NA: BASHIR NKOROMO, MUSOMA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeukabidhi mkoa wa Mara tani za saruji kwa
ajili ya ujenzi wa madarasa mkoani humo ikiwa ni sehemu ya maadhimnisho
ya miaka 35 ya CCM.
Saruji hiyo itatumika kujenga madarasa kwa ajili ya wanafunzi ambao
wameshindwa kuanza kidato cha kwanza kutokana na uhaba wa madarasa licha
ya kufaulu mwaka huu.
Akikabidhi mifuko hiyo kwa mkuu wa mkoa huo, John Tupa, Katibu wa NEC
ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema saruji hiyo imetolewa na
makada wa CCM ambao wameamua kutoa mchango huo kwa kupitia CCM ikiwa
ni kuunga mkono maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM.
Nape
alisema makada hao ni Zulfikar Nanji wa Kampuni ya Mwanza Huduma Ltd
(mifuko 400) Joseph 'Msukuma' Kasheku mfanyabiashara ambaye pia Diwani
wa Kata ya Nzela, Geita na Mjumbe wa NEC, Vedastus Mathayo ambao wote
wametoa mifuko 100 kila mmoja.
Alisema kada mwingine ni Dk. Isack Chacha Ng'ariba ambaye aliahidi
kutoa tani 200 za saruji ahadi ambayo aliitoa papo hapo wakati wa
makabidhiano hayo.
Nape aliwashukuru wafanyabiashara makada hao wa CCM kwa kuiunga mkono
CCM katika kuhakikisha kwamba sherehe za miaka 35 ya CCM inakuwa na
mafanikio makubwa kwa kutekeleza azma ya kuchangia shughuli za
maendeleo.
Alisema, wafanyabiashara na makada hao wanaichangia CCM pia kama
kuonyesha shukurani yao kwa kuweza kufanya biashara zao kwa miaka mingi
katika mazingira ya amani na utulivu chini ya uongozi wa serikali ya
CCM.
"Mkiona
vinaelea vimeundwa, amani na utulivu huu uliopo ni mazingira
yaliyojngwa na kuendelea kutunzwa na CCM tangu ilipoanza kutawala nchi
hii baada ya kurithi uongozi kutoka vyama vya TANU NA ASP miaka 35
iliyopita", alisema Nape.
Akipokea
msaada huo, Mkuu wa mkoa alisema, jumla ya watoto 6486 kati ya
asilimia 50.3 ya watoto waliofaulu, wameshindwa kuanza kidato cha
kwanza mkoani mwake kutokana uhaba wa vyumba vya madarasa licha ya
kufaulu.
Mkuu huyo wa mkoa alisema mkoa unahitaji madarasa 718 wakati yaliyopo
ni 479 na hiyo kuwa na upungufu wa madawati 239 na kwamba wilaya ya
Bunda ndiyo inayoongoza kuwa upungufu wa madarasa.
Alisema licha ya kupata msaada huo wa saruji bado mkoa unahitaji mabati, mbao na madawati kwa ajili ya madarasa yatakayojengwa.
No comments:
Post a Comment