Baadhi ya wenyeviti toka Halmashauri ya wilaya ya Kishapu wakimsikiliza mkufunzi (hayupo pichani) wakati wa mafunzo ya uraghabishi yaliyofanyika wilayani hapo
Na Krantz Mwantepele
“Unakuja kwenye ofisi yangu na kutoa taarifa za ubadhirifu wa mtendaji wa kijiji. Nakuuliza, je umechukua hatua zipi kama kiongozi wa kijiji kabla kuja kwenye ofisi yangu? Unanijibu hapana, hii si sahihi,”
Hayo ni maneno ya mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Hashim Mgandilwa, aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wenyeviti wa vijiji, watendaji wa kata na vijiji kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Loliondo, mwezi Agosti mwaka huu.
Alisema hayo kwa lengo la kufafanua dhana ya uwajibikaji kwa viongozi kama njia muhimu ya kutatua kero zinazowakabili wananchi wa maeneo ya vijijini katika wilaya yake.Ni dhahiri kwamba viongozi wa ngazi za vijiji na kata wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiutendaji katika maeneo husika.
Kuna nafuu kwa watendaji wa kata na vijiji, ambao ni waajiriwa wa serikali na hupewa kazi kutokana na miongozo, lakini siyo kwa wenyeviti wa vijiji na madiwani, wakati mwingine hata wabunge.
Akielezea changamoto hiyo wakati wa mafunzo ya wenyeviti wa vijiji kupitia mradi wa Chukua Hatua yaliyofanyika Septemba mwaka huu na shirika mdau la CABUIPA, mwenyekiti wa kijiji cha Nyakafulu kilichopo wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita, Salum Said amesema:
“Baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa kijiji hiki, hakika sikufahamu vya kutosha kuhusu majukumu yangu mapya kama kiongozi. Na hii ni changamoto kubwa kwa wenyeviti wa vijiji karibu vyote vya wilaya yetu.” Yeye ni mmoja kati ya wenyeviti 200 wanaopatiwa mafunzo katika mikoa ya Shinyanga, Geita na Simiyu.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba, katika awamu ya kwanza ya mradi wa Chukua Hatua, nguvu kubwa iliwekwa katika kuwawezesha wananchi kuwachukulia hatua watendaji na viongozi wabadhirifu wa mali za umma.
Wakati wananchi wakiwezeshwa kuwasimamia viongozi wao, viongozi hawakuwa wakiwezeshwa kutimiza majukumu yao kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi wao. Hivyo, haja ya kutoa mafunzo kwa viongozi hao ili waweze kutimiza majukumu yao kwa wananchi waliowachagua, ilikuwa lazima.
Akielezea umuhimu wa kuwawezesha wenyeviti wa vijiji wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wenyeviti na watendaji wa kata Julai 2015, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, Jane Mutagurwa alisema:
“Kwa muda mrefu wenyeviti mmekuwa mkilalamika kusahaulika kwenye programu zetu za mafunzo, fursa ndio hii imekuja. Tunafahamu kwamba wenyeviti wetu mnakutana na changamoto nyingi za kiutendaji zinazotokana na uwelewa mdogo katika majukumu yenu, hasa kwa wale wanaoingia madarakani kwa mara ya kwanza. Hivyo mtumie mafunzo haya vizuri.”
No comments:
Post a Comment