Posted: 14 Jun 2012 11:35 PM PDT
Kocha
wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen akizungumza wakati wa hafla
ya kuiaga timu hiyo iliyoondoka leo alfajiri kwenda Msumbiji kucheza
mechi ya marudiano ya mchujo wa Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani.
(Picha na Charles Lucas)
|
Posted: 14 Jun 2012 11:38 PM PDT
Na Elizabeth Mayemba
TIMU
ya Taifa (Taifa Stars) imeondoka nchini leo kwenda Msumbiji kwa ajili
ya mechi yao ya marudiano dhidi ya nchi hiyo 'Mambas' kusaka tiketi ya
kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), zitakazofanyika
mwakani nchini Afrika Kusini. Mechi
hiyo inatarajia kuchezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa ulioko
Zampeto nje kidogo ya jiji la Maputo kuanzia saa 9 mchana kwa saa za
huko. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete
ameitakia kila la kheri timu hiyo ili ifanye vizuri, huku akiwapongeza
kwa ushindi katika mechi yao iliyopita dhidi ya Gambia, baada ya kuibuka
na ushindi wa mabao 2-1. Akikabidhi bendera ya taifa kwa Stars,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadik, alisema anaimani timu
hiyo itaiwakilisha nchi vyema katika michuano hiyo na Watanzania wapo
nyuma yao. "Mkumbuke kuwa mnakwenda Msumbiji kuiwakilisha nchi,
hivyo macho na masikio ya Wanzania wote yapo kwenu kuona mtavuna nini
huko, kwa mchezo mzuri mliouonesha mechi iliyopita dhidi ya Gambia bila
shaka na huko mtatuwakilisha vizuri," alisema. Alisema matokeo
mazuri waliyoonesha katika mchezo uliopita isiwe ni nguvu ya soda na
nidhamu, ambayo wanatakiwa kuionesha huko na ushindi kwao uwe wa kwanza. Pia Mkuu wa Mkoa huyo alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete, ameitakia kila la kheri timu hiyo na kuitaka iwakilishe vyema nchi. "Wakati
nakuja kuiaga timu ya taifa, Rais ametoa salamu zake kuwa anawatakia
kila la kheri ili mfanye vizuri na matokeo ambayo yalipita dhidi ya
Gambia yamemfurahisha na anawapongeza sana," alisema. Naye Kocha
Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen alisema ili kuitoa 'Mambas' kwenye
michuano ya Afrika ni lazima timu yake ishinde mechi hiyo. Alisema
maandalizi katika kikosi chake yalikwenda vizuri ingawa ana wachezaji
watatu ambao ni majeruhi, kipa Mwadini Ali na mabeki Nassoro Masoud
'Cholo' na Waziri Salum. Iwapo Taifa Stars itaitoa Msumbiji
katika raundi ya mwisho itapangiwa moja kati ya timu 16 zilizocheza
Fainali za AFCON zilizofanyika Januari mwaka huu katika nchi za Gabon na
Equatorial Guinea. Katika mechi ya kwanza dhidi ya Msumbiji iliyochezwa Dar es Salaam, Februari 29 mwaka huu timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
|
Posted: 14 Jun 2012 11:32 PM PDT
MBUNGE
wa Moshi Mjini, mkaoni Kilimanjaro, Bw. Philemon Ndasambulo (CHADEMA),
ameitaka Serikali kulieleza Bunge ni lini italeta muswada wa sheria ya
Sera ya Taifa ya Ushauri kwenye Viwanda ili iweze kutumika na
kuinufaisha nchi kiuchumi. Bw. Ndesambulo aliuliza swali hilo bungeni mjini Dodoma jana katika kipindi cha maswali na majibu. Akijibu
swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Bw.
Stephen Wassira, alisema Serikali ilianza kuandaa mchakato wa sera hiyo
ili kuwezesha wataalam elekezi kuishauri Serikali mambo ya kiuchumi na
kijamii. Alisema ulijadiliwa na wadau katika hatua mbalimbali na baada ya kukubaliwa, Aprili 2004 ulipelekwa katika Baraza la Mawaziri. Baraza
hilo lilijadili waraka, kukubalina na kumshauri Rais ili aweze kuusaini
na kuwa sera rasmi. Ushauri mwingine waliotoa ili kutekeleza sera hiyo,
lazima kianzishwe Chama cha Washauri elekezi ili kitumike kama
Sekretarieti ya Baraza la Taifa ambapo Ofisi ya Rais, Mipango na
Uwezeshaji, ichukue jukumu la kuandaa mpango mkakati wa sera haraka
iwezekanavyo na kuhakikisha inatekelezwa kwa faida ya Watanzania. Alisema
kutokana na mabadiliko ya muundo wa Serikali ambao ulitangazwa Februari
2008, baadhi ya majukumu yaliyokuwa yakisimamiwa na kutekelezwa na
Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, yalihamishiwa katika Wizara
nyingine. Aliongeza kuwa, hivi sasa utekelezaji wa sera hiyo
unaenda sambamba na Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008, kwa kuhusisha
vyombo vya vitatu ambavyo ni Baraza la Ushauri wa Masuala ya Kazi,
Uchumi na Jamii. Mchakato wa kuandaa rasimu ya sheria ya
uanzishwaji Baraza la Kitaifa la Huduma na Ushauri, unafanyiwa kazi
pamoja na kupata maoni ya wadau mbalimbali chini ya utaratibu wa Wizara
ya Kazi na Ajira. Kwa kuzingatia maoni ya wadau, Serikali itafanya tathmini ya namna kuendelea na utekelezaji wa sera hiyo.
|
Posted: 14 Jun 2012 11:30 PM PDT
|
Posted: 14 Jun 2012 11:28 PM PDT
WAMILIKI
wa shule binafsi zisizo za Serikali, wanawajibika kutangaza ajira za
walimu kwa njia ya matangazo au nyingine wanazoona zinafaa na kuwaajiri
katika shule husika. Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Bw. Philipo Mulugo, aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati
akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Elizabeth Batenga (CCM). Bi.
Batenga alitaka kufahamu kwanini shule na vyuo vya Serikali havina
walimu wa kutosha lakini katika shule na vyuo binafsi kuna walimu wa
kutosha, je, waanawapata wapi? Akijibu swali hilo, Bw. Mulugo,
alisema sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 1995, inafafanua wazi kuwa
utoaji elimu nchini utakuwa kwa ushirikiano wa Serikali na taasisi au
watu binafsi. Alisema shule zisizo za Serikali, zinapata walimu
kwa kutangaza ajira kupitia matangazo na kupata walimu kutoka vyuoni au
nje ya nchi kwa kuhakikisha wanatimiza masharti ya ajira. Aliongeza
kuwa, baada ya kufungua milango ya ajira kwa nchi za Afrika Mashariki,
walimu kutoka nchi jirani watapata ajira katika shule zisizo za Serikali
hivyo upo uwezekano mkubwa wa shule za Serikali kupata walimu wa
kutosha. Akizungumzia suala la utoaji na ukaguaji maendeleo ya
elimu kwenye shule na vyuo vya Serikali na binafsi, Bw. Mulugo alisema
jambo hilo linasimamiwa na Wizara yake kupitia idara na taasisi zake
ikiwemo ya ukaguzi wa shule, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi pamoaja
na Tume ya Vyuo Vikuu.
|
Posted: 14 Jun 2012 11:27 PM PDT
MBUNGE
wa Ole, Zanzibar Bw. Rajabu Mbaruk Mohamed (CUF), amemtaka Waziri
Mkuu, Bw. Mizengo Pinda kutoa tamkoa la kuunda Tume Huru ambayo itafanya
uchunguzi wa kina ili kubaini watu waliosababisha vurugu zilizotokea
hivi karibuni visiwani Zanzibar zikihusishwa na kundi la Uamsho. Bw.
Mohamed aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana waakati akiuliza swali
kwa Bw. Pinda na kudai kuwa yupo tayari kuunda tume huru iweze kufanya
kazi na wahusika ili watakaobainika wachukuliwe hatua. Akijibu
swali hilo, Bw. Pinda alisema Mei 26-27 mwaka huu, vurugu kubwa
zilitokea Zanzibar zikihusishwa na kikundi kimoja kilichosajiliwa ili
kueneza dini ya Kiisilam mwaka 2001 lakini kikaingia katika masuala
mengine yasiyohusiana na dini hiyo. Alisema kikundi hicho
kilianza kupinga Muungano baada ya kuanza mchakato wa Katiba Mpya na
kufanya maandamano ambayo polisi hawakuwa na taarifa nayo. Bw.
Pinda alisema, kikundi hicho kinapaswa kudhibitiwa ili kutoa fursa ya
kufanikisha mchakato wa uandikaji Katiba Mpya kwani Serikali ikiachia
jambo hili bila kuchukua hatua, kukundi hicho kinaweza kuleta madhara
makubwa. Aliongeza kuwa, kutokana na vurugu hizo baadhi ya watu
waliohusika wamekamatwa akiwemo kiongozi wao mmoja ambaye ni Shekhe Juma
Mussa Issa na kudai kuwa taarifa za kiusalama zinasema kikundi hicho
hakitaki Muungano uliopo. Alisema ombi la kuundwa tume hutu ili
kuchunguza chanzo cha vurugu hizo ni zuri na kubainisha kuwa, lazima
lifikishwe katika Serikali ya Zanzibar ndipo hatua zingine zichukuliwe.
|
Posted: 14 Jun 2012 11:35 PM PDT
Mchezaji
Goodluck Mabiriki wa Ilala (kulia) akigombea mpira na mshambuliaji wa
timu ya Lindi, Khalfan Malibiche wakati wa fainali za michuano ya Airtel
Rising Stars inayoendelea kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
|
Posted: 14 Jun 2012 11:21 PM PDT
Na Mwandishi Wetu
TIMU
za soka za Mkoa wa Mbeya za wanaume na wanawake zimejihakikishia
kucheza nusu fainali ya michuano ya kukuza vipaji wenye umri chini ya
miaka 17 ya Airtel Rising Stars inayotarajiwa kuanza leo kwenye Uwanja
wa Karume, Jijini, Dar es salaam. Timu hizo zimefuzu kucheza nusu fainali hiyo baada ya kumaliza katika makundi yao zikiwa zinaongoza. Nayo
Arusha imefanikiwa kupitisha timu zake zote za wanaume na wanawake
baada ya kushika nafasi ya pili katika kundi A nyuma ya Mbeya. Mbali
na timu hizo, zingine zilizofuzu kwa upande wa wanaume ni Temeke
ilioonesha kuwa tishio katika michuano hiyo kwa kufunga idadi kubwa ya
mabao. Ilianza kwa kuisambaratisha Lindi kwa mabao 12-2 kabla ya
kuichakaza tena Ilala kwa mabao 3-0. Wakati wanaume wamefuzu, timu yao
ya wanawake inasubiri matokeo kati ya Ilala na Lindi zilizotarajiwa
kucheza jana. Hata hivyo, kwa upande wa wanaume timu ya mwisho
itakayoungana na timu hizo inategemea matokeo ya mechi za mwisho za
makundi zilizotarajiwa kuchezwa baadaye jana, sambamba na kwa upnade wa
wanawake. Katika mechi zilizochezwa juzi asubuhi timu ya wanawake ya Temeke iliichapa Ilala kwa mabao 2-0. Kwa
upande wa wanaume, Temeke iliendeleza mwendo wake wa kugawa dozi baada
ya kuibugiza Ilala kwa mabao 3-0. Goli la kwanza la washindi lilifungwa
na Khalid Mwenda dakika ya 28, la pili liliwekwa kimiani na Paulo Balama
dakika ya 43 na la mwisho lilpatikana dakika ya 87 kupitia kwa
mshambuliaji wake hatari, Bakari Ally. Katika mechi nyingine
iliyochezwa jioni, timu ya wanawake ya Arusha iliifunga Kinondoni kwa
mabao 2-0, kupitia kwa Anitha Antony dakika za pili na 35. Mechi ya
mwisho ilizikutanisha Kinondoni na Arusha ambapo zilitoka sare ya mabao
2-2. Wafungaji wa Arusha ni Nazir Abdul dakika za 22 na 82, wakati yale
ya Kinondoni yaliwekwa kimiani na Omar Ramadhani na Jarufu Lutonga
katika dakika ya 55
|
Posted: 14 Jun 2012 11:20 PM PDT
Na Zahoro Mlanzi
KAMPUNI
ya Bantu inatarajia kuandaa tamasha la utoaji tuzo za filamu nchini
(Bantu Film Awards), litakalofanyika kwa mara ya kwanza Julai jijini Dar
es Salaam likiwa na lengo la kutambua kazi za wasanii na kuzitangaza
kimataifa. Akizungumzia
tamasha hilo Dar es Salaam jana, Ofisa wa kampuni hiyo, Stewart Kambona
alisema maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri na kwamba wapo
katika mazungumzo na wadau mbalimbali wa sanaa, wakiwemo waadhiri wa
vituo vya sanaa kutoka katika vyuo vikuu mbalimbali nchini. Alisema
tamasha hilo linatarajiwa kufanyika mwezi ujao Dar es Salaam, ambalo
litasaidia kutoa motisha kwa wasanii wanaochipukia na hata wale wakongwe
katika fani hiyo kuongeza bidii katika kuandaa kazi zao. "Unajua
hili tamasha litakuwa ni chachu ya wasanii kuzidi kupata mafanikio
kwani wakiona mwenzao leo amepewa tuzo kutokana na kazi yake fulani,
nina hakika atajipanga ili mwakani naye apewe tuzo, tunatarajia tuzo
hizi kufanyika kila mwaka," alisema Kambona. Alisema kwa kuanzia
kutakuwa na kategoria 27 ambazo alizitaja baadhi yake kuwa ni tuzo ya
muongozaji bora, mtunzi na mpiga picha ambapo watahakikisha wanatoa
fursa kwa wadau kutoa michango yao, ili kusiwepo na maneno ya hapa na
pale baada ya kutoa tuzo hizo. Naye Wasanii Jacob Stephen 'JB' na
Irene Uwoya wakizungumza kwa niaba ya wasanii wenzao kwa nyakati
tofauti, waliishukuru kampuni hiyo kwa kuwa na wazo hilo ambalo
wanaamini litasaidia kuinua tasnia ya filamu hapa nchini ndani na nje ya
nchi. JB alisema wamekuwa wakifanya sanaa kwa muda mrefu, lakini
hakukuwa na kitu cha kuwatia moyo ila hivi sasa kila mmoja ataongeza
ubunifu wake katika kuandaa kazi ili mwisho wa mwaka wapate tuzo. Naye
Uwoya alisema tuzo hizo kwao ni changamoto ya kuzidi kufanya vitu
vizuri zaidi, kwani ana imani tuzo hizo zitawatambulisha kimataifa
kupitia kazi zao na mwisho wa siku mafanikio ya fani hiyo yataongezeka.
|
Posted: 14 Jun 2012 11:36 PM PDT
Wanyange
wanaowania taji la Redd's Miss Kigamboni 2012 wakiwa katika mazoezi
jana, mashindano hayo yanatarajia kufanyika leo katika Ukumbi wa Navy
Beach, Kigamboni. (Picha na Victor Mkumbo)
|
Posted: 14 Jun 2012 11:17 PM PDT
Na Victor mkumbo
MSHINDI
wa kwanza wa taji la urembo la Kitongoji cha Kigamboni mwaka huu
'Redd's Miss Kigamboni City 2012', atazawadiwa sh. 500,000 katika
mashindano yatakayofanyika leo katika ukumbi wa Navy Beach, Dar es
Salaam. Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana, mratibu wa mashindano hayo,
kutoka kampuni ya K&L Media Solutions, Somoe Ng'itu alisema
maandalizi yote yamekamilika na warembo wote wako tayari kwa
kinyang'amyiro hicho. Mratibu huyo alisema mshindi wa pili
atazawadiwa sh. 350,000, wa tatu sh. 300,000, wa nne na watano
wataondoka na cha sh. 200,000 kila mmoja na wengine saba waliobaki
watapatiwa kifuta jasho sh. 150,000 kila mmoja. Alisema mgeni
rasmi katika mashindano hayo atakuwa ni diwani wa kata ya Kigamboni,
Dotto Mawa ambaye ametoa mchango mkubwa katika kufanikisha
kinyang'anyiro hicho. Aliongeza kuwa ili kuboresha shindano hilo
bendi ya muziki wa dansi ya FM Academia maarufu Wazee wa Ngwasuma na
msanii na mchekeshaji mahiri hapa nchini, Mpoki watatumbuiza kwenye
kinyang'anyiro hicho. "Tumeboresha zaidi mashindano ya Redd's
Miss Kigamboni kwa mwaka huu ambapo warembo wote wana sifa na
tunatarajia kuwapata wawakilishi wazuri katika mashindano ya Redd's Miss
Temeke pamoja na Redd's Miss Tanzania 2012," alisema. Aliwataja
warembo watakaochuana kuwa ni Susanne Jeremiah, Agness Goodluck,
Elizabeth Boniface, Dorothea Kessy, Esther Albert, Edda Silyvester,
Sophia Martin, Doreen Kweka, Khadija Kombo, Linnah David, Rosemary Peter
na Winnie Karaya. Aliwashukuru wadhamini ambao wamejitokeza
kusaidia mashindano hayo ambao ni Redd's, Dodoma Wine, Hope Country
Hotel, Screen Masters, Nobro Collections, Times FM na Kitwe Traders. Aliongeza
kuwa warembo watakaoshika nafasi tatu za juu wataungana na wenzao
kutoka vitongoji vya Kurasini na Chang'ombe, ili kuwania taji la Kanda
ya Temeke baadaye mwaka huu.
|
Posted: 14 Jun 2012 11:16 PM PDT
Na Mhaiki Andrew, Songea
SHIRIKA
lisilokuwa la Kiserikali la Good Hope Sports Club la mkoani Ruvuma lina
mikakati ya kutoa mafunzo ya ukocha na waamuzi kwa wanafunzi wa shule
za Sekondari, ikiwa na lengo la kuibua na kuendeleza michezo mkoani
hapa. Akizungumza mjini hapa
juzi Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Joseph Mapunda alisema mafunzo
hayo yatawalenga wanafunzi wa shule hizo kidato cha kwanza hadi cha
tatu ili kuwapatia taaluma ya michezo, badala ya kutegemea makocha
kutoka nje ya mkoa kufundisha. Alisema shirika hilo, limejiwekea
malengo endelevu katika kusaidia kuinua michezo ambapo alidai baada ya
kukamilika kazi hiyo kwa shule za sekondari pia mafunzo hayo yatatolewa
kwa vijana wa shule za msingi kuanzia darasa la tano, ili wajengeke na
uelewa kabla ya kuchaguliwa kuanza kidato cha kwanza. Mapunda
alisema kabla ya kuanza kwa utoaji wa mafunzo ya ukocha kwa wanafunzi
hao, bodi ya shirika hilo imekutana na kuweka mikakati itakayowezesha
kufanikiwa kwa kupendekeza shule za kuanzia, badala ya shule zote kwa
pamoja kwa kutumia kanda za kielimu mkoani Ruvuma. Alisema katika
mapendekezo yao, wamekubaliana wataanzia na shule za sekondari katika
wilaya mbili za Songea na Namtumbo kabla ya kuamia wilaya nyingine za
Nyasa, Mbinga na Tunduru kwa mafunzo hayo ya ukocha na waamuzi ambapo
yamelekezwa kutolewa kwa michezo 11 ikiwemo soka, netiboli, ngumi,
riadha na mpira wa wavu. Mkurugenzi huyo alisema programu hiyo ya
mafunzo itaanza kutolewa baada ya na kuvutiwa na kituo cha michezo cha
Twalipo cha Jijini Dar es Salaam, kilivyofanikiwa kwa kiasi kikubwa
kutoa mafunzo ya ukocha na waamuzi kwa vijana wenye umri wa chini ya
miaka 20.
|
Posted: 14 Jun 2012 11:13 PM PDT
Na Victor Mkumbo
MSANII
wa muziki wa kizazi kipya nchini Isihaka Nassoro 'Dogo Aslay',
anatarajia kuzindua albamu yake ya kwanza Juni 24 mwaka huu katika
Ukumbi wa Dar Live, Mbagala. Akizungumza
Dar es Salaam jana, Meneja wa kundi la TMK Wanaume Family, Said Fella
alisema Dogo Aslay anatarajia kuzindua albamu hiyo, kitabu pamoja na
filamu ambapo zote amezipa jina la Naenda Kusema. Alisema albamu
hiyo ina jumla ya nyimbo 10 ambayo ameirekodia katika studio ya Poteza
Records chini ya mtayarishaji Suresh pamoja na Alow Nem. Fella
alisema katika uzinduzi huo kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii
mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya, ambao watamsindikiza Aslay. Alisema
wasanii watakaoimba jukwaa moja na Aslay ni pamoja na Mh. Temba, Bi.
Cheka, TMK Wanaume Family, Ize Man, Ommy Dimpoz na Mwana FA. "Tumeandaa
onesho maalumu kwa ajili ya Aslay kutambulisha albamu, kitabu pamoja na
filamu ambapo pia kutakuwa na burudani ya aina yake kutoka kwa wasanii
mbalimbali," alisema. Alizitaja baadhi ya nyimbo zilizopo katika
albamu hiyo kuwa ni Nakusemea, Niwe Nawe aliyoimba na Mh. Temba, Kikombe
aliyomshirikisha Ferouz, Umbea ambaye amemshirikisha Chege, Utajuta,
Mapendo, Nastrago aliyoimba na Mkubwa na Wanawe pamoja na Hawakai.
|
No comments:
Post a Comment