Japan na Korea Kusini zimefikia makubaliano ya kihistoria kuhusu wanawake waliolazimishwa kuhudumu katika madanguro kama watumwa wa ngono wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Japan imeomba msamaha na kukubali kulipa yen 1bn ($8.3m, £5.6m) ambazo zitawekwa kwenye hazina ya waathiriwa itakayosimamiwa na Korea Kusini.
Mzozo huo umeathiri uhusiano kati ya mataifa hayo mawili, Korea Kusini ikitaka kuombwa msamaha “kwa dhati” na kutolewa kwa fidia kwa waathiriwa.
Mwafaka wa sasa ndio wa kwanza kuhusu suala hilo tangu 1965 na umepatikana baada ya pande zote mbili kuahidi kuharakisha mazungumzo.
Tangazo hilo limetolewa baada ya waziri wa mashauri ya kigeni wa Japan Fumio Kishida kuwasili Seoul kwa mashauriano na mwenzake Yun Byung-se.
Baada ya mkutano Kishida aliambia wanahabari kwamba Waziri Mkuu Shinzo Abe ameomba msamaha kutoka kwa “wote walioathirika”.
Wanawake takriban 200,000 walilazimishwa kuwa watumwa wa ngono kwa wanajeshi wa Japan wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya DUnia, wengi wao wakitoka Korea.
Ni 46 pekee kati yao walio hai Korea Kusini.
Wengine walitoka Uchina, Ufilipino, Indonesia na Taiwan.
Japan ilikuwa awali imekubali lawama kwenye taarifa iliyotolewa 1993 na katibu wa baraza la mawaziri wa wakati huo Yohei Kono.
Hazina ya kibinafsi ilianzishwa 1995 kwa ajili ya waathiriwa na ikadumu kwa mwongo mmoja.
Pesa hizo hata hivyo zilitoka kwa michango ya wahisani na si kutoka kwa serikali ya Japan.
No comments:
Post a Comment