Dar es Salaam. Siku moja baada ya kifo cha meneja wa operesheni wa kampuni ya Zantel, Gabriel Rafael Kamukala, ndugu wameleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini alikutwa na nakala ya risiti iliyotumika kutoa Sh10 milioni kutoka Benki ya Standard Chartered. Mdogo wa marehemu, Gration Kamukala alidai kabla ya kuuawa, Rafael alionekana akiwa na mtu ndani ya gari ambaye hakufahamika, lakini baada ya kufanyika mauaji hayo mtu huyo alikimbia kusikojulikana. “Lakini hatukufahamu fedha hizo anakwenda kufanyia kazi gani kwa sababu alikuwa na ujenzi wa nyumba yake kule Madale. Tunaomba polisi izingatie mazingira hayo,” alisema mdogo huyo. Juzi, polisi walisema ndani ya gari la marehemu walikuta simu, laptop na fedha taslimu Sh1 milioni. Rafael aliuawa juzi saa 4.45 asubuhi baada ya kupigwa risasi na majambazi katika eneo la Ofisi za Nabaki Afrika, Mikocheni ikiwa ni saa chache baada ya kutoka duka la Shoppers Plaza. “Kwa sasa tumeondoa mwili wake kutoka Hospitali ya Mwananyamala na tumeuhamishia Lugalo, kesho tunatarajia Mungu akipenda tutauhifadhi katika makaburi ya Kinondoni,” alisema Kamukala. Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura aliitaka familia ya marehemu kuwa na uvumilivu wakati jeshi hilo likifanya kazi ya uchunguzi ili kuhakikisha ukweli wa kifo chake unajulikana na wahusika wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria. Wambura alisema taarifa hizo ni sehemu ya kazi ya uchunguzi unaofanywa na polisi, hivyo ni vema kuwa na subira ili kufanikisha kazi hiyo. “Hao ndugu wamefika hapa kituoni, lakini sikuwapo ila taarifa zote tunazifanyia kazi. Hatuwezi kufanikiwa kama tutakuwa tunatoa kila sehemu ya taarifa tunazofanyia uchunguzi, nadhani wangekuwa wavumilivu kidogo tukamilishe kazi yetu,” alisema. Msemaji wa familia, Paul Mashauri alisema marehemu ameacha mjane, Melinda Kamukala na watoto wawili ambao ni Gabriel Junour (15) na Adriel Kamukala (6). “Utaratibu wa mazishi unaendelea na familia imeshtushwa sana na msiba huu, ” alisema. Mtoto wa marehemu, Gabriel Junior alisema kabla ya kupata taarifa za msiba huo, alimpigia simu baba yake saa 5 asubuhi na kupokewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni ofisa wa polisi. “Nilimuuliza baba yuko wapi? akasema kuna matatizo yamejitokeza ila hakusema zaidi. Dakika chache geti likafunguliwa mama akaingia akilia, basi nikafahamu kilichoendelea,” alisema kijana huyo. Mjane wa marehemu huyo hakuweza kuzungumza kutokana na hali ya majonzi kutawala, lakini rafiki wa karibu wa marehemu, Dk David Mwenesano alisema hakuamini msiba huo hadi alipokwenda kushuhudia mwili katika Hospitali ya Mwananyamala.
No comments:
Post a Comment