Michuano ya Ligi Daraja la Pili
(SDL) msimu huu iliyokuwa ianze kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu kwa
mechi kumi katika viwanja vitano tofauti imesogezwa mbele hadi Desemba 6
mwaka huu.
Mechi hizo zimesogezwa ili kutoa
fursa ya kukamilisha maandalizi mbalimbali ya ligi hiyo inayoshirikisha
timu 24 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.
Mikoa yenye timu katika ligi hiyo
ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Katavi, Kigoma, Lindi, Mara,
Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga,
Singida na Tabora.
MASHINDANO YA TAIFA YA U12 YASOGEZWA
Mashindano ya Taifa kwa vijana
wenye umri chini ya miaka 12 yanayoshirikisha kombaini za mikoa yote ya
Tanzania yatafanyika jijini Mwanza kuanzia Desemba 30 mwaka huu hadi
Januari 5 mwakani.
Awali mashindano hayo yalipangwa
kuanza Desemba 6 mwaka huu, lakini yamelazimika kuyasogeza ili kutoa
fursa ya kukamilika kwa matengenezo ya viwanja vitatu ambayo vitatumika.
Kila timu ya mkoa inatakiwa kuwa
na ujumbe wa watu 16, wakiwemo wachezaji 14 na makocha wawili katika
mashindano hayo ya timu yenye wachezaji saba (7 aside).
Timu zinatakiwa kuwasili jijini
Mwanza kuanzia Desemba 28 mwaka huu tayari kwa ajili ya uhakiki wa umri
na taratibu nyingine za mashindano. Timu zote zitafikia katika shule ya
Alliance (Alliance Schools).
Wachezaji wanaotakiwa kushiriki
mashindano hayo ni wenye umri chini ya miaka 12, hivyo ni wale
waliozaliwa kuanzia Januari 2003 na kuendelea.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MUNYUKU, KARASHANI
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko vifo vya waandishi wa habari
Innocent Munyuku na Baraka Karashani vilivyotokea jana (Novemba 19 mwaka
huu) jijini Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa katika
familia ya mpira wa miguu, na tasnia ya habari nchini kwa ujumla
kutokana na mchango mkubwa waliotoa katika ustawi wa mpira wa miguu
nchini kupitia kalamu zao.
Munyuku alikuwa mmoja wa
waandishi waanzilishi wa gazeti la Mwanaspoti wakati Karashani kwa
nyakati tofauti alifanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari
ikiwemo kampuni ya New Habari 1996 akiripoti habari za mpira wa miguu.
Tunatoa pole kwa familia za
marehemu, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), na
kampuni ya New Habari 1996 na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu
katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment