Afisa
Madini Mkaazi Tunduru Fredrick Mwanjisi (kushoto) akifurahia jambo
wakati akimwongoza Katibu Mkuu Nishati na Madini Eliakim Maswi (wa pili
kushoto) kutembelea eneo itakapojengwa ofisi ya Madini Tunduru. Wengine
katika picha ni ujumbe wa Maafisa walioongozana na Katibu Mkuu na
watumishi wa ofisi ya Madini Tunduru.
Jengo
ambalo litatumika kama Makao Makuu ya Ofisi ya Madini Kanda ya Ziwa
Nyasa mjini Songea. Jengo hilo limenunuliwa na Wizara na litaanza
kutumika mara baada ya ukarabati. Wengine katikati ni Kaimu MKurugenzi
Idara ya Utawala Wizara ya Nishati na Madini, Caroline Msika na wengine
ni maafisa wWizara ya Nishati na Madini na Maafisa wa Madini Kanda
waliofuatana na Katibu Mkuu.
Kamishna
wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul Masanja, (wa kwanza kushoto)
akitafakari jambo mara baada ya kukagua kiwanja kitakapojengwa ofisi ya
Madini ya Kamishna Mkaazi wa Madini, Nachingwea. Wa pili kushoto ni
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, wa kwanza,
wengine ni Afisa Madini Mkaazi Nachingwea, Mhandisi Mayigi Makolobela
(wa pili kulia) na wa kwanza kulia ni Mjiolojia kutoka ofisi ya Madini
Mtwara.
======= ======== =======
Na Asteria Muhozya, Songea
Kamishna
wa Madini Tanzania, Mhandisi Paul Masanja ameeleza kuwa, Serikali
kupitia Wizara ya Nishati na Madini itajenga kituo maalum cha kuuza na
kununua madini ya vito kutokana na nchi kuwa na hazina kubwa ya madini
jambo ambalo pia litachangia katika kuyaongezea thamani madini hayo.
Masanja
ameyasema hayo mjini Songea wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Nishati
na Madini Eliakim Maswi kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na
wizara ikiwemo kuonana na Makamishna Wasaidizi wa Kanda, Maafisa Madini
Wakaazi, Watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania, kuangalia shughuli za
wachimbaji wadogo wakiwemo wafanyabiashara wa madini na wawekezaji
katika sekta ya madini.
Kamishna
aliongeza kuwa, kituo hicho kitakuwa na huduma zote muhimu zikiwemo za
kibenki ambazo zitawawezesha wachimbaji na wafanyabiashara kutokutafuta
huduma muhimu zinazoendana na shughuli hizo nje ya kituo hicho.
“Shughuli zote za uuuzaji na ununuzi madini ya vito na usonara
zitafanywa katika kituo hicho.
Kutakuwa
pia na helkopita itakayotua moja kwa moja katika jengo hilo jambo
ambalo litawezesha uwepo wa usalama katika biashara nzima ya kuuza na
kununua madini,” alisisitiza Masanja.
Aidha,
aliongeza kuwa, ili kuiwezesha sekta hiyo kupaa kwa kasi na kuchangia
katika ukuaji wa uchumi, wizara imeamua kuanza kwa kuboresha ofisi za
kanda za madini ikiwa ni pamoja na kununua maeneo maalum kwa ajili ya
kujenga ofisi hizo ili kuboresha utendaji wa sekta ya madini nchini na
kuwa na ofisi za uhakika.
“Tunataka
kupitia sekta ya madini kuiwezesha serikali kuongeza mapato yake na
kutoka hapa tulipo kiuchumi. Jambo hilo linawezekana ndio sababu
tunaanza na kuboresha sehemu za kazi ili kuwawezesha watumishi kufanya
kazi katika mazingira mazuri zaidi na kuongeza uwajibikaji,”aliongeza
Masanja.
Katika
hatua nyingine, Kamishna Masanja amewataka Makamishna Wasaidizi wa
Kanda na Makamishna Wakaazi walioteuliwa hivi karibuni kutimiza wajibu
wao vizuri na kufikia lengo la makusanyo ambayo wizara imewapangia na
kwa wale wasiotekeleza agizo hilo la makusanyo ndani ya kipindi cha
miezi mitatu wataondolewa katika nafasi zao.
“Tumeamua
kupaa kupitia sekta hii, asiyeweza kutekeleza jambo hili kama
tulivyokubaliana, tutamwondoa na kuwapa wengine wenye uwezo wa kufanya
hivyo. Tunataka kufanya kazi kwa kasi na kisasa zaidi,” alisisitiza
Masanja.
Wakati
huo huo, aliwata watumishi wote walioko katika ofisi za Kanda kuwa
waadilifu, wawajibikaji, wawazi na wabunifu ili kuweza kutekeleza
majukumu yao kikamilifu ikiwemo kufuata sheria, taratibu na kanuni za
utumishi wa umma.
Vilevile,
aliongeza kuwa, wizara imejipanga kuanza kutumia mfumo wa kieletroniki
kuanzia mwezi Septemba kwa ajili ya waombaji wa leseni jambo ambalo
litasaidia kurahisisha zoezi la uombaji wa leseni na kuondoa
manungu’niko miongoni mwa waombaji.
No comments:
Post a Comment