha ya
kwamba wapinzani wao wana wachezaji wengi wanaocheza ligi kubwa barani
Ulaya. Akizungumza Dar es Salaam jana, Kim alisema anaiheshimu
Ivory Coast kutokana na aina ya wachezaji iliyonayo, lakini kikubwa
katika mechi ya Jumamosi atahakikisha wanacheza soka la uhakika. "Nadhani
hakuna asiyewajua akina Drogba, Toure na Kalou (Salomon) ni wachezaji
wazuri Ulaya kutokana na kuwa fit kiuchezaji, hivyo tunatakiwa kujituma
zaidi ili kupata matokeo mazuri," alisema Kim na kuongeza; "Drogba
na Toure wana 'massive indivudual powers' (nguvu kubwa binafsi) ambayo
huweza kusababisha matokeo ya aina yoyote uwanjani na ndiyo maana
ninawaheshimu kwa hilo." Akizungumzia kuhusu upungufu wa kikosi
chake, Kim alisema kina ukosefu wa nguvu (fitness) ambapo kwa muda
uliobaki wa siku nne kabla ya kukutana na Ivory Coast, hawezi
kurekebisha hilo ila atajitahidi wacheze soka la kiushindani. Alisema
watatumia mbinu za kulinda na kutawala mchezo ambapo mbinu hiyo
itawafanya wawe na nafasi ya kutengeneza nafasi za kufunga. Wakati
huohuo, Kim alimwagia sifa kiungo Mrisho Ngassa kwa kusema sasa
anaonekana kubadilika na kucheza kama alivyokuwa akicheza awali. "Ngassa
amefanya kazi kubwa katika mechi dhidi ya Malawi, kiwango kile
sijakiona akicheze kwa muda mrefu hivyo ni mabadiliko makubwa kwake na
ametambua thamani yake akiwa na timu ya taifa," alisema Kim. Katika
hatua nyingine, Kim aliliomba Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), kuwa na mpango maalumu kwa wachezaji wa Ligi Kuu wawe na kiwango
fulani cha nguvu (fitness) ili wakiwa Taifa Stars wasipate shida. Kikosi
hicho cha Stars kilipanga kuondoka nchini leo kwenda jijini humo kwa
ajili ya mechi hiyo ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2014,
zitakazofanyika nchini Brazil.
|
No comments:
Post a Comment