UTENDAJI MBAYA NA MAAMUZI MABOVU YA KAZI ZA WAWAPELEKEA WENYEKITI KUMCHUKULIA HATUA MWENYEKITI WAO WA KIJIJI.
Kijiji hiki kinapatikana kata ya Masumbwe wilaya ya Mbogwe, mkoa wa Geita. Jumla ya wakazi 2,454 wanaishi katika kijiji hiki wakijishughulisha na shughuli za kilimo, uchuuzi na uchimbaji wa madini. Fredson Yaida ni mmoja kati ya waraghabishi wanaofanya kazi na program hii, kama walivyo waraghabishi wengine yeye pia alichaguliwa na wananchi na baadaye kuhudhuria mafunzo maalumu ya uraghabishi,
“Baada ya kuchaguliwa basi tulienda kwenye mafunzo kule Ushirombo. Kule tulijifunza na kujengewa uwezo wa kufahamu mapato nmatumizi, kujua vyanzo vya mapato vya maeneo tunayotoka, haki na wajibu wetu katika kusimamia mali za umma lakini pia kuweza kuzihojia pale inapohitajika,” anaelezea Fredson Yaida. Kwa kuwa mraghabishi hana mamlaka ya kisheria ya kuitisha mikutano kwa ajili ya kuwashirikisha wananchi wote kile alichojifunza, badala yake amekuwa akitembelea vikundi mbalimbali kwa ajili ya uhamasishaji na kushirikishana. Vikundi hivyo ni pamoja na Mkombozi, Jiandae na Twende na Wakati; kila kikundi kina wastani wa wanachama 25 mpaka 30.
“Tukaanza kuhojiana sisi kwa sisi vipi mbona magari yanasomba tu, watu wakasema tuyasimamishe yasisombe, bahati nzuri serikali ya kijiji ikaliona hilo kwa haraka, wakawa wameitana mwenyekiti wa kijiji na wajumbe na mtendaji wa serikali ya kijiji. Wakaliwekea mkakati wa kulifuatilia,” anaelezea Fredson Yaida.
Kamati ya serikali ikiwa tayari imeshanusa kilichopo mbele yao iliwalazimu kuchukua hatua za haraka kujinusuru na hasira za wananchi, kama anavyoelezea mjumbe wa kamati ya kijiji, Makemba Kubezia,“Tukaanza kujiuliza sisi wenyewe wa kamati ya kijiji, mh, mbona huu mchanga unatoka kwenye mashimo yetu pasipo sisi kujua, labda hapo mwenyekiti amefanya bila kutuhusisha serikali ya kijiji. Baadaye basi katika ufuatiliaji wananchi wakaanza kutuhoji ikabidi tuamke kweli na kuchukua Hatua stahili,”
No comments:
Post a Comment