Rais Jakaya Kikwete
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ameueleza mchakato wa kutafuta Katiba mpya nchini na changamoto zake
kama barabara ndefu yenye kona.Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa mchakato huo, kimsingi, unatakiwa kuongozwa
na ukweli kuwa Katiba ni kuhusu wananchi wenyewe na maisha yao na wala
siyo tu mchakato huo kuongozwa na idadi ya Serikali – mbili ama tatu.Rais
pia amesema kuwa ni dhahiri kuwa yapo mengi ambayo hayajakaa sawasawa
katika mchakato mzima hasa kuhusu jinsi Katiba mpya itakavyolinda maisha
ya wananchi na kusaidia kuboresha ustawi wao.Rais
Kikwete ameyasema hayo usiku wa Jumamosi, Agosti 2, 2014, kwenye
Hoteli ya Marriot Washington, mjini Washington wakati alipokutana,
akazungumza na kujadili na Watanzania wanaoishi katika Marekani hasa
kutoka maeneo ya jiji la Washington D.C., na majimbo ya Virginia,
Maryland, California na New York.Akiwaeleza
Watanzania kuhusu hali ilivyo nchini – kisiasa na kichumi – Rais
Kikwete amesema kuwa ni kweli kuwa mchakato wa kutafuta Katiba mpya
umekuwa unakabiliwa na changamoto kadhaa katika siku za karibuni.
Rais
Kikwete amewaambia Watanzania hao: “Najua kuwa mchakato wa Katiba
umekuwa na changamoto katika siku za karibuni lakini kwangu mimi
mchakato huo ni sawa na barabara ndefu ambayo haikosi kona. Kona
zitakuwepo lakini mimi ni mtu ambaye anaishi kwa matumaini na ni
matumaini yangu kuwa mchakato huo utaendelea na hatimaye kufikia mwisho
vizuri kama tunavyotarajia wote.”
Rais Kikwete ameongeza:
“Aidha, naamini kuwa yapo mengi kuhusu Katiba ambayo hayajapata muda wa
kutosha wa kuyajadili katika Bunge la Katiba. Kimsingi, Katiba ni
Katiba ya wananchi, ni Katiba kuhusu maisha yao na ustawi wao. Hili
jambo sijaona kama linaonekana sana katika mjadala wa Katiba.”
Ameongeza:
“Mchakato wetu kwa muda mrefu umekuwa kuhusu idadi ya Serikali, ziwe
mbili ama ziwe tatu. Kwangu mimi, idadi ya Serikali ni muhimu, lakini
naamini kuwa Katiba iwe ni kuhusu maisha yenyewe ya wananchi na ustawi
wao lakini mwelekeo mzima wa Mchakato huo usiwe kuhusu idadi ya Serikali
tu.”
Rais
Kikwete amesema kuwa anajua kuwa yamekuwepo maneno mengi kuhusu Katiba
lakini akaongeza kuwa anaamini majawabu ya changamoto na matatizo ya
sasa ya mchakato huo yatapatikana.
“Najua
kuwa maneno yamekuwa mengi lakini siyo ndiyo demokrasia ya wazi
inavyofanya kazi lakini sisi katika Serikali hatuna wasiwasi na hali
hiyo. Ndiyo mambo yanavyotakiwa kuwa katika nchi ambako demokrasia
inafanya kazi. Yale mambo yanayotusumbua kwa sasa yanazungumzwa na vyama
vyetu na naamini majawabu yatapatikana.”
Wakati
huo huo, Rais Kikwete amerudia kusema kuwa Serikali inaandaa utaratibu
wa kisheria ambao utalinda mapato yatakayotokana na mauzo ya rasilimali
ya gesi nchini kwa kizazi cha sasa cha Watanzania na vizazi vijavyo.
“Tutahakikisha
kuwa tunaanzisha Mfuko Maalum kulinda fedha zitakazotokana na mauzo ya
gesi. Raslimali hii pamoja na fedha ambazo zinatokana na rasilimali hiyo
siyo mali ya kizazi chetu tu bali ni mali ya vizazi vijavyo vya
Watanzania”.
Mwisho!
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
04 Agosti,2014
No comments:
Post a Comment