Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abbas Kandoro
akisalimiana na wachezaji wa Timu ya Mbaspo wakati akifungua rasmi mashindano ya
Airtel Rising Stars.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abbas Kandoro
akisalimiana na wachezaji wa Timu ya Mbozi wakati akifungua rasmi mashindano ya
Airtel Rising Stars.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Abbas Kandoro akipiga mpira
kuashiria ufunguzi wa mashindano ya Airtel Rising Stars Mbeya
Kandoro afagilia mashindano ya vijana.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro amefungua rasmi
mashindano ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars mkoa
wa Mbeya na kusisitiza umuhimu kwa wadau wote wa soka kutilia maanani programu
za vijana. Ufunguzi huo ulifanyika kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya juzi
Jumatatu.
“Hii ndio njia pekee ambayo inaweza kutuletea
maendeelo ya soka na kuiwezesha nchi yetu kuondokana na matokeo mabaya katika
mashindano mbali mbali ya kimataifa”, alisema. Aliishukuru kampuni ya Airtel
Tanzania kwa kubuni programu hii ambayo imekuwa ikiwapa vijana fursa ya
kuonyesha na kuviendeleza vipaji vyao.
Aliwataka vijana kucheza kwa kujituma na kuwataka
wafahamu kwamba hatma ya mchezo wa soka kwa siku za usoni iko mikononi mwao “Miamba
yote ya soka ambayo tunaihusudu na kuishabikia hivi leo imepata mafanikio hayo
makubwa baada ya kuwekeza na kutilia manani soka la vijana na naamini kwamba
kwa mwendo huu na sisi tutapata mafanikio ya kuridhisha. Ni suala la muda tu”, alisema.
Amewataka viongozi wa chama cha soka mkoa wa Mbeya (MREFA)
kuyatumia vizuri mashindano ya Airtel Rising Stars ngazi ya mkoa na kuchagua
vijana nyota watakaounda timu ya mkoa kushiriki kwenye fainali za Taifa za Airtel
Rising Stars zinazotarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Agosti 10 hadi 17.
Fainali za Taifa zitashirikisha timu za wavulana na
wasichana kutoka mikoa ya kisoka ya Ilala, Temeke na Kinondoni. Timu nyingine
zitatoka Morogoro, Mwanza, Mbeya na Zanzibar. Alisema mbali na kutumika kubaini
vipaji vya soka, programu ya Airtel Rising Stars pia inatoa fursa kwa vijana
kushiriki mazoezi hivyo kuwafanya kuwa na afya njema.
Kalenda ya mwaka ya Airtel Rising Stars inatarajiwa
kufikia tamati mwishoni mwa mwezi huu ambapo zaidi ya nchi 20 za Afrika
zitachuana kwenye mashindano ya kimataifa yaliyopangwa kufanyika nchini Gabon.
Katika kindumbwendumbwe hicho Tanzania itawakilishwa na timu za wavulana na
wasichana zenye wachezaji 16 kila moja. Wawakilishi hao watachaguliwa wakati wa
fainali za Taifa jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa MREFA Juma Killa
ameishukuru kampuni ya Airtel kwa kubuni programu hii ili kutumika kama jukwaa
linatotumika kubaini vipaji vya wanasoka chipukizi. Alisema kuwa mashindano ya
Airtel Rising stars yameifanya kazi yao ya kutafuta vipaji vya soka kuwa rahisi
zaidi.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Meneja wa Airtel
Tanzania Kanda ya Mbeya Straton Mushi amewashukuru wadau wote wa soka kwa
kuyaunga mkono mashindano ya Airtel Rising Stars na kuyapa umuhimu yanaostahili.
No comments:
Post a Comment