Wanamgambo wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria, ambao chanzo chake kinatajwa kuwa ni ukosefu wa ajira na ujinga.
Rais mstaafu wa Nigeria, Jenerali Olusegun Obasanjo (aliyeinama) akimuonyesha kitu Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin William Mkapa, katika mkutano wa marais wastaafu uliofanyika jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.
Rais mstaafu wa Nigeria, Jenerali Olusegun Obasanjo (aliyeinama) akimuonyesha kitu Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin William Mkapa, katika mkutano wa marais wastaafu uliofanyika jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.
SIRI ya
kuanza kwa kundi la ugaidi la Boko Haram linaloendesha vitendo vyake vya
kigaidi nchini Nigeria, iliyofichuliwa wiki iliyopita na aliyekuwa rais
wa nchi hiyo, Olusegun Obasanjo, sasa inaweza kuiathiri Tanzania.
Obasanjo,
akiwa katika kikao na viongozi wenzake wastaafu jijini Dar es Salaam,
alisema ukosefu wa elimu na ajira kwa vijana wa nchi hiyo ndiyo chimbuko
la Boko Haram.
Onyo hilo la
Obasanjo kwa serikali za Afrika kujikita katika kutatua tatizo la
ukosefu wa ajira na elimu linaweza kuwa chachu kwa viongozi wa Tanzania
kutafuta ufumbuzi badala ya kushambulia wanasiasa.
Obasanjo
aliongeza kuwa kundi la Boko Haram ambalo linatokea kusini mwa Nigeria,
limekusanya wapiganaji wengi ambao hawana ajira, huku wengi wao wakiwa
hawajapata elimu na ajira.
Akitoa
ushauri kwa nchi za Afrika kuondoa tatizo hilo ili kuhakikisha uchumi
wake unakua na kuondoa uwepo wa makundi kama hayo yanayosababisha
kushusha uchumi, ni lazima wahakikishe wanatoa elimu na kutengeneza
ajira kwa vijana wa mataifa yao.
Wito kama
huo umewahi pia kutolewa na viongozi kadhaa nchini, akiwamo aliyekuwa
Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, waliotaka kutafutwa kwa ufumbuzi wa
tatizo la vijana wasiokuwa na ajira.
Lowassa,
amekuwa akielezea namna ambavyo ukosefu wa ajira unavyotengeneza bomu
kwa vijana linalosubiri kulipuka muda wowote, akitolea mfano wa
kujitokeza kwa vijana 10,000 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakiwania
nafasi 70 pekee za kazi Idara ya Uhamiaji.
Katika
mazungumzo yake, Lowassa aliwaeleza wanahabari kwamba ili kuepusha
ongezeko hilo linalokua kwa kasi, serikali ni lazima ihakikishe
inatengeneza ajira kwa kuwa kila mwaka zaidi ya vijana 30,000 wanahitimu
katika vyuo mbalimbali nchini.
Lowassa
aliyejiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008, amekuwa akiishauri
serikali kuchukua hatua kukabiliana na tatizo la ajira, ambalo
limemsababishia malumbano na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka
aliyejibu mapigo Machi 21, 2012 bungeni kwa kutoa takwimu zinazoonyesha
namna serikali ilivyotengeneza ajira.
Kwa upande
wake, Mbowe alilalamikia serikali kwa kutokuwa makini kwa kushindwa
kulitafutia ufumbuzi tatizo la ajira kwa vijana ambalo aliomba liwe hoja
maalum bungeni, serikali kuu, halmashauri na katika baraza la mawaziri
kwani ni janga la taifa.
Wakati Mbowe
akichangia hotuba ya Waziri wa Fedha bungeni kuhusu mapendekezo ya
serikali ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2014/15, alisema
ajira ni mkakati na siyo suala la kufumania.
Akielezea
njia za kuondoa tatizo hilo, aliishauri serikali kubadili mfumo uliopo
wa kurundika kila kitu serikali kuu katika kutengeneza ajira kwani
haiwezi kufanikiwa na badala yake alitaka kuwe na mkakati wa kutengeneza
ajira katika halmashauri zote 133.
Mbowe
alisema kuwa haoni sababu ya kuwa na wakurugenzi na wataalam wa uchumi
katika halmashauri wasiokuwa na uwezo wa kutengeneza ajira.
Aliishauri
serikali kuanzisha Mamlaka ya Majengo (Real Estate Authority – REA)
itakayohusika kusimamia majengo mijini na kukusanya fedha kwa ajili ya
kusaidia kujenga ajira kwani bila ya kufanya hivyo, vijana watalazimika
kukimbilia mijini kwa sababu vijijini hakuna maendeleo wala mwelekeo.
Alisema ni
aibu kwa halmashauri za Kinondoni na Ilala kutegemea ruzuku toka
serikali kuu wakati zina vyanzo vingi vya mapato ambavyo vinaweza
kusaidia kutengeneza fedha na ajira kwa vijana.
Aliongeza
kuwa idadi ya Watanzania kwa sasa wanafikia milioni 50 na kila mwaka
wahitimu wa vyuo vikuu wanafikia zaidi ya 40,000 huku kukiwa hakuna
ajira.
Tanzania
Daima Jumapili, imedokezwa kuwa kutovalia njuga kupuuza ushauri huo
kunaweza kuchangia kushamiri kwa makundi ya kihalifu kama Boko Haram
aliyoitaja Obasanjo.
Tayari hapa
nchini kumezuka makundi ya kihalifu ambayo baadhi yao ni Watoto wa Mbwa,
Panya Road na Badface ambayo yalitikisa maeneo mbalimbali kwa uhalifu
uliozimwa na vyombo vya dola, lakini unaweza kuzuka tena siku za usoni.
Vijana hawa
wamekuwa wakienda kupora wakiwa kundi kubwa lenye watu 30 hadi 100
wakiwa wamebeba silaha za jadi ambazo huzitumia kuwashambulia
wanaowapora.
Zipo taarifa
nyingine zinasema kwamba vijana hao hutumia njia ya kuimba kwa sauti
kubwa wimbo huu; “Tunatakaa… pesa zetuu..!” huku wakiingia ndani
kuchukua vitu vya thamani na kuwaacha baadhi ya majirani wakiduwaa kwa
kudhani mtu anadaiwa kumbe anaibiwa.
Makundi ya vijana hawa yanaelezwa kuwa maskani yao yapo maeneo ya Manzese, Kigogo, Mburahati, Kigogo Luhanga na viunga vyake.
Vijana
wanaofanya uhalifu kama huo, pia wamekuwa wakipatikana katika Mkoa wa
Mara wakitumia majina ya Jamaica Mob, Mbio za Vijiti na Midomo ya Furu
ambao mara kadhaa wamekuwa wakiwasumbua wakazi wa mkoa huo kwa kuwaibia
na baadaye kuwajeruhi kwa silaha za jadi.
Mkoani Kilimanjaro pia liliibuka kundi la vijana lililokuwa likifanya uhalifu lijulikanalo kwa jina la Kunguru Hafugiki.
Tanzania
Daima Jumapili, limekuwa likifuatilia baadhi ya nyendo za viongozi wa
serikali katika kutatua kero za ajira, ambao wengi wao wamekuwa wakitoa
zawadi za fedha na ahadi kwa vijana wakati wa uchaguzi badala ya
kujikita kwenye miradi itakayokuwa endelevu.
Ahadi hizo
na fedha hizo ndizo zinadaiwa kuwajenga chuki vijana pindi zinaposhindwa
kutekelezwa na kujikuta wakishiriki kwenye vitendo vya kihalifu.
Chanzo: TanzaniaDaima: 'Boko Haram' waja nchini
No comments:
Post a Comment