Na Elizabeth Mayemba
ALIYEKUWA
Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Davis Mosha amesema kwamba hayupo
tayari kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya klabu hiyo katika
uchaguzi mdogo wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Julai 15, mwaka huu.
Mosha
alitoa kauli hiyo wakati Wazee wa muafaka wa klabu hiyo wakiongozwa
Katibu wake Ibrahim Akilimali walipoenda kumpa pole baada ya Alhamisi
kufiwa na baba mkwe wake mzee Malick Said Kiongoli, ambapo pia walitumia
fursa hiyo kumshauri mpiganaji huyo ili agombee nafasi moja wapo katika
uchaguzi huo.
"Kwanza kabisa nawashukuru sana wazee wangu kwa
kuja kunifariji katika kipindi hiki kigumu cha kufiwa na baba mkwe wangu
Mzee Malick, na ombi lenu la kutaka nirudi kuiongoza Yanga nimelisikia
lakini sitakuwa tayari kufanya hivyo,ila naomba niwaahidi kitu kimoja
kuwa mimi ni mwanachama wa Yanga na mwenye mapenzi ya dhati na timu
hiyo, nitakuwa tayari kutoa msaada wowote kwa timu hata kama nitakuwa
nje ya uongozi," alisema Mosha
Alisema anashukuru kwamba wazee
hao wametumia busara na hekima kubwa kwani tangu ajiuzulu wadhifa huo
hakuwahi kukutananao, lakini juzi ndiyo kwanza amewaona hivyo hapuuziii
ombi lao lakini kwa sasa hatakuwa tayari kuongoza Yanga lakini atakuwa
bega kwa bega na timu hiyo.
Mosha alisema kuwa sasa timu hiyo
inakabiliwa na michuano ya kombe la Kagame anachoahidi kwa wazee hao ni
kushirikiana nao na kuhakikisha timu yao itatetea ubingwa wake ikiwa na
kusajili wachezaji bora ambao watawaletea ubingwa.
Pia amewataka
wanachama wa klabu hiyo kuwa makini katika kuchagua viongozi, wawachague
wale ambao wanamapenzi mema na klabu na pia wenye uwezo kifedha na si
wale ambao watataka kuja Yanga ili wanufaike na mapato ya milangoni.
"Chagueni
viongozi ambao angalau watakuwa wanauwezo kifedha na hata kiuongozi,
sio wale viongozi ambao wanategemea kujiendesha kupitia fedha za Yanga,"
alisema
Naye Mzee Ibrahim Akilimali alisema kuwa wanatambua kuwa
Mosha ni mpiganaji kwani baada ya kujiuzulu alihakikisha anaisaidia
timu hiyo na hatimaye ilitwaa ubingwa wa bara msimu uliopita, na ndio
maana waaona watumie nafasi hiyo kumshawishi arudi tena Yanga.
"Hakuna
ambaye hajui kuwa Mosha ni mpiganaji kila mwanayanga anajua hilo na
ndio maana tukatumia fursa hii ili kumshawishi agombee, lakini ilimradi
ametuahidi kuendelea kutusaidia hilo tunampongeza sana na sisi
tunamuombea kwa Mungu afanikiwe hilo," alisema Akilimali.
No comments:
Post a Comment