BY- MWANDISHI WETU, MWANANCHI
Alhamisi ni siku ya nne ya wiki katika kalenda inayotumika sehemu nyingi duniani, ipo baada ya Jumatano na kabla ya Ijumaa.
Wako wengi wanaoamini katika siku, baadhi wakiita Alhamisi kuwa ni
“Siku ya Mungu wa Radi”, na wengine kuitumia kuanzia mapumziko ya wiki,
wakitofautiana na wale wanaoanzia Ijumaa.
Lakini kwa Dk John
Magufuli, siku hii inaonekana kuwa na umuhimu wa pekee kuanzia siku
aliyozaliwa hadi sasa, Mwananchi inaweza kukujulisha baada ya kupitia
matukio kadhaa ya maisha yake.
Leo ni Alhamisi ya 20 tangu Rais Magufuli aingie Ikulu Novemba 5, 2015.
Katika kipindi hicho, mara nyingi Rais Magufuli ameitumia siku hii
kufanya au kutangaza uteuzi kama ilivyokuwa wakati akitangaza Baraza la
Mawaziri la kwanza kwa Serikali yake, na pia kutoa matamko.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa asilimia kubwa ya
uteuzi wa Rais Magufuli umefanywa au kutangazwa siku za Alhamisi.
Huenda matukio hayo hutokea kwa bahati siku ya Alhamisi au ameamua kufanya hivyo kwa umuhimu fulani.
Historia ya Magufuli hapa duniani ilianza kuandikwa Alhamisi ya Oktoba
29, 1959 siku ambayo alizaliwa Chato wakati huo ikiwa mkoani Kagera
(sasa mkoani Geita).
Hata alipoibuka kidedea kwenye
kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015, Tume ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza
rasmi kuwa mshindi siku ya Alhamisi.
Kama vile haitoshi, NEC ilimkabidhi cheti chake cha ushindi Alhamisi ya Oktoba 29 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.
Alhamisi iliendelea kujidhihirisha kwenye maisha ya Magufuli kuwa ni
siku ya aina yake Novemba 5, 2015 wakati alipoapishwa rasmi kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuanza kazi mara moja.
Kumbukumbu zinaonyesha Rais Magufuli alifanya uteuzi wake wa kwanza
Alhamisi ya Novemba 5 mwaka jana alipomteua George Masaju kuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ikiwa ni saa chache baada ya kuapishwa.
Alhamisi ya Novemba 19 mwaka jana alifanya uteuzi wa Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa ikiwa ni takribani wiki mbili baada ya kuingia Ikulu.
Haikuishia hapo, Alhamisi ya Desemba 10 alitangaza Baraza la Mawaziri na
kuteua mawaziri na manaibu wao. Katika uteuzi huo Magufuli aliacha wazi
wizara nne kwa kile alichoeleza kuwa alikuwa anaendelea kutafuta watu
wanaofaa.
Akiendelea na kutengeneza Serikali yake na kujenga
taasisi, Alhamisi ya Januari 21, 2015 alipomteua Rais wa Serikali ya
Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM).
Yako matukio mengine mengi ambayo Rais Magufuli
ameyafanya siku nyingine za wiki, lakini makubwa yanaonekana kuangukia
Alhamisi.
“Hii ni siku tukufu kwa kuwa ni siku ambayo Mtume
alipewa utukufu,” alisema Sheikh Othman Zuberi alipoulizwa kuhusu
umuhimu wa siku ya Alhamisi.
Alifafanua kuwa Waislamu huitumia
Alhamisi kufunga na kujinyenyekeza kwa Mungu kwani matendo aliyotenda
Mola kwa wiki nzima hunyanyuliwa na kupelekwa mbinguni.
“Kwa
imani yetu Alhamisi ni siku tukufu ndiyo maana Waislamu wengi hufunga na
kujinyenyekeza kwa Mungu, kwa kuwa matendo yao hupelekwa mbinguni siku
hiyo,”alisema Sheikh Zuberi.
Lakini mtaalamu wa nyota, Maalim AbalHasan alikuwa na maelezo tofauti.
“Ni siku yenye mafanikio na hutumiwa na watu wanaotaka kufanikiwa
katika mambo wanayofanya,” alisema alipoulizwa umuhimu wa Alhamisi
katika maisha.
Alisema siku hii inahusu masuala ya utawala na
mara nyingi wanaofanya jambo Alhamisi huwa na nia njema hivyo hupata
baraka kutoka kwa Mungu.
“Alhamisi ni siku muhimu kwa wasomi,
watawala, waadilifu na wale wenye kupenda kuweka mambo sawa. Ukimuona
mtu anapenda kufanya jambo lake Alhamisi, basi ujue huyo ni mkweli na
lazima atapata baraka,” alisema.
Siku nyingine ambazo zimeonekana
kujirudia mara kwa mara kwenye shughuli anazofanya au zinazomtokea Rais
Magufuli ni Jumatatu, Jumatatu na Jumapili.
Jumatano, Desemba
16, 2015 alimteua Valentino Mlowola kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Takukuru kuziba nafasi ya Edward Hosea aliyetolewa kutokana na
kutoridhishwa na utendaji wake, hasa katika suala la utoroshaji
makontena Bandari ya Dar es Salaam.
Jumatano ya Desemba 23, 2015
aliwateua mawaziri wanne kujaza nafasi zilizoachwa wazi wakati
akitangaza Baraza la Mawaziri. Pia alimtangaza naibu waziri mmoja na
kumhamisha wizara mmoja. Katika siku hii pia alimteua Alphayo Kidato
kuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kuziba nafasi ya Dk
Philip Mpango aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Fedha.
Jumatano ya Desemba 30, Rais Magufuli alifanya uteuzi mwingine ambao ulihusisha makatibu na manaibu wao.
Siku hiyo, alimteua pia Balozi Ombeni Sefue kuwa Katibu Mkuu Kiongozi
kuendelea kushikilia nafasi aliyokuwa nayo wakati wa utawala wa awamu
wanne.
Jumatatu ya Novemba 16, alimteua Dk Tulia Ackson kuwa mbunge. Kabla ya uteuzi alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Jumatatu ya Februari 15, 2016 alimteua Dk Modestus Kipilimba kuwa Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuziba
nafasi ya Dickson Maimu aliyesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.
Jumatatu ya Februari 15, 2016 alifanya uteuzi wa mabalozi watatu bila ya
kuwapangia vituo. Mabalozi hao ni pamoja na Dk Asha-Rose Migiro,
Mathias Chikawe na Dk Ramadhan Dau aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF.
Siku ya Jumapili imeonekana kujirudia mara mbili kwenye uteuzi wake.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Jumapili ya Machi 6, 2016 alimteua Balozi
John Kijazi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kuchukua nafasi ya Balozi Ombeni
Sefue.
Jumapili ya Machi 13, 2016 alifanya uteuzi wa wakuu wa mikoa.
Ijumaa imejitokeza mara moja ambayo ni Januari 29, 2015 alipofanya
uteuzi wa makatibu tawala wawili wa mikoa ya Mwanza na Katavi. Kamishna
wa Polisi, Clodwing Mtweve(Mwanza) na Kamishna wa polisi Paul Chagonja
(Katavi).
Source - Mwananchi 17/3/2016
No comments:
Post a Comment