Wajumbe
 wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakitia saini Rasimu ya Pili ya Katiba 
juzi. Rasimu hiyo itakabidhiwa leo kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais Ali 
Mohamed Shein, Karimjee, Dar es Salaam. Picha ya mtandao. 
………………………………………………………………………………………………
Dar 
es Salaam. Swali la nini kilichomo katika Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya 
litajibiwa leo wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapokabidhi rasimu
 hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali 
Mohammed Shein.
Rasimu inayosubiriwa kwa hamu na
 wananchi wa kada zote itatolewa ikiwa imepita miezi saba tangu tume 
hiyo ilipotoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba ambayo ilijadiliwa na 
kuboreshwa katika Mabaraza ya Katiba yaliyoketi kuanzia Julai 12 mpaka 
Septemba 2, mwaka huu.
Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 3, 2012 kwa kukusanya maoni ya wananchi, iliandaa rasimu ya kwanza iliyotangazwa Juni 4, mwaka huu.
Hafla ya kukabidhi rasimu hiyo 
itafanyika leo saa 6.00 mchana katika Viwanja vya Karimjee, jijini Dar 
es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya 
siasa na asasi mbalimbali.
Baada ya kukabidhi rasimu hiyo ya Katiba, Tume ya Mabadiliko ya Katiba itavunjwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume 
hiyo, Jaji Warioba ndiye atakayesoma rasimu hiyo kwenye Bunge Maalumu la
 Katiba linalotazamiwa kuanza vikao vyake Februari, mwakani.
Alipoulizwa nini kilichoongezwa 
au kupunguzwa katika rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema: “Siwezi kueleza 
kama kuna kilichoondolewa au kurekebishwa… kesho (leo), Watanzania 
watapata fursa ya kujua mapendekezo ya tume, wasubiri.”
Baadhi ya mambo yanayosubiriwa 
kwa hamu kujua kama yamefanyiwa marekebisho au la kwenye Rasimu Mpya ni 
pamoja na mfumo na muundo wa Muungano, umri wa kugombea urais, wabunge 
kutokana na mikoa, umri wa kugombea urais na mengine.
Serikali Tatu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba 
kupitia Rasimu ya Kwanza ilipendekeza kuundwa kwa Serikali Tatu na 
alipokuwa akizungumzia hilo wakati akitangaza Rasimu ya Kwanza, Jaji 
Warioba alisema uamuzi huo ulifikiwa kwa kuwa yalikuwa ni maoni ya 
wananchi walio wengi.
Hata hivyo, pendekezo hilo 
lilizua mjadala mkubwa kwani chama tawala, CCM, kilipinga na kuweka 
bayana kwamba kinataka muundo wa Muungano uendelee kuwa wa Serikali 
mbili.
Vyama
 vya upinzani kwa upande wake, viliunga mkono pendekezo hilo la muundo 
wa Serikali Tatu huku CUF kikienda mbali zaidi kwa kutaka Zanzibar ipewe
 mamlaka ya kuwa na dola kamili.
Katika Rasimu ya Kwanza ilipendekezwa mambo saba tu ndiyo yabakie kwenye mamlaka ya Muungano.
Mambo hayo ni pamoja na Katiba 
na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama, Uraia 
na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya 
Siasa na Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo 
ya Muungano.
Mambo hayo, ilipendekezwa na 
Tume hiyo kuwa chini ya wizara ambazo zitaongozwa na mawaziri wakazi 
ambao hawatatokana na wabunge kwani watatakiwa kuchaguliwa nje ya 
taasisi hiyo.
Kurejeshwa kwa jina la Tanganyika
Baada ya kutolewa kwa Rasimu ya 
Kwanza, mjadala mwingine ulioibuka hasa baada ya kupendekezwa kwa muundo
 wa Muungano kuwa wa Serikali Tatu ni hatua ya Tume kuendelea kutumia 
jina la Tanzania Bara.
Baadhi ya wadau walikosoa pendekezo hilo wakitaka jina la Tanganyika litajwe katika Katiba badala ya Tanzania Bara.
Katika Rasimu ya Kwanza, Tanzania Bara na Zanzibar zilihesabiwa kuwa washirika wa Muungano.
Ikiwa Serikali tatu zitarudishwa
 swali linakuja kama Tanzania Bara itatumia jina la Tanganyika ambalo 
ililitumia kuanzia mwaka 1961  hadi 1964 ilipoungana na Zanzibar.
Kufutwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu
Rasimu ya kwanza ilipendekezwa 
kufutwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu kwenye Serikali ya Muungano na badala
 yake kupendekeza kuwapo kwa Rais na Makamu wake.
Baadhi ya wadau walihoji juu ya usimamizi wa kazi za kila siku za Serikali jukumu ambalo kwa sasa lipo kwa Waziri Mkuu.
Umri wa kugombea urais
Suala hilo nalo lilizusha mjadala mkali wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya.
Mapendekezo ya Rasimu ya Kwanza 
yalitaka moja ya sifa za mgombea urais kuwa miaka 40 lakini baadhi ya 
wanasiasa, hasa vijana, wametaka umri huo ushushwe hadi miaka 35.
Wagombea binafsi
Jambo jingine lililopendekezwa katika Rasimu ya Kwanza ni kuwapo kwa mgombea binafsi kuanzia ubunge hadi urais.
Hilo halikuwa na mjadala mkubwa 
miongoni mwa wadau mbalimbali kutokana na ukweli kwamba ni jambo ambalo 
limekuwa likipigiwa kelele kwa muda mrefu na wananchi.
Muundo wa Bunge la Muungano
Rasimu ya Kwanza ilipendekeza kuwa wabunge watakuwa 75.
Kwa maana ya 50 kutoka Tanzania 
Bara, 20 kutoka Zanzibar na watano kutoka kundi maalumu ambao 
watateuliwa na Rais kwa ajili ya kuwatetea watu wenye ulemavu.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya Rasimu ya Kwanza, wabunge wa kuchaguliwa watagombea kupitia mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Rasimu ya kwanza ilipendekeza 
kuwa kila mkoa utachagua mbunge mmoja wa kike na wa kiume ili kuleta 
uwiano na kupendekeza kufutwa kwa viti maalumu suala ambalo lilizua 
mjadala.
Haki za Binadamu
Moja 
ya mambo ambayo yaliibuka mjadala ni haki za binadamu. Katika Rasimu ya 
Kwanza, ilipendekezwa kuundwa kwa Tume ya Haki za Binadamu itakayokuwa 
na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wasiozidi saba.
Lakini wadau wengi waliotoa maoni yao walitaka sheria kandamizi 40 za Tume ya Nyalali zisiwepo katika Katiba Mpya.
Mambo mengine
Kuhusu madaraka ya Rais, Tume 
hiyo ilipendekeza katika Rasimu yake ya Kwanza kwamba yabaki kama 
yalivyo hasa kwa uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu, pia ashirikiane na 
taasisi na vyombo vingine katika uteuzi.
Katika Rasimu hiyo ya Kwanza, 
pia ilipendekezwa kusiwepo na uchaguzi mdogo, isipokuwa kama nafasi hiyo
 itaachwa na mgombea binafsi lakini kama ni wa kutoka katika chama cha 
siasa, ijazwe na mtu kutoka chama chake.
Kuhusu Tume ya Uchaguzi, Tume 
hiyo ilipendekeza katika Rasimu ya Kwanza kwamba jina la Tume ya 
Uchaguzi ya Taifa (NEC), libadilishwe na iitwe Tume Huru ya Uchaguzi.
Rasimu
 hiyo, ilipendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court), 
majaji wa Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani watateuliwa na Rais, 
baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment