Rais
mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi
akifungua Skuli mpya ya ,Sekondari ya Mapinduzi Chaani ikiwa ni shamra
shamra za kuadhimi miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
PICHA NA MAKAME MSHENGA-MAELEZO ZANZIBAR.
…………………………………………………….
NA RAMADHANI ALI /MAELEZO
Rais mstaafu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi amesema Zanzibar ni miongoni
mwa nchi chache Duniani zinazoendelea kutoa Elimu bila malipo tokea
kuasisiwa Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.
Akizungumza katika ufunguzi
wa Skuli mpya ya Sekondari ya Mapinduzi, Chaani katika maadhimisho ya
sherehe za kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mzee Mwinyi
amesema mafanikio hayo yanatokana na viongozi shupavu wa Mapinduzi na
wale waliofuatia kuongoza Zanzibar.
Amewapongeza viongozi na
wananchi wa Zanzibar kwa jumla kwa kuendeleza malengo ya Mapinduzi ya
1964 ya kuimarisha maendeleo katika nyanja mbali mbali.
Rais mstaafu amewahimiza wananchi kuendeleza Umoja kwani bila umoja na mshikamano hakuna maendeleo yatakayopatikana.
Amewashukuru wahisani
wanaosaidia maendeleo ya Zanzibar hasa katika nyanja ya elimu na afya
na amesema misaada yao itaendelea kuthaminiwa .
Amewataka wazee wa Chaani
kuendelea kuwasimamia watoto wao na kuhakikisha wanaitumia skuli hiyo
katika kubadilisha uwezo wao wa kusoma kuwa bora zaidi.
Akizungumza katika sherehe
hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna amesema
baada ya kupata msaada wa skuli mpya 19 za sekondari na Benki ya Dunia
na skuli mbili msaada wa BADEA, Wizara yake inatilia mkazo katika
kuondosha tatizo la walimu wa sayansi linalokabili Skuli nyingi za
Zanzibar.
Amesema Nigeria imewapatia msaada wa walimu 13 wa sayansi
na tayari wamefanya mazungumzo na nchi ya Marekani, Uingereza, Ghana,
India, Palestina, Misri na Oman na wote wameonyesha azma ya kusaidia
kupunguza tatizo hilo.
No comments:
Post a Comment