…………………………………………………..
MAANDALIZI ya Mkutano Mkuu wa
Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) yanaenda
vizuri na wajumbe wanatarajiwa kufika Bagamoyo Ijumaa Desemba 28, 2012
mchana kwenye hoteli ya Kiromo View Resort watakapolala na kufanyia
mkutano.
Ijumaa hiyo washiriki watatembelea
maeneo mbalimbali ya kihistoria Bagamoyo na jioni kutakuwa na mechi ya
kirafiki kati ya timu ya soka ya TASWA FC na Bagamoyo Veterani
itakayofanyika Uwanja wa Mwanakalenge na usiku wajumbe watakuwa na
chakula cha pamoja na kubadilishana mawazo kuhusiana na masuala
mbalimbali yahusiyo michezo na taaluma ya habari.
Mkutano Mkuu utafunguliwa Jumamosi
Desemba 29, saa tatu asubuhi na mgeni rasmi atakuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Kusaidia timu za Taifa za Vijana, Ridhiwani Kikwete.TASWA
imechukua jukumu la kumualika kutokana na kuwa mdau mkubwa na rafiki wa
chama chetu.
Mkutano utafungwa jioni ya siku hiyo na Mkurugenzi
wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene ambaye hiyo pia itakuwa
nafasi nzuri kwake kuweza kuzungumza na wana habari kuhusiana na masuala
mbalimbali ya kitaaluma.
Katika mkutano huo wanachama wa
TASWA watapata fursa ya kupokea na kujadili Ripoti ya Utendaji ya chama,
Mapato na Matumizi, maendeleo ya chama na masuala mbalimbali yanayohusu
waandishi wa habari za michezo na maendeleo ya michezo kwa ujumla
Pia kutakuwa na semina maalum
itakayoendeshwa kwa washiriki wa mkutano huo, ili wawe na uelewa
kuhusiana na ajenda ya kuinua kipato kwa wanachama ambayo nayo
itajadiliwa kwenye mkutano huo.
Kamati ya Utendaji ya TASWA
imekubaliana iwasaidie wanachama wake waweze kujitegemea kwa kuanzisha
Chama cha Akiba na Mikopo (SACCO’S), lakini imeamua kwanza iwaite
wataalamu wa vyama vya ushirika watoe elimu juu ya jambo hilo na
kukishakuwa na uelewa wa kutosha suala hilo litakuwa kama ajenda kamili
ya kuanzisha chama hicho kwenye mkutano wetu.
No comments:
Post a Comment