Picha ya pamoja ya wajumbe wa mkutano wa wadau wa PSPF pamoja na Mgeni Rasmi (katikati). Mkutano huo uliofanyika Jijini Mbeya hivi karibuni.
PSPF imesifiwa kwa kubuni bidhaa mpya kwa kuwanufaisha wanachama wake. Sifa hizo zilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Bi. Mariam Mtunguja, alipokuwa akifungua mkutano wa PSPF pamoja na wadau wake Mkoani Mbeya hivi karibuni.
Katibu Tawala Mkoa Mbeya alisema kuwa mkopo wa elimu, mkopo kwa waajiriwa wapya na fao la uzazi litakaloanza kutolewa Julai mwaka huu vitatoa haueni kwa wanachama wa PSPF. “Kila mtu anaelewa jinsi vijana wetu wanavyopata tabu wanapoajiriwa, kwani unapopata ajira au wakati wa uzazi mahitaji yanakuwa mengi sana, hivyo kwa PSPF kuja na bidhaa hizi mpya mtakuwa mnasaidia vijana wetu kwa kiwango kikubwa” alisema Bi. Mtunguja.Kwa upande wa mkopo wa elimu, Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, alipongeza PSPF kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha kila mtanzania anapata elimu. “Sisi wa upande wetu Serikalini tunajitahidi, lakini sasa tunafarijika kwa kuona PSPF nanyi mnasaidia eneo hili muhimu, asanteni na hongereni.”Katibu Tawala Mkoa Mbeya aliishukuru PSPF kwa kutoa misaada katika maeneo elimu, afya, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha kila mtanzania anapata maisha bora. Kwa upande wa washiriki, Katibu Tawala Mkoa Mbeya, aliwaasa kutumia vizuri fursa hii iliyotolewa na PSPF kwa kutatua changamoto wanazokabiliana nazo kuhusiana na mafao ya wanachama wa PSPF na kupata ufafanuzi sahihi kutoka taarifa potofu dhidi ya Mfuko. Kwa upande wa PSPF, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa PSPF Adam Mayingu , Bw. Msafiri Mugaka, alisema Mfuko kwa upande wake umekuwa ukitekeleza vyema miongozo na maelekezo kutoka Serikalini na mamlaka zote. Akiainisha changamoto zilizopo, Bw. Mugaka, alisema changamoto kubwa ni kwa watumishi ambao wanakaribia kustaafu kushindwa kuwasilisha nyaraka muhimu zinazohitajika hivyo kuleta usumbufu kuandaa mafao kwa wakati. Aliomba wadau wa mkutano kuwaelimisha wanachama wa PSPF juu ya umuhimu wa kuwa na nyaraka sahihi na kuziwasilisha kwa wakati ili kuepusha usumbufu.Waliohudhuria ni maafisa utumishi, makatibu afya, maafisa kilimo, waratibu wa elimu kata pamoja na maafisa elimu msingi na sekondari.
No comments:
Post a Comment