Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kulia)
akimsikiliza Mwenyekiti wa kikundi cha Nyakalalo kililopo kijiji cha
Kitigiri wilayani Geita, Gideon Msabila (kushoto) ambaye alimuelezea
jinsi walivyonufaidika na mkopo wa mfuko wa maendeleo ya vijana fedha
ambazo zimewawezesha kufungua duka la rejareja la bidhaa za nyumbani.
Picha na Anna Nkinda – Maelezo
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kulia)
akimsikiliza Mwenyekiti wa kikundi cha Bodaboda kilichopo kijiji cha
Bugalama wilayani Geita, Enos Komanya wakati alipotembelea kikundi
hicho ambacho kilipata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo wa halmashauri.
Waziri Dk. Mukangara alitembelea kijiji hicho jana ili kuona fedha za
mkopo zilizotolewa na mfuko wa maendeleo ya vijana zimewasaidiaje vijana
kujikwamua kimaisha.
Vijana
wa kikundi cha kusaidiana kulima cha Busaka katika kijiji cha Kitigiri
wakifurahia fedha shilingi 50,000/= walizopewa jana na Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (wanne kulia) kwa
ajili ya kununulia soda za sikukuu ya Krismasi . Waziri Dk. Mukangara
aliwahimiza vijana hao kujiunga kwenye vikundi vya maendeleo vya kilimo
ili weweze kupata mkopo wa kununulia pembejeo na kuweza kuzalisha
chakula kwa wingi zaidi.
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (wanne
kulia) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wilaya ya Geita,
Kata ya Bukondo na kijiji cha Kitigiri mara baada ya kumaliza ziara
yake katika kijiji hicho jana ili kuona fedha za mkopo za mfuko wa
maendeleo ya vijana zimewasaidiaje vijana kujikwamua kiuchumi.
……………………………………………………
Na Anna Nkinda – Maelezo, Geita
Vijana wametakiwa kushiriki
katika suala la ulinzi na usalama wa maeneo wanayoishi kwa kujiunga na
vikundi vya ulinzi shirikishi ili kulinda na kusimamia rasilimali za
vijiji vyao.
Hilo litafanikiwa endapo vijana
watakuwa na moyo wa kujituma na kutambua kuwa wanajukumu la kujenga
taifa kwa kuhakikisha kuwa wanajiletea maendeleo yao na nchi kwa ujumla
kutokana na kazi mbalimbali wanazozifanya.
Rai hiyo imetolewa mjini hapa
jana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella
Mukangara wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wanavikijiji vya
Bugalama na Kitigiri vilivyopo wilayani Geita alipozitembelea baadhi ya
Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) zilizopata mkopo kupitia
mfuko wa maendeleo wa vijana na fedha za maendeleo ya mfuko wa
Halmashauri.
Dk. Mukangara alisema kuwa
maendeleo ya nchi yanawategemea vijana ambao ndiyo nguzo ya taifa hivyo
basi wizara yake kupitia halmashauri za wilaya itahakikisha kuwa inatoa
mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana jambo la muhimu ni kujiunga katika
vikundi vya maendeleo ili waweze kufikiwa kwa urahisi.
“Uongozi wa kijiji uhakikishe kuwa
unawahimiza vijana na kuwajengea uwezo katika mtazamo wa
kujitengemea, kujituma na kufanya kazi na kujiunga kwenye vikundi vya
maendeleo ili iwe rahisi kupata mkopo kupitia SACCOS zilizopo vijijini
mwenu” alisema Dk. Mukangara.
Aliwataka wanakijiji hao
kuwasimamia vijana wao ili wanawajibike na kutambua kuwa wanajukumu
kubwa la kuhakikisha kuwa wanashiriki katika shughuli za kilimo cha
chakula na biashara jambo ambalo litasababisha kuwa na chakula cha
kutosha na kuepukana na janga la njaa.
No comments:
Post a Comment