TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Thursday, February 12, 2015

JAMII YATAKIWA KUWASAIDIA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM – MAMA SALMA KIKWETE

3
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimpongeza mtoto Mohammed Hashim mara baada ya kuimba wimbo wa Taifa.
……………………………………………………………………………………..
Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete ameitaka jamii kutumia sauti zao  kuwasemea watoto wenye mahitaji maalum kwani watoto hao wanakabiliwa na changamoto  mbalimbali na hawana mtu wa kumwambia matatizo yao.

Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa rai hiyo jana alipotembelea kitengo cha wanafunzi wenye mahitaji maalum kilichopo shule ya Msingi Mpilipili wilaya ya Lindi mjini.
Alisema watoto wenye mahitaji maalum wanakabiliwa na changamoto nyingi ukilinganisha na watoto wengine  pia matatizo yao hayafanani hivyo basi ni jukumu la kila mtu katika jamii kuwasaidia watoto hao ili waweze kuishi kama watoto wengine.
“Katika kitengo hiki kuna watoto wenye tatizo la usonji (Autism) na wasiosikia (viziwi), kila mtoto anahitaji lake na  pale anapokabiliwa na tatizo anatakiwa kusaidiwa kwa haraka  ili asijisikie kunyanyapaliwa. Nawapongeza walimu mnaowafundisha watoto hawa kwani kazi hii ni ngumu na inahitaji moyo wa ziada”, alisema Mama Kikwete.
Akisoma taarifa ya kitengo cha wanafunzi wenye mahitaji maalum mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mpilipili Fadhili Mtitima alisema kitengo hicho kilianzishwa mwaka 1993 kikiwa na wanafunzi watano na hivi sasa kuna wanafunzi 20 wenye tatizo la usonji 16 kati yao wavulana ni 16 na wasichana wawili na wasiosikia (viziwi) wawili msichana mmoja na mvulana mmoja.
Mwalimu Mtitima alisema njia zinazotumika kuwapata wanafunzi hao ni wanafunzi wa kawaida kutoa taarifa ya uwepo wa watoto wenye mahitaji maalum katika mitaa yao kwa walimu, wazazi ambao wamehamasika huwaleta watoto kujiunga na shule, kutoa hamasa na matangazo kwa jamii katika maadhimisho ya wiki ya elimu kwa wote na kupitia sensa ya watoto inayofanyika  kila mwaka.
“Changamoto zinazotukabili ni watoto wengi wanaoishi mbali na kitengo wanakosa fursa ya kupata elimu kutokana na umbali uliopo, baadhi ya wazazi wa watoto wenye ulemavu hawawaandikishi watoto wao wakiwa na imani kuwa watoto hawa hawafundishiki, idadi ya walimu haitoshelezi kwani kuna walimu wawili kati ya wanne wanaohitajika kufundisha watoto wenye tatizo la usonji.
“Kitengo hakina mwalimu mtaalamu wa elimu ya walemavu wasiosikia na walimu kutojitokeza kujiendeleza katika mafunzo ya kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum”, alisema Mwalimu Mtitima.

Akiwa shuleni hapo Mama Kikwete aliwaita na kuwasalimia wanafunzi wa kawaida na kuwahimiza kusoma kwa bidii, kufuata sheria za shule na kuwatii walimu wao kwa kufanya hivyo watafanya vizuri katika masomo yao na kufika hadi elimu ya Chuo kikuu.
“Licha ya kusoma kwa bidii na kuhudhuria darasani mwanafunzi bora anatakiwa kuwahi shuleni na kufanya kazi za shule ikiwa ni pamoja na kusafisha eneo lake”, alisisitiza.
Kwa upande wa mimba za utotoni aliwasihi  kuepuka vishawishi na mazingira yatakayowapelekea  kupata ujauzito kwani mimba zitawazuia kuendelea na masomo na hivyo kukatisha ndoto za maisha yao.
Wakati huo huo Mama Kikwete alifanya vikao na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama Chama Cha Mapinduzi  katika matawi ya Mtuleni ‘B’ na Mpilipili Kaskazini na kuwataka  wazazi kuwakanya watoto wao pale wanapoona njia wanayoenda siyo sahihi.
Mama Kikwete alisisitiza, ”Hivi sasa vijana wengi tuliowazaa sisi wenyewe wanatumika kufanya vurugu zinazotishia  amani ya nchi lakini tukumbuke vita inapotokea waathirika wakubwa ni wanawake, watoto, walemavu na wazee hivyo basi tukae chini na kuzungumza na watoto wetu ili wasikubali kufanya mambo haya.
Katika Tawi la Mtuleni  ‘B’ Mama Sharifa Mkufu ambaye ni balozi wa nyumba kumi katika mtaa wa Ripsi alimshukuru Mama Kikwete kwa semina ya mabalozi aliyoiandaa iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana ambayo imemsaidia katika utendaji wake wa kazi.
“Nilisoma katiba ya Chama na kuitisha kikao cha mwezi na kuwafundisha wengine yale niliyojifunza, watu waliuliza maswali mbalimbali yahusuyo chama chetu na kutoa maoni yao baada ya hapo utendaji wangu umebadilika naweza kufanya kazi zangu vizuri tofauti na mwanzo”, Mama Mkufu alisema.
Aidha MNEC huyo aliongea na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika tawi la Mpilipili Kaskazini na kuwasisitiza kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, kuipigia kura ya ndiyo katiba inayopendekezwa na kuchagua kiongozi mwenye sifa katika uchaguzi mkuu ujao.
Mama Kikwete alisema, “Nawapongeza wananchi wa Kata hii katika uchaguzi uliopita wa Serikali ya mitaa mmewachagua wanawake wengi kuwa viongozi wenu  hili ni jambo jema, pia nawapongeza wanawake waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. Ninawaomba wanawake wenzangu katika uchaguzi mkuu ujao msiogope jitokezeni kwa wingi kugombea nafasi za uongozi.
Akiwasalimi wananchi waliohudhuria mkutano huo Mkuu wa wilaya ya Lindi Dkt. Nassoro Hamidi aliwaomba viongozi wa dini kuwahimiza waumini wao kukubali matokeo ya uchaguzi  kwani katika Ulimwengu wa kawaida kama watu hawatakubali matokeo ya uchaguzi matokeo yake huwa ni vurugu zinazohatarisha amani.
Dkt. Hamidi alisisitiza, “Pigeni vita ukabila na udini ugomvi wa hivi vitu unaweza kusababisha vita katika jamii ili amani iliyopo iendelee kudumu na tuweze kuitumia gesi inayopatikana katika mkoa wetu ambayo itatuletea maendeleo ni lazima tuishi kwa upendo, umoja na mshikamano”.
Naye Omary Chatanda ambaye alikuwa Mwenyekiti  wa mkoa wa Lindi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuhamia CCM aliwasihi vijana wenzake kutokubali kutumika katika vurugu zinazoharibu maendeleo yao  kwani chama chochote cha siasa lengo lake kuu ni kushika dola.
Mama Kikwete yupo wilayani humo kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010 .

No comments:

Post a Comment