NYASI
 za uwanja wa Kinesi , jijini Dar es salaam zinaendelea kuhimili daluga 
za wekundu wa msimbazi, Simba SC, ambao wanajiandaa na mechi ya ufunguzi
 ya michuano ya kombe la Mapinduzi januari mosi, majira ya saa 2:00 
kamili usiku dhidi ya AFC Leopard kutoka Kenya, nuwanja wa Amaan, 
kisiwani Unguja.
Simba
 iliyopangwa kundi moja na timu za  KMKM, AFC Leopard ya Kenya pamoja na
 KCC kutoka Uganda inaendelea kujifua chini ya kocha msaidizi, Seleman 
Matola `Veron`, huku kocha mkuu Mcroatia, Zdravko Logarusic `Loga` 
akitarajia kuwasili Zanzibar januari 2 mwakani.
Kaimu
 Afisa habari wa klabu hiyo, Stanley Philipo `Stan` ameuambia mtandao 
huu kuwa wanatarajia kuendelea na mazoezi leo jioni, huku wakitarajia 
kung`oa nanga jijini Dar es salaam kueleka Zanzibar jumanne (Desemba 
31).
“Maandalizi
 ni mazuri sana. Ongezeko la wachezaji wapya na kocha mpya kumeleta 
mabadiliko katika kikosi, wachezaji wanajituma zaidi kutafuta namba 
kwani mwalimu hawajuii”. Alisema Stanley.
Stanley
 aliongeza kuwa kukosekana kwa kocha mkuu hakujaathiri chochote kwani 
Matola ni kocha mzuri na ataongoza timu  katika mchezo wao wa kwanza 
dhidi ya miamba ya soka kutoka nchini Kenya, AFC Leopard.
“Mechi
 ya ufunguzi itatupa dira halisi ya michuano ya msimu huu. Tunaheshimu 
ubora wa Leopard, lakini tunajipanga vizuri kuhakikisha tunapata ushindi
 wa kwanza na kuongeza imani kwa mashabiki wetu”. Alisema Stanley.
Kaimu
 Afisa habari huyo alisema,  kombe la Mapinduzi ni nafasi nzuri ya 
kuandaa kikosi chao kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu soka 
Tanzania bara, hivyo mashabiki watarajie soka zuri na la uhakika.
“Tumekuwa
  wakati wa mpito kutengeneza timu, lakini sasa dawa imeanza kupatikana 
kutokana na mabadiliko ya kikosi na benchi la ufundi yaliyofanywa. 
Umefika wakati wa mashabiki wetu kupata burudani ya soka”. Alijisifu 
Stanley.
Wakati
 huo huo, kocha msaidizi wa Simba SC, Seleman Matola amejigamba kuwa 
mtihani aliopewa na bosi wake ataumudu vizuri katika mchezo wa kwanza 
huko Zanzibar.
Matola
 alisema klabu hiyo itashusha kikosi kamili , wala haina mzaha na 
mashindano hayo kutokana na umuhimu wake  katika kujenga kikosi chao.
“Simba itashuka na kikosi kizima. Malengo ni kutwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi”. Alisema Matola.
Logarusic
 na Matola walirithi mikoba ya makocha waliofukuzwa kazi, Abdallah 
Kibadeni na Jamhuri Kiwhelo `Julio` baada ya kumalizika mzunguko wa 
kwanza wa ligi kuu soka Tanzania bara, huku Simba ikiwa nafasi ya nne na
 pointi 24.
Mbali
 na mabadiliko ya benchi la ufundi, Simba imefanya usajili katika 
dirisha dogo na kuwaongeza kikosini makipa Ivo Philip Mapunda na Yaw 
Berko.
Wanandinga
 wengine ni Juma Awadh Issa, Ali Badru, Donald Mosoti, na Uhuru Seleman 
Mwambungu, ingawa TFF imewataka kufanya marekebisho katika usajili wao.
Zilibaki
 nafasi tano, lakini wamewaombea usajili wachezaji sita (6), hivyo 
wanatakiwa kupunguza,  kama watashindwa kufanya hivyo, kamati Kamati ya 
Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania 
(TFF) itafanya yenyewe.
Kocha
 Logarusic anatarajia kuwatumia wachezaji wote ikiwa ni mikakati yake 
kuandaa kikosi cha kwanza cha ligi kuu soka Tanzania bara, ngwe ya lala 
salama inayotarajia kuanza kushika kasi januari 25 mwakani.
Mbali
 na Simba SC, timu nyingine za Tanzania bara zitakazoshiriki michuano 
hiyo ni mabingwa watetezi, Azam fc, Dar Young Africans na Mbeya City.

No comments:
Post a Comment