*Ataka makabila mengine yatunze historia zao.
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
amezindua kitabu cha historia ya kabila la Wapimbwe lililoko mkoani
Katavi na kutayataka makabila mengine kuandika historia zao ili waweze
kutunza kumbukumbu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Akizindua kitabu hicho hivi
karibuni mjini Mpanda, Waziri Mkuu aliwataka watu wa makabila mengine ya
mkoa wa Katavi ambayo ni Waruira, Wabende, Wakonongo na Warungwa
wafanye tafiti kuhusu mila na tamaduni zao na kisha waandike vitabu
vyao.
Kabla ya uzinduzi huo, mtunzi wa
kitabu hicho, Bw. Peter Mgawe alisema kitabu hicho kimetokana na
utafiti uliofanywa tangu mwaka 2007 ambao ulilenga kukusanya taarifa na
masimulizi mbalimbali kutoka kwa wazee wa Kipimbwe ambao wameishi miaka
mingi huku wakiwa na hazina ya mila na tamaduni za kabila hilo ambalo
pia ni kabila lake Waziri Mkuu Pinda.
“Hili ni kabila dogo
lisilofahamika na wengi, nimekuwa nikitafuta taarifa na machapisho
(literature) mbalimbali kuhusu kabila hili lakini sikuwahi kupata
chochote… ndipo nikamshirikisha Mheshimiwa Waziri Mkuu juuya kufanya
utafiti na kuandika historia yetu naye akalikubali wazo langu,” alisema
Bw. Mgawe ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo cha Ustawi wa Jamii,
Kijitonyama, Dar es Salaam.
Akizungumza na wakazi
waliohudhuria uzinduzi huo, Waziri Mkuu alisema utafiti huo usiishie
hapo tu, bali wafanye tafiti nyingine kuhusu mavazi, vyakula, ndege,
wanyama waliokuwa wakipendelewa na mababu zao ili kuongeza hazina ya
taarifa ya kabila hilo.
“Lengo la kitabu hiki lilikuwa
ni kuhifadhi katika maandishi historia ambayo ilikuwa imefichika ndani
ya vichwa vya wazee wetu kutoka vijiji mbalimbali vya Mpimbwe… nafurahi
kwamba tunao wazee watatu waliokuwa katika warsha ya kwanza kabisa
iliyofanyika mwaka 2008. Leo hii wako hapa na wanashuhudia matunda ya
kazi yao,” alisema Waziri Mkuu.
Wazee hao ni Mzee Simba Pangani
Kalulu (76) kutoka kijiji cha Mamba, Mzee Valeri Kipande (76) kutoka
kijiji cha Lyangalile na Mzee Moses Kasalani (67) kutoka kijiji cha
Mirumba. Vijiji vyote hivyo viko wilaya ya Mlele, mkoani Katavi.
Waziri Mkuu amerejea jijini Dar
es Salaam leo mchana (Jumanne, Januari 9, 2013) akitokea kijijini kwake
Kibaoni, wilayani Mlele, Katavi ambako alifanya ziara ya siku 10 kwenye
jimbo lake la Katavi na kisha kuwa na mapumziko ya Krismasi na mwisho wa
mwaka.
No comments:
Post a Comment