KANISA la Waadventista wa Sabato la Pugu Chanika
lililopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam sasa linaweza kuendeleza mradi
wake wa ujenzi na upanuzi wa kanisa baada ya kupata msaada wa fedha wa shilingi
milioni 5 kutoka kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited
(IPTL). Msaada huo uliotolewa wakati wa ibada Jumamosi,
umefufua jitihada la kanisa za kutanua na kumalizia ukumbi wa kanisa uliopo
sasa pamoja na kumalizia ujenzi wa majengo mengine.
Mwakilishi kutoka IPTL ambayo ni kampuni tanzu ya Pan
African Power Solutions Tanzania (PAP), Bw. Joseph Makandege, ambaye ni Katibu
na Mwanasheria Mkuu wa kampuni hiyo, amesema msaada huo ni sehemu ya jitihada
za kampuni yake kuunga mkono miradi mbali mbali yenye manufaa makubwa kwa kijamii.
“Baada ya kupokea maombi toka katika kanisa hilo
ya kututaka kusaidia mradi huo wa ujenzi, Bodi ya wakurugenzi ya IPTL/PAP
ikiongozwa na Mwenyekiti Mtendaji Bw. Harbinder Singh Sethi mara moja
ilipitisha kiasi cha shilingi milioni 5 kwa kuwa inaamini kuwa taasisi za
kidini zinasaidia kulijenga taifa lenye watu wanaomuogopa Mungu na hivyo
kuifanya nchi iwe na mazingira mazuri ya kufanya biashara ambayo inasaidia
kuleta maendeleo ya kiuchumi.
“Tunaamini kuwa katika makanisa, familia
zilizotengana zinaunganishwa, waliuokosa matumaini wanapewa matumaini, na
maisha ya watu yanabadilika. Inampendeza Mungu kusikia sauti za nyimbo
zinazomtukuza, ujumbe madhubuti kutoka kwa wachungaji, ushuhuda wa kazi
zitokanazo na Mungu, na sauti nzuri za watoto zisema Amina.
“Kampuni yetu isingeweza kukataa ombi hilo la kusaidia
kanisa katika mradi ambao utatukuza kazi ya Mungu na maisha ya walio wengi
katika jamii yetu yatabadilishwa kwa ujumla,” alisema Makandege. Aliliasa kanisa kutumia fedha hizo vizuri ili
kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Naye, Mchungaji wa Kanisa hilo, Gallus Gido
aliishukuru IPTL/PAP kwa mchango wao ambao alisema umewagusa watu wengi na
utalisaidia kanisa kuweza kuwahudumia waumini wengi wanaomtukuza na kumuomba
Mungu.
"Katika kitabu cha Matendo 10:1-4, kulikuwa
na mtu aliyekuwa akitoa misaada/sadaka kwa jamii yake. Siku moja Mungu
alimtokea na kumwambia kwamba sala na sadaka zake zimefika mbinguni. Nataka
kuwaambia IPTL/PAP kwamba mchango wao wa kuendelea kusaidia taasisi mbalimbali
ya kidini na jamii kwa ujumla, utawafungulia milango mbinguni kwa ajili ya
baraka zaidi," alisema.
Mchungaji aliongeza kuwa mchango wa IPTL/PAP
unadhihirisha upendo wa kampuni hiyo kwa Mungu na watu, na kuhaidi kuwa
atafanyakazi kwa ukaribu na kamati ya ujenzi kuhakikisha kuwa fedha hizo
zinatumika vizuri kwa lengo lililokusudiwa.
No comments:
Post a Comment