Wasanii
wa fani ya Uchekeshaji mahiri kutoka
nchini Uganda,Kenya na Tanzania wakitoa burudani kwa washabiki na
wapenzi wa fani hiyo ,iliofanyika kwenye moja ya ukumbi wa hotel ya
Golden Tulip Jijini Dar,pichani shoto ni Fred Omondi kutoka
Kenya,mwanadada Anne Kansiime kutoka nchini Uganda na Mc Pilipili wa
Tanzania.
Sehemu ya washabiki na wapenzi wa fani hiyo wakivunjika mbavu kwa kucheka.
mwanadada Anne Kansiime
kutoka nchini Uganda akitoa burudani ya vichekesho kwa watazamaji
(hawapo pichani),ndani ya moja ya ukumbi wa hotel ya Golden Tulip jijini
Dar hivi karibuni
Kituo cha Radio 5, kimepongezwa na wadau wa sanaa
kwa mchango wake wa kukuza sanaa za vichekesho vya majukwaani hapa nchini.
Wadau hao wa sanaa za vichekesho vya majukwaani
waliipongeza Radio 5, wakati wa burudani ya wachekeshaji wa majukwaani
iliyofanyika mwishoni mwa wiki hii katika ukumbi wa Golden Tulip. Burudani hiyo ambayo ilifana sana iliwajumuisha
mchekeshaji kutoka Uganda, mwanadada Anne Kansiime, Fred Omondi kutoka Kenya na
Pilipili wa Tanzania.
Akizungumzia onyesho hilo, mmoja ya mashabiki
waliohudhuria onyesho hilo, amesema sanaa ya vichekesho vya majukwaani nchini
haijapewa kipaumbele kama aina nyingine za sanaa. ‘Watu wengi bado wanaamini sanaa za kuchekesha majukwaani
sio kazi rasmi kama kazi nyinginezo, lakini hii imeanza kubadilika hapa nchini,
na tutarajie mabadiliko zaidi kama wadau wengine kama radio 5 wakijitokeza
kusaidia’ alisema Farida Akida.
Akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari kuhusiana
na anavyoiona tasnia ya vichekesho vya majukwaani Afrika Mashariki, mchekeshaji
Anne Kansiime anasema anaamini sanaa ya vichekesho vya majukwaani inaanza
kujijengea heshima kubwa miongoni mwa wananchi. ‘Mimi sio mbunge au mwanasiasa, lakini nimepata mapokezi
makubwa, kwa kazi hii tu ya kuchekesha watu, hivyo naona hii tu pekee ni dalili
ya kukua kwa tasnia hii hapa Afrika Mashariki’ alisema Anne.
Ikiwa ni mara ya kwanza kwa mwanadada Kansiime kuja
Tanzania kutoa burudani, hasa baada ya kujijengea umaarufu mkubwa kupitia
vipande vyake vya vichekesho vilivyo mtandaoni, tiketi za burudani yake
ziliisha wiki moja kabla hajawasili. Katika usiku huo wa burudani ulioitwa, Cheka Kwa
Nguvu, mchekeshaji toka Tanzania, Pilipili aliwatoa kimasomaso mashabiki waliofurika
kwa vichekesho vyake vilivyoonekana kuwagusa mashabiki moja kwa moja.
Huku mashabiki wengi wakiwa hawamfahamu vyema,
Pilipili ambaye kitaaluma ni mwalimu, anasema aliacha kazi ya ualimu ili awe
mchekeshaji, hivyo kwake yeye, kuchekesha ni kazi kama kazi nyingine. ‘Kwangu mimi hii ni kazi ambayo najivunia, na
naamini nitaweza kuwawakilisha watanzania vyema kimataifa kupitia uchekeshaji,
na naishukuru Radio 5 kwa kunipa fursa ya kuonyesha kwamba ninaweza’ alisema
Pilipili.
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa kituo cha Radio 5, Robert Francis amesema huu ni mwanzo tu wa
kuwaandalia watanzania burudani za kipekee na watarajie mengi zaidi kutoka
Radio 5. ‘Sanaa ya uchekeshaji jukwaani bado haijapewa
nafasi kubwa hapa nchini, lakini kama mlivyoona, mashabiki wamejitokeza kwa
wingi sana kwenye burudani yetu, hivyo watu watarajie burudani za aina hii
nyingi zaidi kutoka kwetu’ alimaliza Francis.
No comments:
Post a Comment