DODOMA.
MWENYEKITI Mteule wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amezungumzia uwezekano wa kutumia kura ya siri katika kuamua ibara nyeti katika Rasimu ya Katiba.
MWENYEKITI Mteule wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amezungumzia uwezekano wa kutumia kura ya siri katika kuamua ibara nyeti katika Rasimu ya Katiba.
Sitta aliyechaguliwa juzi kushika wadhifa huo,
alisema atashirikiana na kamati ya uongozi itakayoundwa ya wenyeviti wa
Kamati 15 za Bunge hilo na kamati ya ushauriano kupata jawabu la suala
hilo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu nyumbani
kwake mjini Dodoma juzi, Sitta alisema: “Unajua kuna baadhi ya vifungu
na ibara za Rasimu ya Katiba ni vizuri vipigiwe kura ya wazi na vingine
ambavyo ni nyeti zaidi vipigiwe kura ya siri.”
Alisema si vizuri vifungu vyote vipigiwe kura sawa, yaani si lazima zote ziwe za siri au ziwe za wazi.
Alitoa mfano wa ibara inayosema kutakuwa na
Mahakama Kuu ya Tanzania na kusema: “Hatuwezi kushindana katika suala la
kuwapo kwa Mahakama na ni wazi kuwa jambo hilo mnaweza kupiga kura ya
wazi. Nasema hivyo kwa sababu Katiba yoyote lazima ionyeshe mihimili
yote ambayo ni Bunge, Serikali na Mahakama.”
Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki alishinda kiti hicho katika uchaguzi uliofanyika juzi
kwa kura 487 kati ya 563 (sawa na asilimia 85).
Mbunge huyo wa Urambo Mashariki ambaye kaulimbiu
yake ni ‘kasi na viwango’, alisema vifungu na ibara za Rasimu ya Katiba
vinavyoweka misingi ya Katiba, ni vizuri vikapigiwa kura ya siri.
“Unajua tuna viongozi wa dini na halitakuwa jambo
la busara kama tukizijua hisia zao. Kama wewe uko karibu na imamu au
askofu halafu anapiga kura ya wazi ya kutaka Serikali tatu wakati wewe
muumini unataka Serikali mbili ni wazi kuwa jambo hilo linaweza kuleta
hisia tofauti na kuwanyima watu haki na uhuru wa kuamua,” alisema Sitta.
Alitoa mfano wa Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba
inayozungumzia Serikali na muundo wa madaraka katika Jamhuri ya Muungano
na kufafanua kuwa katika sura hiyo atapendekeza ipigiwe kura ya siri.
Kuhusu suala hilo la muundo wa Serikali alisema:
“Kikubwa ni wajumbe kujenga hoja, hatuwezi kwenda na misimamo
isiyobadilika kwa sababu tunataka maridhiano. Nitatenda haki na nitatoa
muda mrefu zaidi kwa wajumbe kujadili sura ya kwanza na ya sita ambazo
zina uzito mkubwa kuliko sura nyingine ambazo ni za maelezo tu. Mfano
suala la haki za binadamu ambazo wote tunakubaliana nazo.”
Alisema wakati wa kujadili muundo wa Serikali
ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukifika, ataishauri kamati ya
uongozi, kutenga muda wa ziada katika suala hilo na mengine yenye utata.
No comments:
Post a Comment