Posted: 14 Jun 2012 01:03 AM PDT
Na Godfrida Jola
WAKATI
bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/13, ikitarajia kusomwa leo
mjini Dodoma, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa
Ibrahim Lipumba, amesema bajeti ya mwaka 2011/2012 ambayo ilikuwa sh.
trilioni 13.5, haijatekelezwa. Alisema vipaumbele vya bajeti hiyo, vilikuwa na kasoro nyingi pamoja na wafadhili kutotoa fedha walizoahidi. Prof.
Lipumba aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na Majira kwa
njia ya simu juu ya maoni yake kuhusu bajeti iliyopita na inayotajariwa
kusomwa leo. Alisema bajeti iliyopita imeongeza ukali wa maisha ya Watanzania mara mbili zaidi kutokana na ongezeko la matumizi ya ndani. Aliongeza
kuwa, asilimia 39 ya bajeti yote ilikuwa katika sekta ya maendeleo
ambayo hadi kufikia Machi mwaka huu, asilimia 32 pekee ndiyo
iliyotekelezwa. “Bajeti ya kesho (leo), maendeleo yametengewa sh.
trilioni 4 na bilioni 500 wakati mwaka 2011, ilikuwa trilioni 4 na
bilioni 900 hivyo imepungua na haiwezi kufikia wanapotaka, hii inatokana
na Serikali kunyimwa fedha na wafadhili,” alisema. Alisema
bajeti hiyo ilishindwa kumaliza tatizo la ajira kwa vijana kwa kutumia
sekta binafsi, kufufua viwanda vilivyopo na kuboresha upatikanaji wa
nishati ya umeme ili kuongeza uzalishaji viwandani na kuongeza ajira. “Bajeti
ilishindwa kufanikiwa kutokana na utegemezi wa fedha za wafadhili ambao
waligoma kutoa fedha na kuipa Serikali wakati ugumu hivyo kuyumba
katika matumizi yake. “Tatizo la msingi Serikali kutokuwa na dira
kwa sababu inafuata malengo ya milenia na utekelezaji wa Mkakati wa
Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA 2), ambavyo vyote vimepitwa
na wakati, muhimu kubuni njia nyingine ili kupiga hatua ya maendeleo,”
alisema Prof. Lipumba. Alisema Waziri wa Fedha kwa sasa, Dkt.
William Mgimwa hajapata muda wa kutosha kuipitia bajeti iliyopita na
hana utaalamu kuhusu uongozi hivyo hawezi kubaini kasoro zilizopo. “Dkt.
Mgimwa hana utaalamu wa kutosha wa 'fiscal policy', ni mwezi mmoja tu,
toka aingie katika Wizara hii, atawezaje kujua kinachoendelea,” alihoji. Wakati
huo huo, Watanzania wengi wamekuwa na shauku ya kutaka kujua vipaumbele
vilivyotolewa katika bajeti iliyopita vimefanyiwa kazi kwa kiwango
gani. Bajeti iliyopita, ilitaja mambo manne ya msingi ili
kupunguza makali ya maisha na kutenga asilimia 14 ya bajeti yote kwa
ajili ya kulipa deni la Taifa. Mambo hayo ni pamoja na maboresho
ya sheria za kodi, kuongeza nguvu za uwekezaji katika sekta ya umeme,
kupunguza bei ya mafuta ya petroli, matumizi ikiwamo ukubwa wa misafara
ya safari za viongozi na kuongeza fedha katika sekta tano. Pia
bajeti hiyo ilitoa vipaumbele katika sekta ya miundombinu ya barabara,
reli, bandari na mkongo wa mawasiliano wa Taifa ambao ulitengewa sh.
bilioni 2,781.4. Katika mchanganuo huo, nishati na madini
ilitengewa sh. bilioni 539.3 ambayo kwa kiasi kidogo imepunguza tatizo
la mgawo wa umeme. Maji ilitengewa sh. bilioni 621.6 bilioni
ikilinganishwa na sh. bilioni 397.6 mwaka 2010/11, sawa na ongezeko la
asilimia 56, kilimo na umwagiliaji sh. bilioni 926.2 ikilinganishwa na
sh. bilioni 903.8 mwaka 2010/11, sawa na ongezeko la asilimia 2.5. Wakitoa
maoni yao kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema wanatarajia
kupata unafuu wa ukali wa maisha kwa bajeti ya leo kutokana na hali
iliyopo kuzididi kupoteza mwelekeo. Walisema ni muhimu bajeti ya
leo ikaweka vipaumbele ambavyo vitatekelezeka ila kuepuka lawama baada
ya kuisha kwa mwaka wa fedha. “Mwaka 2011 Serikali ilisema
itasaidia kuweka mikakati ya kupunguza ukali wa maisha lakini imekuwa
tofauti maana maisha yamepanda maradufu na kutuacha njia panda,” alisema
Bi. Lenarda Christian, mkazi wa Dar es Salaam. Alisema bajeti ya
leo inatakiwa kuonesha namna ya utekelezaji wa malengo yaliyokusudiwa
na pia iendane na mipango ya Serikali ya ukusanyaji wa mapato na
matumizi sahihi ya fedha. Bw. George Martine, mkazi wa Magomeni
alisema kutokana na bei ya mafuta na bidhaa kupanda mara kwa mara,
imechangia kuongeza ukali wa maisha kwa wananchi. Alisema
Serikali inapaswa kuwaangalia wananchi wake hasa wa kawaida kwa
kupunguza bei za nafaka ili kuwanusuru. “Hivi sasa vyakula vimepanda bei
maradufu hivyo kusababisha maisha kuwa magumu,” alisema. Bei za
vyakula zilianza kupanda nchini mwishoni mwa 2011 ambavyo ndiyo hutumiwa
na watu wengi ukiwemo mchele, maharage, sukari, unga na viungo vya
mboga. Mchele katika masoko ya Dar es Salaam umepanda na kufikia
sh.2,300 hadi 2,500 kwa kilo moja, maharage sh. 2,300, 2,500 hadi 2,600
ambapo awali yalipatikana kwa sh.2,000 hadi Sh. 2,200 kwa kilo, unga
umefikia sh. 1,000 hadi Sh.1,200 kwa kilo ambapo bei ya awali ilikuwa
800 hadi sh. 900 kwa kilo.
|
Posted: 14 Jun 2012 01:02 AM PDT
Na Peter Mwenda
MBUNGE
wa Mwibara, mkoani Mara, Bw. Kangi Lugola, amemtaka aliyekuwa Waziri wa
Fedha, Bw. Mustapha Mkulo, alithibitishie Bunge juu tuhuma
alizozielekeza kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya
Umma (POAC), na kudai imehongwa na Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma
(CHC). Bw. Lugola aliyasema
hayo Bungeni Mjini Dodoma jana baada ya kuomba mwongozo wa spika na
kudai kuwa, katika kikao cha Bunge lililopita, alimtaka Bw. Mkulo
athibitishe kauli aliyowahi kuitoa bungeni akidai kamati hiyo ilihongwa
sh. milioni 60 na CHC ili kupindisha ukweli lakini hakuwepo bungeni. Alisema
katika tuhuma hizo, Bw. Mkulo alimtaja Mwenyekiti wa POAC, Bw. Zitto
Kabwe kuwa ameweka rehani ubunge wake kwa ajili ya rushwa hivyo kuishuka
hadhi kamati hiyo. “Kwa vile Bw. Mkulo yupo hapa, naomba Naibu
Spika atoe mwongozo ili afute kauli yake ili kuweka kumbukumbu sawa au
alete ushahidi bungeni,” alisema. Katika majibu yake, Naibu Spika Bw. Job Ndugai alisema amepokea jambo hilo na atalitolea mwongozo kwa wakati muafaka.
|
Posted: 14 Jun 2012 01:10 AM PDT
Naibu
Kamishina wa Polisi (DCP), Issaya Mungulu, akiwaonesha waandishi wa
habari, picha ya mtuhumiwa wa ugaidi, raia wa Ujerumani, Emrah Erdogan,
au kwa jina lingine Abdulrahaman Othman (24), aliyekamatwa nchini
akituhumiwa kuwa mpiganaji wa kundi la Al-Qaeda aliyehusika katika
matukio mbalimbali ya ugaidi, Dar es Salaam jana. (Picha na Prona Mumwi)
|
Posted: 14 Jun 2012 12:46 AM PDT
Na Salim Nyomolelo
JESHI
la Polisi nchini, linamshikiria raia wa Ujerumani aliyefahamika kwa
jina la Bw. Emrah Erdogan, ambaye aliyekamatwa jijini Dar es Salaam,
Juni 10 mwaka huu. Bw. Erdogan ambaye kwa jina lingine anaitwa 'Abdulrahaman Othman', inadaiwa ni mfuasi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda. Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Kamishna wa jeshi
hilo, Bw. Isaya Mngulu, alisema kijana huyo ana umri wa miaka 24. Alisema
Bw. Erdogan anadaiwa kushiriki mapambano mbalimbali nchini Afghanistan
na hivi karibuni alishirikiana na Kikundi cha Al-Shabab kufanya ugaidi
Aliongeza kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kumuhoji wakishirikiana na mataifa mengine. “Tunashirikiana
na nchi za Uganda, Kenya na Ujerumani kumhoji ili kubaini taarida zake,
baada ya hapo tutatoa taarifa kwa Watanzania,” alisema Bw. Mngulu. Hata
hivyo, Bw. Mngulu alisema jeshi hilo linatambua mchango wa wananchi
ambao ndio uliosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa na kuongeza kuwa, hiyo
ndio dhana halisi ya ulinzi shirikishi. “Jeshi la Polisi
linawahakikishia wananchi kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara
kukabiliana na vitisho vyote vya uhalifu na ugaidi, natoa wito kwa
wananchi waendelee kutupa ushirikiano katika vyombo vyetu ili kuimarisha
amani na utulivu.
|
Posted: 14 Jun 2012 12:41 AM PDT
Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI
wa Muungano wa Vyama vya Wazalishaji na Wachapishaji Maarifa (KOPITAN),
Bw. Abdullah Saiwaad, amesema kanuni na muongozo wa tozo kwa kazi
zinazorudiwa utasaidia kuliongozea Taifa mapato. Bw.
Saiwaad aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika warsha ya siku moja
kuhusu kanuni ya urudufishaji na hakimiliki na kusisitiza kuwa, kanuni
hizo zitawasaidia waandishi na wachapishaji wa kazi za maandishi. “Kanuni
hizi zitasaidia ukusanyaji wa kodi kwa Taifa na wenye hakimiliki
kunufaika kutokana na kazi zao ambazo muda mrefu zimekuwa zinarudufiwa
kinyume na sheria,” alisema. Katika warsha hiyo, njia mbalimbali
za ukusanyaji mapato za kurudufu kazi zenye hakimiliki zilielezwa pamoja
na namna ya kutekeleza mifumo hiyo. Mifumo ya ukusanyaji
mirabaha kwa kiasi kikubwa imeletwa ili kulinda na kuzipa hadhi kazi za
wazalishaji ambao ni waandishi na wachapaji mbalimbali. Aliongeza
kuwa, licha ya kuwepo kwa wimbi kubwa la kurudufu kazi za sanaa, Chama
cha Hatimiliki nchini COSOTA kinashirikiana beka kwa bega na KOPITAN
kuhakikisha mfumo na muongozo wa kanuni hizo ambazo Serikali inatarajia
kuzitoa, utakuwa daraja bora la mafanikio ya kuhakikisha kazi za wasanii
na waandishi zinalindwa ipasavyo. “Tuna nia ya kuwa na mfumo
bora ambao kila mtu atanufaika, kuja kwa mfumo huu ni mafanikio bora
ambayo yatanufaisha watu wote,” alisema Ofisa Mtendaji wa COSOTA, Bw.
Yustus Mkinga. Kwa upande wake, Mwakilishi wa Afrika wa
Shirikisho la Kimataifa la Haki za Urudufishaji (IFRRO), Bw. Greenfield
Chilongo, aliwataka wamiliki wa haki za kazi mbalimbali za kimaandishi
na sanaa nyinginezo, kusimamia haki za umiliki wa kazi zao ili kuzuia
urudufishaji wa kazi hizo unaofanyika bila kufuata sheria na kanuni za
hakimiliki.
|
Posted: 14 Jun 2012 01:10 AM PDT
Mbunge
wa Tabora Mjini Bw. Aden Rage (kushoto) akimsikiliza Naibu Waziri wa
Maji Dkt Binilith Mahenge mara baada ya kipindi cha maswali na majibu
Bungeni Mjini Dodoma jana. (Picha na Vicent Tiganya-Maelezo)
|
Posted: 14 Jun 2012 12:22 AM PDT
Na Willbroad Mathias
TATIZO
la ubovu wa miundombinu katika viwanja vya ndege na ukosefu wa mafunzo
kwa marubani, linadaiwa kuwa chanzo kikuu cha ajali nyingi za ndege
zinazotokea nchini. Wadau wa sekta ya usafiri wa anga nchini,
waliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano wao uliolenga kujadili
na kutafuta njia mbadala ya kuimarisha usalama wa safari za ndege. Wakichangia
mada inayohusu changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo, wadau
hao walisema ajali nyingi za ndege nchini, zinasababishwa na ufinyu wa
miundombinu katika viwanja. Walisema pamoja na kuboreshwa kwa
njia za ndege zinazotumika wakati wa kuruka au kutua, viwanja vingi
nchini vimezungukwa na mazingira yasiyo salama. Akiwasilisha mada
katika mkutano huo, Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege nchini, kutoka
Wizara ya Uchukuzi, Bw. John Nyamwihura, alisema ipo haja ya kuboreshwa
miundombinu hiyo ili kuleta ufanisi. Akizungumzia tatizo la uhaba
wa mafunzo ya marumbani nchini Bw. Nyamwihura alisema sekta hiyo kwa
sasa inakabiliwa na changamoto hizo baada ya Serikali kujitoa tofauti na
ilivyokuwa miaka ya nyuma. Alisema awali Serikali ilikuwa ikibeba jukumu la kugharamia masomo ya marubani tofauti na sasa. “Hali
hii inachangia kuwa na marubani wengi vijana tena wa kigeni tofauti na
Tanzania ambayo marubani wengi wazee, enzi ya Hayati Mwalimu Julius
Nyerere, tulikuwa na utaratibu wa kusomesha marubani katika nchi
mbalimbali,” alisema Bw. Nyamwihura. Kwa upande wake, Mwakilishi
kutoka Chama cha Wasafirishaji wa Anga (TAOA), Bw. Eva Jackson, alisema
ipo haja ya kuwepo uwazi katika kuchunguza vyanzo vya ajali za ndege
nchini. “Hivi sasa ukienda katika taarifa za Mamlaka ya Anga
(TCAA), hakuna taarifa za matukio ya ajali au ya usalama licha ya
kuripotiwa zaidi ya mara 10,” alisema. Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Bw. Fadhili Manongi, alisema ajali za ndege nchini zimepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma. Alisema mwaka huu kumetokea ajali moja tofauti na miaka iliyopita ambayo zilikuwa zikitokea mara kwa mara.
|
Posted: 14 Jun 2012 12:21 AM PDT
Na Anneth Kagenda
KAMANDA
wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga, amekiri
kuwepo vitendo vya uchakachuaji leseni ambavyo ni moja ya sababu
inayochangia ongezeko la ajali nchini. Akizungumza na Majira kwa
njia ya simu Dar es Salaam jana, Kamanda Mpinga alisema kuwa madereva
wengi wanadanganya kuwa wamesea udereva katika vyuo mbalimbali kikiwemo
VETA. “Kuna matukio ya
kufoji vyeti ambayo yamekuwa yakijitokeza katika vyuo mbalimbali
kikiwamo VETA, utakuta mtu anafanya udanganyifu na kudai amesema katika
chuo hiki wakati katika orodha ya waliohitimu hayumo. “Tumekuwa
tukikemea vitendo hivi na kuvitaka vyuo husika kutuletea orodha ya
waliomaliza vyuoni baada ya wanafunzi kumaliza masomo yao ila vitendo
hivi vitakoma,” alisema. Alisema wale wananaondelea na tabia hiyo
wakikamatwa sheria itachukua mkondo wake ambapo baadhi ya watu
waliozungumza na Majira wakiwamo wamiliki wa vyuo vya udereva, walidai
vitendo hivyo bado vinaendelea kwa madereva wengi kupata vyeti bila
kuvisomea vyuoni.
|
Posted: 14 Jun 2012 01:11 AM PDT
Baadhi
ya wanahabari wa vyombo mbalimbali kutoka Mikoa ya Iringa,Mbeya na Dar
es salaam ambao walishiriki katika utafiti na ukibua kero mbalimbali za
wananchi wa kata ya Ijombe wakiwa pamojana Waraghbish wa Mtandao wa
Jinsia TGNP hivi karibuni.
|
Posted: 14 Jun 2012 12:12 AM PDT
Na Kassian Nyandindi, Namtumbo
MADIWANI
wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wametakiwa kuibua
miradi ya kimaendeleo ambayo itakuwa na tija kwa wananchi. Mwenyekiti
wa halmashauri hiyo, Bw. Steven Nana, aliyasema hayo juzi mjini
Namtumbo, mkoani hapa wakati akifafanua mambo mbalimbali ya maendeleo
katika halmashauri hiyo. Alisema hivi sasa halmashauri hiyo
inakabiliwa na changamoto nyingi hivyo ni vyema madiwani wawe na upeo
mpana wa kutafuta njia mbadala za kuharakisha maendeleo ya wananchi. Bw.
Nana aliongeza kuwa, madiwani wana nafasi kubwa katika hilo kama
watashirikiana na wananchi kwenye kata zao badala ya kufanya maamuzi
mbalimbali bila kuwashirikisha Alisema halmashauri nyingi nchini
zinashindwa kujiendesha kwa sababu ya malumbano yasiyo ya lazima
miongoni mwao hasa kwa watendaji hivyo kukwamisha maendeleo.
|
Posted: 14 Jun 2012 01:11 AM PDT
Samaki
waliovuliwa katika nyavu sizizoruhusiwa.Utungaji sheria ndogo za
kudhibiti uvuvi haramu zitasaidia kustawisha uvuvi endelevu na wenye
tija.(Picha na Mtandao wetu).
|
Posted: 14 Jun 2012 12:05 AM PDT
Na Heckton Chuwa, Same
BENKI
ya Ushirika mkoani Kilimanjaro (KCBL), imeanzisha huduma ya akiba kwa
watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ili waweze kupata uelewa wa
huduma za kibenki.
Meneja Masoko wa benki hiyo Bw. Ahsanterabi
Msigomba, aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na viongozi
mbalimbali wa Vyama vya Ushirika vya Msingi na wale wa Chama Kikuu cha
Ushirika Wilaya za Mwanga na Same (VUASU). “Huduma
hii inalenga kuwajengea watoto mazingira ya kuanza kuwa na uelewa wa
kujiwekea akiba tangu utotoni,” alisema Bw. Msigomba na kuongeza kuwa,
benki hiyo pia imeshirikiana na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom
kwa kuanzisha huduma ya M-PESA na wao kuwa wakala wa huduma hiyo. “Huduma
hizi nyongeza ya huduma zingine tunazozitoa ambazo ni pamoja na zile za
Western Money Union Transfer na stakabadhi ya mazao ghalani ambazo
zimekuwa na mafaniko makubwa,” alisema. Bw. Msigomba alisema
mpango wa stakabadhi ya mazao ghalani umeendelea kuwa na mafanikio
makubwa tangu uanzishwe kutokana na huduma wanazotoa kwa wakulima ambao
hawana rasilimali zinazowapa uwezo wa kukopa fedha kwa ajili ya kilimo. Kwa
upande wake, Ofisa Masoko wa benki hiyo Bi. Regina Ndesanjo, alitoa
wito kwa wanachama wa benki hiyo kukamilisha hisa zao ili zifikie
kiwango cha milioni moja ambacho kimewekwa ili waweze kushiriki Mkutano
Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.
|
Posted: 14 Jun 2012 01:11 AM PDT
|
Posted: 13 Jun 2012 11:42 PM PDT
MIGOGORO
ya ardhi imekithiri katika maeneo mbalimbali nchini, kusababisha
umwagaji damu, kuhatarisha amani na utulivu tulionao kutokana na umuhimu
wake. Ni wazi kuwa migogoro hiyo imegawanyika katika makundi
mawili, moja likihusisha wakulima na wafugaji, jingine linahusisha
wananchi na wawekezaji. Kimsingi migogoro inayohusisha wananchi na wawekezaji inachangia wananchi kuichukia Serikali yao na kuharibu mali. Katika
maeneo mengi yaliyohusishwa na migogoro ya ardhi, tayari kumetokea
vurugu zilizosababisha uvunjifu wa amani na kusababisha vifo vinavyoweza
kuzuilika. Vurugu hizo pia zimetokea katika maeneo ambayo
wananchi walioheshimiana muda mrefu, wameamua kuvunja udugu wao kwa
sababu kasi ya Serikali kumaliza migogoro husika haiendani na tatizo
lililopo. Hatua zinazochukuliwa na Serikali ni zile za kujaribu
kutuliza hasira za wahusika jambo linaloweza kutuletea maafa makubwa
baadaye. Sisi tunasema kuwa, migogoro mingi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji inatokana na makundi hayo kutotengewa maeneo. Mtu
akipata eneo mahali popote anajenga, kulima au kufuga kwa sababu
Serikali haijachukua hatua stahiki ya kutenga maeneo na matumizi yake. Ili
kuepuka mapigano ya mara kwa mara na kutunza mazingira, umefika wakati
wa Serikali kutenga maeneo ya kilimo, ufugaji, makazi ya watu na yale ya
wazi. Maofisa ardhi ni miongoni mwa watu wanaochangia migogoro
hiyo kwa kuuza maeneo zaidi ya mara moja hivyo kusababisha jamii
kugombana hata kuchukiana. Sababu kubwa inayochangia maofisa hao
kusababisha migogoro hiyo ni tamaa ya fedha mbali ya kujua wazi kuwa
wanachokifanya ni kinyume na maadili ya kazi zao. Ardhi ni mali ya mwananchi na Serikali hivyo kila upande unapaswa kushirikishwa wakati wa kuuza au kumtafuta mwekezaji. Umefika
wakati wa maofisa hao kubadilika na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria
ili kupunguza migogoro hii ambayo inaweza kuharibu historia ya nchi
yetu.
|
Posted: 14 Jun 2012 01:11 AM PDT
Mfanyabiashara
wa kuku (jina halikufahamika) akiwalinda huku akisoma gazeti,kama
alivyokutwa katika foleni ya kuingia ndani ya Soko la Kisutu Barabara ya
Bibi Titi, Dar es Salaam jana. Kuongezeka kwa wafanyabiashara kwenye
soko hilo kunasababisha msongamano. (Picha na Charles Lucas)
|
Posted: 13 Jun 2012 11:28 PM PDT
Na Suleiman Abeid, Shinyanga
WAKULIMA
wa zao la pamba mkoani Shinyanga, wametakiwa kuuza pamba yenye ubora na
kushirikisha wadau ili kudhibiti uchafu wa zao hilo unaofanywa kwa
makusudi na baadhi ya wakulima wanapokwenda kuiuza sokoni. Wito
huo umetolewa juzi na Meneja Uendeshaji wa Kiwanda cha Kuchambua na
Kusindika zao hilo cha Afrisian Ltd, kilichopo mjini hapa, Bw.
Hrishikesh Katre, katika hafla fupi ya kukabidhi zawadi kwa vituo vya
ununuzi wa pamba vilivyofanya vizuri msimu uliopita. Alisema kama
wakulima na wadau wengine watadhibiti uchafu wa zao hilo unaofanywa kwa
makusudi na baadhi ya wakulima ili kuongeza uzito wa pamba wanapokwenda
kuiuza sokoni thamani yake katika soko la dunia itaongezeka. Aliongeza
kuwa, baadhi ya wakulima wamekuwa na tabia ya kuweka michanga, maji au
magadi katika pamba kabla hawajaenda kuiuza sokoni kitu ambacho mbali ya
kushusha ubora wake, pia husababisha hasara kwa kampuni zinazoinunua na
serikalini.
“Suala la kurejesha ubora wa pamba yetu lipo
mikononi mwetu sisi wenyewe wakulima na wadau wa zao hili, tukidhibiti
uchafuzi huu pamba ambayo itanunuliwa itakuwa safi na ubora wake utakuwa
mzuri hivyo bei katika soko itapanda na wakulima kufaidika,” alisema
Bw. Katre. Alisema kampuni hiyo imeanzisha utaratibu wa
kuvizawadia vituo vyake vya ununuzi ambavyo hununua pamba safi isiyo na
uchafu pamoja na kuwapa motisha watu wanaosimamia vituo hivyo
kuhakikisha wananunua pamba safi. Katika hafla iliyofanyika juzi
kampuni hiyo ilitoa zawadi mbalimbali kwa wahasibu wa vituo hivyo
ikiwemo pikipiki mbili aina ya Toyo, baiskeli mbili aina ya Phoenix,
majembe manne ya kukokotwa na ng’ombe na simu tano za mkononi aina ya
Nokia vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 4.8. Bw. Katre
alivitaja vigezo vinavyomfanya Mhasibu aweze kushinda na kupewa zawadi
kuwa ni pamoja na kufikia lengo la makisio ya ununuzi wa pamba katika
kituo chake. Vigezo vingine ni uaminifu anapokabidhi pamba yake
kiwandani na kuhakikisha hanunui pamba iliyochanganywa na mchanga,
kokoto au kuwekwa maji ya magadi. Aliongeza kuwa, kampuni hiyo
inanunua pamba katika mikoa ya Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mwanza na
tayari imeingia mikataba na vikundi 256 vya wakulima ambavyo vitapatiwa
pembejeo za kilimo katika msimu wa mwaka 2012/2013.
|
No comments:
Post a Comment