WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, William
Lukuvi, amesema anayekwamisha mjadala wa Katiba Mpya ni mmoja wa wajumbe
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Tundu Lissu.
Amesema kwamba, kama Lissu ataamua kubadili msimamo uwezekano wa Ukawa
kushiriki Bunge Maalumu la Katiba ni mkubwa kwa vile ana uwezo mkubwa wa
kushawishi, kujieleza na kujenga hoja.
Kutokana na hali hiyo, amemuomba Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alegeze kamba ili Ukawa warudi bungeni.
Lukuvi alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza katika mdahalo wa
Katiba Mpya ulioandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (UDASA).
“Namuomba Tundu Lissu awashawishi wenzake warudi bungeni, huyu ndiye
kimzizi kikubwa cha Ukawa, yaani kama kuna mchawi namba moja ni Lissu.
“Huyu akilegeza tu kamzizi kake, nawaambia tutaendelea na Bunge kama
kawaida. Tundu Lissu namfahamu sana na kwa muda mrefu ana uwezo mkubwa
wa kushawishi, ni mtaalamu wa sheria na ana uwezo wa kujifungia ndani
akaandaa kitu ili ashawishi watu hata kwa muda wa saa 12.
“Uncle, legeza kidogo kwa sababu wewe ndiye unayewaendesha hawa Ukawa,”
alisema Lukuvi huku akimnyooshea kidole Lissu aliyekuwa amekaa jirani
naye.
Pamoja na hayo Lukuvi alionyesha kutoridhishwa na uamuzi wa Ukawa
kususia Bunge Maalumu la Katiba kwa kuwa walikuwa wakielewa kilichokuwa
kikiendelea wakati wa mijadala ya Bunge hilo.
Kutokana na hali hiyo, alisema Ukawa hawana haja ya kuendelea kukaa nje ya Bunge hilo linalotarajiwa kuanza kesho mjini Dodoma.
“Nawaomba mrudi bungeni, utaratibu tulioweka katika kanuni utaenda
vizuri na kama kutakuwa na tatizo, tutatafuta njia ya kutatua kwa
makubaliano,” alisema.
Naye Lissu alipokuwa akichangia, alisema Ukawa hawataweza kushiriki tena Bunge hilo kwa kuwa kanuni za kuliendesha zimekiukwa.
Kwa mujibu wa Lissu, kinachotarajiwa kufanyika baada ya Bunge hilo
kuanza kesho ni CCM kuandaa rasimu ya Katiba wanayotaka kuliko
wanavyotaka wananchi.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha cha mjini Iringa, Profesa Gaudence
Mpangala, alisema wajumbe wa Bunge la Katiba wanatakiwa kuheshimu
rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi.
Wakati hayo yakiendelea, mjadala huo ulitawaliwa na zomea zomea baada ya baadhi ya washiriki kuzomewa.
Pamoja na wachangiaji kadhaa kuzomewa, aliyekumbwa na hali hiyo pia ni
Lukuvi ambaye alizomewa dakika chache kabla ya kuanza kuchangia. Wakati
akizomewa, baadhi ya washiriki waliondoka ukumbini wakionyesha kutotaka
kusikiliza alichokuwa akitaka kukichangia.
“Kama ni kuzomea, zomeeni kwa sababu mimi ni mzoefu wa kuzomewa,” alisema Lukuvi.
Wengine waliozomewa ni George Kinde ambaye alichangia kwa kumshambulia
aliyekuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba.
Katika mchango wake, Kinde alimshutumu Jaji Warioba kwa kusema kuwa
kitendo cha tume aliyoiongoza kupendekeza muundo wa Serikali tatu,
hakiwezi kukubalika kwa kuwa kitaliingiza taifa katika machafuko.
Kinde alipokuwa akiendelea kuchangia, baadhi ya washiriki wa mdahalo huo
walichachamaa na kumzomea huku wakitaka anyang’anywe kipaza sauti.
Baada ya kelele kuzidi, muongozaji wa mdahalo alilazimika kuchukua kipaza sauti na kumfanya Kinde asiendelee kuchangia.
Mwingine aliyezomewa alikuwa ni Dk. Emmanuel Makaidi ambaye alianza kuchangia kwa kupiga vita muundo wa Serikali mbili.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Jaji Joseph Warioba na wajumbe wa tume hiyo, wanatarajiwa kushiriki
mdahalo wa Katiba Mpya ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
Mbali na Jaji Warioba, wengine watakaoshiriki mdahalo huo ni pamoja na
wajumbe wa tume hiyo, Joseph Butiku, Dk. Salim Ahmed Salim, Profesa
Palamagamba Kabudi na Mwantumu Malale.
Taarifa iliyotolewa jana katika mitandao ya kijamii na mmoja wa
waliokuwa wajumbe wa tume hiyo, Hamphrey Polepole iliwataja wajumbe
wengine watakaoshiriki mdahalo huo ni Polepole mwenyewe pamoja na Rais
wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadh Ali Salim.
Taarifa hiyo ilisema mdahalo huo utarushwa moja kwa moja na kituo cha runinga cha ITV na Redio One.
No comments:
Post a Comment