Na Anna Nkinda – Maelezo, Kagera
…………………………………………
Serikali Mkoani Kagera
imevikopesha vikundi mbalimbali vya maendeleo vya vijana kupitia Vyama
Vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) zaidi ya shilingi milioni 83 katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita ilikuwawezesha vijana waweze kujiajiri wenyewe na kujikwamua kiuchumi .
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa
huo Kanali Mstaafu Fabian Massawe wakati akisoma taarifa fupi ya mkoa
kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella
Mukangara aliyepo mkoani humo kwa ajili ya kuangalia jinsi fedha za
mkopo kutoka mfuko wa vijana zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua
kimaisha.
Kanali Mstaafu Massawe alisema
kuwa Serikali inasimamia utekelezaji wa sera ya maendeleo ya vijana kwa
kuratibu shughuli za mifuko ya vijana na kufuatilia utoaji na
urejeshaji wa mikopo, kuhamasisha vijana na kufufua moyo wa kujitolea na
kukuza na kuendeleza vipaji mbalimbali walivyonavyo vijana ili
kuwawezesha kujiajiri kupitia mafunzo yanayohusu stadi za kazi na maisha
“Changamoto tunazokabiliana nazo
katika kuwakopesha vijana ni mahitaji makubwa ya mkopo ukilinganisha na
uwezo wa SACCOS au wakopeshaji wengine, urejeshaji hafifu wa mikopo
kutoka kwa wakopaji, ukosefu wa ajira, uvivu na uzurulaji, vijana kutaka
mafanikio kwa haraka na matumizi ya madawa ya kulevya kwa baadhi ya
vijana”, alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Aliendelea kusema kuwa ili
kukabiliana na changamoto hizo Serikali ngazi ya mkoa inafuatilia kwa
karibu ili kuona kwamba matamko ya sera ya Taifa ya Maendeleo ya vijana
yanazingatiwa na kuingizwa katika maendeleo ya Halmashauri lengo kuu ni
mkoa kuwa na vijana wenye ari ya kuwajibika na kushiriki kikamilifu
katika maendeleo ya jamii, wazalendo, wenye maadili na kupenda nchi yao.
Kwa upande wake waziri Dk.
Mukangara alisema kuwa hivi sasa Serikali inaangalia uwezekano wa
kuongea mkopo kwa SACCOS zinazolenga shughuli za maendeleo ya vijana
kutoka shilingi milioni tano hadi kumi kwani mahitaji ni makubwa na
hayakidhi haja.
Mkoa wa Kagera unakadiriwa kuwa
na idadi ya watu 2,739,492 kati ya hao wanawake 1,386,669 na wanaume
1,353,123 ambapo vijana ni 903,608 wenye umri wa miaka 15 hadi 35 sawa
na asilimia 33 ya wakazi wote ambapo kati ya hao wa kike ni 459,867 na
wa kiume 443,741.
No comments:
Post a Comment