CHAMA
cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania(TABOA) kimepongeza hatua
zilizochukuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Dk Emmanuel Nchimbi
kupunguza kero katika usafiri wa mabasi iliyokuwa ikichangiwa na wingi
wa vituo vya ukaguzi vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha kimemtaka Waziri huyo
kudhibiti tabia inayofanywa na baadhi ya mabasi yasiyo na leseni za
usafirishaji, kusafirisha abiria kinyume na utaratibu uliopo,jambo
alilosema litasaidia kupatiakana kwa haki za abiria pindi tatizo lolote
litakapotokea.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana,Katibu wa Taboa Enea Mrutu alisema hivi karibuni walimuomba
Waziri huyo kuyafanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyoyopo barabarani,
ikiwemo ya kupunguza vituo vya ukaguzi, jambo alilosema kuwa
amelitekeleza kikamilifu na hivyo kuwaondolea usumbufu uliokuwepo.
Alisema mbali na kero hiyo pia
Nchimbi amefanikiwa kudhibiti tabia ya baadhi ya askari waliokuwa na
tabia ya kujificha vichakani na kujitokeza ghafla barabarani pindi
wanapoona basi limekalibia na kuliandikia faini kwa madai kuwa
lilikuwa katika mwendo mkali.
“Tunashukuru siku chache baada
ya kulilalamikia suala hili na kumuomba Waziri kulifanyia kazi, tayari
majibu yake tumeyaona na tunawaomba viongozi wengine wawe mfano wa
viongozi hawa ambao mara nyingi hufanyia kazi kero zinazofikishwa mbele
yao” alisema Mrutu.
Aidha alisema kumekuwepo na
mabasi katika mikoa mbalimbali yanayofanya kazi ya kusafirisha abiria
bila kuwa na leseni za usafirishaji, jambo alilosema ni hatari pindi
ajali inapotokea na hivyo kumtaka waziri kulisimamia suala hilo kupitia
kitendo cha usalama barabarani.
No comments:
Post a Comment