Na Mwandishi Wetu
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) na Jeshi la Polisi nchini wameunda
kikosikazi maalum kitakachokuwa kikifuatilia uharamia na maovu
mbalimbali katika shughuli za Sanaa na Burudani.
Kikosikazi
hicho kimeundwa baada ya Jeshi la Polisi nchini kutumia Sanaa
shirikishi katika kutoa elimu kwa wadau wa Sanaa kuhusu dhana ya polisi
jamii na ulinzi shirikishi kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila
wiki makao makuu ya BASATA Ilala Sharif Shamba.
Akizungumza
kuhusu kikosikazi hicho, Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa, BASATA Bi. Vivian
Shalua alisema kuwa, kazi kubwa ya kikosi hiki itakuwa ni kufuatilia
maonesho yasiyokuwa na vibali, uharamia kwenye kazi za wasanii na
wasanii kutoka nje wanaoingia nchini kinyume cha sheria.
Aliyataja
majukumu mengine ya kikosikazi hicho kuwa ni pamoja na kudhibiti
maonesho yanayodhalilisha utu na maadili ya mtanzania, kusimamia utoaji
vibali kwa wasanii wa kitanzania wanaoenda kufanya maonesho nje ya nchi
na majukumu mengine yatakayojitokeza.
“Kikosikazi
hiki kitakuwa tayari kufuatilia taarifa yoyote ya uharamia kwenye kazi
za wasanii, maonesho yanayodhalilisha utu na maadili ya mtanzania na
wasanii wanaoingia ndani ya nchi na kufanya maonesho bila vibali”
alisisitiza Shalua.
Kikosikazi
hicho kinaundwa na Shani Kitogo (Afisa Utamaduni Ilala), Tatia Ramadhan
(Polisi, TAZARA), Afande Jeremiah (Polisi Kati), Koplo Juma Mashauri
(Polisi Airport), Michael Kagondela (Idara ya Utamaduni), Afande Deus
Matoro (Reli) na Afande Swai (Traffic),
Wengine
ni Vivian Shalua (BASATA), Jonathan Abel na Tatu Burhan (Uhamiaji),
Deus Kessy (Polisi Reli), Koplo Josephat Syllively (Polisi – Maji),
Masanja Nyalali (Polisi – Airport) na PC Mwakajaby (Polisi – TAZARA)
Akizungumza
kwenye Jukwaa hilo la Sanaa, Asp Edson Kasekwa kutoka Polisi Makao
Makuu Kitengo maalum cha Operesheni uzuiaji uhalifu,alisema kuwa, Jeshi
la Polisi linawategemea wadau wa Sanaa wakiwemo wasanii katika kutoa
taarifa juu ya matukio ya uharamia na uhalifu kwa ajili ya ufuatiliaji
na udhibiti.
“Ni
vema Wasanii na wadau wa Sanaa kwa ujumla wakaonesha ushirikiano kwa
Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa na kudhibiti uharamia na maovu
kupitia sekta ya Sanaa. Hii ndiyo maana ya dhana hii ya polisi jamii na
ulinzi shirikishi ya polisi kushirikiana na jamii” alisema Afande
Kasekwa.
Kikosikazi
hiki kimeundwa huku kukiwa na taarifa za uwepo wa vikundi mbalimbali
vinavyofanya maonesho yenye kudhalilisha utu na maadili ya mtanzania
huku uharamia kwenye kazi za Sanaa ukizidi kushika kasi.
No comments:
Post a Comment