Waziri
wa Ajira na Kazi, Gaudensia Kabaka (kushoto), akitembelea moja ya
miradi mikubwa ya ujenzi wa shule inayotekelezwa na mgodi wa North Mara
unaomilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold (ABG) wakati wa ziara
yake kwenye mgodi huo uliopo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara hivi
karibuni. Kushoto kwa waziri ni Mkurugenzi wa ABG wa Mahusiano na
Serikali, Bw. Emmanuel ole Naiko.
…………………………………………………………
MWANDISHI WETU
Tarime
SERIKALI imewataka wafanyakazi wa
sekta ya madini kuwa watulivu wakati inafanyia kazi malalamiko yao
kuhusu fao la kujitoa katika mifuko ya hifadhi ya jamii, ambapo amesema
inaandaa utaratibu maalumu utakaowawezesha wanachama wa mfuko husika
kunufaika nao wakiwa kazini ama baada ya kumaliza utumishi wao.
Serikali imewasisitizia wafanyakazi nchini kuwa suala hilo limepewa kipaumbele ili kupatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
Ari hiyo ilitolewa hivi karibuni
na Waziri wa Ajira na Kazi, Gaudensia Kabaka, wakati akizungumza na
wafanyakazi wa mgodi wa dhahabu wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya
African Barrick Gold (ABG) wakati wa ziara yake kwenye mgodi huo uliopo
wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara.
Waziri huyo aliwasihi wafanyakazi
wenye mawazo ya kuacha kazi ili tu wachukue mafao yao ya kujitoa
kuachana na fikra hizo potofu ambazo alisema zitaleta athari kwa familia
zao.
Bi.Kabaka amesema serikali
imesikia kilio cha wafanyakazi we sekta ya madini na wengine na kwamba
kwa pamoja na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya
Jamii (SSRA), wako katika jitihada za kuangalia jinsi ambavyo wanachama
walioandikishwa kwenye pensheni kama wanaweza kuanzishiwa utaratibu wa
kuweka na kukopa yaani “supplementary scheme.”
”Serikali haijafikia uamuzi
wakati wowote wa kufanya kuhusiana na mtu ama watu wanaotaka kujitoa
katika fao hilo ndio maana niko hapa,” alisema.
Alitangaza kuwa serikali
itakutana na SSRA na watu wa sekta ya madini jijini Dar es Salaam tarehe
7 Januari, kwa ajili ya kupata mawazo yao juu ya suala la mafao ambapo
wafanyakazi wa Migodini watawakilishwa na wawakilishi wao amabo ni
chama cha wafanyakazi.
Alisema kuwa serikali haina haraka juu ya suala hilo kwa kuwa inataka kusikiliza mawazo yawananchama wote, Watanzania, wabunge na wadau mbalimbali ili kupata maoni ambayo yatatafsiriwa kisheria.
Alisema serikali itawasikiliza
Watanzania ili kujua ni nini wanapenda kiwepo katika masuala ya hifadhi
ya jamii kwa sababu sheria na sera siyo msahafu hivyo inaweza kubadilika
kila mara kutokana na mahitaji ya wakati husika.
Waziri Kabaka pia alitembelea
miradi mbalimbali ya jamii inayofadhiliwa na mgodi huo wa Barrick na
kuisifu kampuni hiyo kwa kusaidia jamii.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa shule mpya na ukarabati mkubwa wa kituo cha afya cha Nyangoto.
No comments:
Post a Comment