Posted: 28 May 2012 01:01 AM PDT
Diwani
wa kata ya msongola ambaye pia ni Mwenyekiti wa Huduma za Uchumi za
Jamii wa Manispaa ya Ilala, Bi.Angelina Malembeka (katikati) akipiga
makofi pamoja na Mratibu wa Benki za Wananchi Vijijini (VICOBA)
Tanzania, Bw.Aldo Mfinde, kulia na Mwenyekiti wa kikundi cha Mlimani
Vicoba cha Ukonga jeshini, Bi.Shia Simba, wakati wa uzinduzi wa kikundi
hicho, Dar es Salaam juzi. (Picha na Charles Lucasa)
|
Na Amina Athumani
LIGI ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa inaanza kutimua vumbi leo kwenye vituo vya Kigoma, Musoma na Mtwara.
Akitoa
ratiba hiyo Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema katika Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma, Flamingo ya Arusha itacheza na Forest
ya Kilimanjaro saa 8 mchana wakati saa 10 jioni ni Ashanti United ya
Ilala na Polisi ya Mara.
Alisema kituo cha Kigoma leo kina mechi
moja kati ya Mwadui ya Shinyanga na JKT Kanembwa ya Kigoma
itakayochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika kuanzia saa 10 kamili jioni.
Alisema
Tenende ya Mbeya na Kurugenzi ya Iringa ndizo zitakazoanza saa 8 mchana
kwenye Kituo cha Mtwara na kufuatia na mechi kati ya Mpanda Stars ya
Rukwa na Ndani ya Mtwara kuanzia saa 10 kamili jioni ambapo mechi hizo
zinachezwa katika Uwanja wa Umoja.
|
Msanii
AT kutoka Zanzibar akitumbuiza jukwaani wakati wa shoo maalum ya
Washindi wa Tuzo za Kili Music zilizofanyika juzi kwenye Uwanja wa
Umoja,Mtwara.
|
Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI
Mtendaji wa Shirika la Ndege nchini ATCL Bw. Paul Chizi amesema idadi
ya abiria wa shirika hilo imezidi kuongezeka baada ya wananchi kuonesha
uzalendo na imani kwa kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi huyo ilieleza hatua hiyo inatokana na mpango walionao wa
kujizatiti ili kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri wa
anga kupitia mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa shirika hilo.
Bw.
Chizi alisema tangu uzinduzi wa safari za Dar es
Salaam-Kilimanjaro-Mwanza wiki moja iliyopita kwa kutumia ndege ya aina
ya Boeing 737-500, kampuni yake imekuwa ikijaza abiria takribani 106
katika kila safari kwa siku tatu mfulilizo hali ambayo inaashiria kuwa
wananchi wameanza kuwa na imani na huduma zinazotolewa na shirika lake.
“Ndege
yetu kwa takribani siku tatu zilizopita imekuwa ikijaza abiria katika
safari zote za Dar es Salaam-Kilimanjaro-Mwanza . Sikujua kuwa tutakuwa
na uwezo wa kurejea na kupata mapokezi ya namna hii kwa haraka kutokana
na kuwa kuna watoa huduma wengine katika njia hii,"alisema Bw.Chizi.
“Baada
ya wananchi kuonesha imani na uzalendo,tutaendelea na kuongeza nguvu
zetu katika kutoa huduma zetu kwa wakati na kwa bei nafuu. Nawaomba
wananchi kuendelea na uzalendo wanaouonesha kwa faida ya kampuni yetu na
nchi nzima kwa ujumla,” aliongeza.
Bw. Chiza alisema kuwa kurudi
kwa huduma za ndege ya ATCL kumeanzisha vita ya viwango vya bei za
usafiri wa anga baada ya ATCL kutoza bei ya chini kwa safari zake
kunadaiwa kusababisha watoa huduma wengine wakiwemo Precision Air nao
kupunguza gharama zao ili kukabiliana na ATCL.
|
Na Mwandishi Wetu
MECHI
ya kirafiki ya kimataifa kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Malawi (The
Flames), imeingiza sh. 40,980,000 kutokana na mashabiki 9,365 walioingia
uwanjani.
Mechi hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya kujiandaa na mechi
zao za kuwania kucheza Kombe la Dunia 2014 ambapo Stars itacheza na
Ivory Coast Juni 2, mwaka huu na Malawi itaumana na Uganda. Timu hizo ziliumana juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu. Kwa
mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana
na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface
Wambura alisema mapato hayo yametokana na hao waliokata tiketi kwa
viingilio vya sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 51,000 na sh. 20,000.
Alisema
asilimia 18 ya mapato hayo ambayo ni sh. 6,251,186 ilikwenda kwenye
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati gharama kabla ya mgawo zilikuwa
tiketi (sh. 4,999,800), waamuzi (sh.,105,000), usafi na ulinzi (sh.
2,350,000), maandalizi ya uwanja (sh. 400,000), Wachina (sh. 2,000,000)
na umeme (sh. 300,000).
Aliongeza kwa upande wa mgawo asilimia 20
ya gharama za mechi ni sh. 4,714,803, asilimia 10 ya uwanja sh.
2,357,401, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh.
1,178,701, asilimia 20 ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
4,714,803 na asilimia 45 ya TFF (sh. 10,608,306).
|
Wasanii
wa kikundi cha Kinoko kutoka Dar es Salaam,wakilishambulia jukwaa
wakati wa promosheni ya Airtel Jiunge na Supa 5 katika Uwanja
waJamuhuri,mkoani Dodoma jana.Uzinduzi rasmi ulifanyika jijini Dar es
Salaam hivi karibuni.
|
Na Pendo Mtibuche, Dodoma
UCHUMI
wa Tanzania umekua kwa asilimia 6.4 mwaka 2011 ambapo katika sekta ya
usafirishaji na mawasiliano, ukuaji huo upo asilimia 11.3.
Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Beno Ndulu aliyasema hayo mjini
Dodoma mwishoni mwa wiki wakati akitoa mada katika mafunzo elekezi
yanayoshirikisha wakuu wa mikoa, wilaya na makatibu tawala wa mikoa.
Alisema,
uchumi katika sekta ya fedha umekua kwa asilimia 10.7, ujenzi 9.0,
biashara 8.1 na uzalishaji 7.8 ambapo hadi sasa, Tanzania inakopesheka
kinyume na taarifa zinazotolewa ambazo si rasmi.
Alisema, sekta ya kilimo bado inaongoza katika kuliingizia Taifa ikifuatiwa na biashara, uzalishaji na ujenzi.
Pia
Gavana huyo aliishauri Hifadhi ya Taifa ya Chakula kuanza kuwa na
mkakati wa kuhifadhi mpunga badala ya mahindi pekee ili kupunguza
mfumuko wa bei kwani mchele ni nafaka inayotumiwa sana na kaya
mbalimbali.
Hata hivyo Prof. Ndulu alisema kushuka kwa thamani ya fedha nchini kumepungua kutoka asilimia 19.7 hadi 19.0 mwaka 2002.
“Kushuka
kwa thamani ya fedha, kumetokana na kushuka kwa bei ya bidhaa hasa
katika eneo la nishati na mafuta hadi sasa asilimia 75 ya Watanzania
wanategemea kilimo hivyo ili Tanzania iweze kupiga hatua katika
maendeleo, sekta hii inatakiwa kutiliwa mkazo,” alisema Prof. Ndulu.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Tume ya Mipango Dkt. Phillip
Mpango aliwataka viongozi kuongoza kwa mifano badala ya nadharia ili
kujua changamoto zinazowapata wale wanaowaongoza.
Aliwataka
viongozi kuwa na uchungu na uduni wa maisha ya wananchi wengi
wanaowaongoza, kuangalia namna ya kuwasaidia ili waweze kuondokana na
matatizo yanayowakabili.
Mafunzo hayo yanahudhuriwa na Wakuu wa Mikoa 24, Makatibu Tawala wa Mikoa 25 na Wakuu wa Wilaya 133
|
Askari
polisi akipita kando ya uzio ulioangushwa na upepo kwenye eneo la
ujenzi wa Barabara ya Mtaa wa Manfierd na kusababisha usumbufu kwa
watumiaji wa barabara hiyo, Dar es salaam jana.Picha na Prona Mumwi.
|
Na Mwandishi Wetu, Mtwara
MWENYEKITI
wa Chama cha NCCR-Mageuzi Bw. James Mbatia amesema bei ya zao la
korosho imepanda kutokana na jitihada za chama chake na kuahidi
kuendelea kuwapigania wakulima.
Bw. Mbatia alitoa kauli hiyo kwa
nyakati tofauti juzi mkoani Mtwara alipokuwa akifungua matawi ya chama
hicho katika Jimbo la Mtwara Mjini. Aliongeza
kuwa, baadhi ya watu wanaweza wasikubaline na hilo, lakini ukweli ni
kwamba wakulima wa zao hilo katika mikoa ya Mtwara na Lindi wanalipwa
sh. 1,200 kwa kilo kutokana na jinsi chama hicho kilivyokuwa kikiwatetea
kwa nguvu wakulima hao.
Alisema, wananchi wa Mtwara wamesahaulika wakati wanalima korosho na ufuta kwa kuwa fedha wanazolipwa ni kidogo. Aliongeza
kuwa Machi, mwaka huu, alikuwa mkoani humo, ambapo alishangaa kusikia
wapata hasara. "Niliposikia hivyo, nikachachamaa, hadi bei ya zao la
korosho ikapanda," alisema. “Pamoja na kuandika barua kwa rais,
tuliendelea kupiga kelele kila siku na hatimaye kelele zetu zimekuwa
mkombozi kwa wana Mtwara na Lindi kwa sababu sasa naambiwa mnalipwa sh.
1,200 kwa kilo moja ya korosho," alisema. Alisisitiza kuwa fedha hizo bado hazitoshi, wanataka walipwe zaidi ya kiasi hicho kwa sababu maisha ni magumu. Katika
ziara yake hiyo, Bw. Mbatia alifungua tawi katika Kijiji cha Namayanga
pamoja na matawi mawili katika Kata ya Likombe likiwamo Tawi la Likombe
na Tumaini Jema. Pia alifungua Ofisi ya Kata ya Majengo,
alifungua Tawi la Mbatia, lililoko Kata ya Ufukoni, alifungua Tawi la
Uledi lililoko Kata ya Chikongola na pia mwanasiasa huyo alifungua Tawi
la Harakati lililoko Chikongora.
|
Na Amina Athumani
ZANZIBAR
imefanikiwa kutetea ubingwa wake wa Judo katika michuano ya Taifa ya
mchezo huo iliyomalizika jana katika Ukumbi wa Land Mark Hotel, Dar es
Salaam.
Zanzibar ambao pia ni mabingwa wa Afrika Mashariki katika
mchezo huo wamefanikiwa kutwaa ushindi wa jumla katika michuano hiyo
iliyoandaliwa na Chama cha Judo Tanzania Bara (JATA).
Michuano
hiyo ambayo imeanza juzi ilishirikisha wachezaji kutoka Zanzibar na
Tanzania Bara ambayo ilikuwa ikiwakilishwa na timu kutoka mikoa na klabu
mbalimbali.
Kwa upande wa washindi mmoja mmoja, Ahmed Magongo
kutoka Korogwe, Tanga amenyakua ubingwa wa jumla na kufanikiwa kupata
kitita cha dola za marekani 1,000 zilizotolewa na mdhamini Gemin.
Pia
kwa upande wa washindi wa uzito wa juu mchezaji Masoud Amour kutoka
Zanzibar anayecheza uzito wa kilo 100 amefanikiwa kukaa kileleni katika
uzito huo.
Mohamed Hamis kutoka Zanzibar aliyepigana katika
uzito wa kilo 81, amefanikiwa kukaa kileleni ambapo kwa upande wa
wanawake mchezaji Matilda Mgasi anayecheza kilo 63 ameshika nafasi ya
kwanza katika uzito wake.
Akizungumzia mashindano hayo,
Mwenyekiti WA JATA, Chief Kiumbe alisema mashindano hayo ni mara ya
kwanza kufanyika kwa wachezaji kupewa fedha taslim.
Alisema
kupitia mdhamini wao Genim wamefanikiwa kuyafanya mashindano kuwa katika
ubora wa hali ya juu na kuomba wadau, Kampuni na taasisi binfsi kuunga
mkono maendeleo ya mchezo huo kwa kutoa sapoti katika mashindano
mbalimbali watakayoyaandaa.
Alisema changamoto kubwa inayoikabili
JATA hadi sasa ni kukosekana kwa ukumbi wa kudumu wa kuchezewa mchezo
huo na kwamba Zanzibar wamekuwa wakifanya vema katika mashindano
mbalimbali ya Afrika kutokana na kuwa na ukumbi mkubwa kwa ajili ya
mchezo huo.
|
Baadhi
ya wakazi wa jiji wakijitolea damu kwa hiari katika kituo cha Huduma na
Ushauri Nasaha cha FEMINA (HIP) wakati wa maadhimisho ya Siku ya UKIMWI
ya Chuo cha Mwalimu Nyerere Kigamboni, Dar es salaam juzi, ambayo
huadhimishwa kila mwaka.
|
Na Speciroza Joseph
NAIBU
wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla ambaye
pia ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha ya Klabu ya Simba, amewataka wana-Simba
kuendeleza umoja na mshikamano ili waendelee kufanya vizuri katika
mashindano mbalimbali.
Mbali na
hilo, pia wafanye haraka kuwa na uwanja wao wenyewe wa kisasa zaidi ya
ule unaomilikiwa na timu ya Azam FC kwani timu hiyo ina historia kubwa
nchini.
Kauli hiyo aliitoa jana jioni wakati wa sherehe za
kusherehekea ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao timu hiyo uliupata
zilizofanyika katika Ukumbi wa Dar Live, Dar es Salaam.
Akizungumza
na wanachama na mashabiki wa Simba waliojitokeza katika sherehe hizo,
Makalla alisema Simba ni timu kubwa na inatakiwa kupiga hatua kubwa
tofauti na ilivyo hivi sasa.
"Simba ina historia kubwa
haikutakiwa kuwa katika hali hiyo, Serikali inajikita kukuza michezo kwa
kuongeza walimu wa ndani wa kuendeleza mchezo huo uwe na mafanikio
zaidi kwa wachezaji wa ndani," alisema Makalla. Kabla ya Makalla
kuzungumza, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Godfrey Nyange 'Kaburu'
aalisema ubingwa wao umetokana na ushirikiano wa wapenzi, wanachama na
kuahidi watatengeneza timu bora zaidi ushindani ligi kuu na Klabu
Bingwa.
Alisema baada ya arobaini ya aliyekuwa mchezaji wao, Patrick Mafisango kupita watafanya sherehe kubwa Watanzania wote. Naye
aliyekuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda alisema mwezi ujao
anatarajia kutoa kitabu maalum kitakachoelezea historia ya Simba tangu
ilivyoanzishwa na mafanikio iliyopata. Alisema kitabu hicho
kimechapishwa nje ya nchi ili kiwe na ubora zaidi ambapo anawaomba
wanachama wao wakae mkao wa kula kusubili kitabu hicho. Sherehe
hizo zilipambwa na burudani mbalimbali ambapo Bendi ya Msondo Ngoma ndio
ilikuwa ya kwanza kupanda jukwaani baada ya michezo ya watoto
kumalizika na burudani zingine ziliendelea.
Vikundi mbalimbali
vya ngoma na wasanii wa bongofleva walitoa burudani ya aina yake lakini
iliyokonga nyoyo za watu wengi ni burudani kutoka kwa Bendi ya Taarab ya
Mashauzi Classis iliyo chini ya msaniii, Isha Mashauzi.
|
Amina Athuman na Zahoro Mlanzi
KAMATI
ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imeitaka
Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Yanga, ianze mchakato wa kujaza nafasi
zilizo wazi kuanzia Juni Mosi, mwaka huu na Julai 15 ifanye uchaguzi wa
viongozi wapya.
Hatua hiyo
ya Kamati ya Uchaguzi imekuja baada ya kujadili kwa kina mustakabali wa
uongozi ndani ya klabu hiyo pamoja na kupokea ushauri kutoka kwa Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi kwa Wachezaji ya shirikisho hilo kutokana na
kujiuzulu kwa Wajumbe nane na kifo cha Mjumbe mmoja wa Kamati ya
Utendaji. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari
Dar es Salaam jana na kusainiwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo,
Deogratias Lyatto alieleza kwamba katika kikao chao kilichofanyika jana
jioni kiliamua Kamati ya Uchaguzi Yanga ifanye mambo matano muhimu.
Taarifa
hiyo iliainisha mambo hayo ni kwamba kamati hiyo ianze mara moja
mchakato wa kujaza nafasi zilizo wazi kwa wajumbe wa kuchaguliwa
waliojiuzulu kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba ya Yanga. "Mchakato
huo uanze Juni Mosi kwa kuzingatia kikamilifu kanuni za uchaguzi wa
uanachama wa TFF na uchaguzi wenyewe ufanyike Julai 15, mwaka huu mahali
patakapopangwa na kamati hiyo na Sektetarieti ya klabu hiyo," ilieleza
sehemu ya taariaf hiyo.
Ilifafanua zaidi kwamba Mkutano Mkuu
utakuwa na agenda moja ambayo ni kujaza nafasi za viongozi hao wa
kuchaguliwa na pia kamati hiyo iandae na kusimamia shughuli za uchaguzi
kwa kuishirikisha sekretarieti chini ya kanuni za wanachama wa TFF kwa
mujibu wa katiba ya TFF ibara ya 49(1) na katiba ya Yanga ibara ya 45(1)
na (2). Wakati huohuo, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imekabidhi
shughuli zote za Klabu ya Yanga kufanywa na Sekretarieti ya Yanga chini
ya Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa.
Kamati hiyo pia imewataka
wajumbe wote wa klabu hiyo ambao hawajajiuzulu kutofanya shughuli zozote
za klabu hadi nafasi za viongozi wa klabu hiyo waliojiuzulu
zitakapozibwa. Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa
Kamati hiyo, Alex Mgongolwa, alisema nafasi za viongozi waliojiuzulu
zitajazwa katika mkutano wa kawaida wa Yanga. Alisema maamuzi
hayo yamefanywa na kamati hiyo baada ya kukaa kikao na Kamati ya
Utendaji Mei 26, mwaka huu na kutoa mwongozo kwa Yanga baada ya Kamati
ya Uchaguzi Yanga kuomba mwongozo huo. Alisema baada ya kupata
taarifa rasmi kutoka Yanga, Kamati imebaini kuwa Kamati ya Utendaji ya
Yanga imekosa akidhi baada ya wajumbe wake wengi kujiuzulu hivyo
kutokuwa na uwezo wa kufanya uamuzi kwa mujibu wa Ibara ya 32(1) ya
Katiba ya klabu hiyo.
|
No comments:
Post a Comment