Mkuu
wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu (mwenye kaunda suti nyeusi)
akisikiliza maelezo ya kilimo kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Songea Thomas
Sabaya (kulia) wakati wa ziara ya kukagua usambazaji wa pembejeo
kijiji cha Lugagara wilaya ya Songea
Mkuu
wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu akiongea na watendaji wa
vijiji vya Magagula.Muungano Zomba na Lugagara wilaya ya Songea jana
alipotembelea kuhamasisha wakulima kuzalisha mahindi kwa kuzingatia
kanuni bora za kilimo.Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas
Sabaya(kulia) na mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea Rajab Mtiula(Picha
na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma)
Wakulima
wa kijiji cha Magagula wilaya ya Songea wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa
Ruvuma Said Mwambungu (hayupo pichani) jana alipofanya ziara ya kukagua
shughuli za kilimo
Revocatus A.Kassimba
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ruvuma
Serikali
imewataka wakulima mkoani Ruvuma kulima kwa wingi mahindi katika msimu
huu kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo licha ya changamoto za soko
lililowakabiri msimu wa kilimo uliopita.
Kauli
hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu
wakati wa ziara yake katika vijiji vya Magagula, Lugagala na Muungano
Zomba vilivyopo wilaya ya Songea .
Mwambungu
aliwaeleza wananchi kuwa serikali inatambua kero ya ununuzi wa mahindi
iliyotokea msimu wa 2011/2012 ambapo wakulima wengi walichelewa
kupokea fedha zao kutoka Wakala wa Hifadhi za Chakula (NFRA).
Aliongeza
kusema kuwa changamoto ya fedha za wakulima hazitajitokeza tena msimu
ujao kwani tayari serikali imejiandaa kwa kutengwa fedha katika bajeti
ili kuhakikisha mahindi yote yatanunuliwa kwa wakati.
“Limeni
kuliko mwaka jana kwani serikali imejipanga kununua kwa wakati na
kuhakikisha kuwa hakuna mkulima atakayecheleweshewa malipo na serikali”
alisema Mwambungu na kuongeza kuwa hakuna mkulima sasa anayeidai
serikali wote wamelipwa.
Mkuu
wa mkoa Mwambungu alisisitiza kuwa serikali inafanya kila
linalowezekana kuondoa kero ya kukopa mahindi ya wakulima hivyo ni vema
wakulima wakaendelea kuunga mkono juhudi hizi za serikali kwa kuongeza
uzalishaji.
Katika
msimu 2011/2012 wa kilimo kwa mujibu wa taarifa za Wakala wa Hifadhi
ya Chakula jumla ya tani 50,018 za mahindi zimenunuliwa kutoka kwa
wakulima mkoani Ruvuma zenye thamani ya shilingi bilioni 17.5 ambapo
kilo ilinunuliwa kwa shilingi 350.
Mkuu
wa Mkoa alitumia fursa hiyo kuwapongeza wakulima wa vijiji hivyo
alivyovitembelea kwa kutumia vema pembejeo za ruzuku kwa mfumo wa vocha
kwani wameongeza uzalishaji wa mahindi na kuifanya wilaya ya Songea
kuongoza katika kuzalisha mahindi mkoani.
Ziara
ya Mkuu wa mkoa ilihusisha pia kukagua zoezi la ugawaji wa vocha za
pembejeo ambapo kwa mujibu wa taarifa ya iliyotolewa na Mkuu wa wilaya
ya Songea Thomas Sabaya alisema wilaya imepata mgao wa vocha 64,417
ambazo zimesambazwa kwa wakulima.
Sabaya
alisema vocha hizo zinahusisha mbegu bora za mahindi, mbolea ya
kupandia na mbolea ya kukuzia ambapo bei ya mfuko wa mbolea ya kupandia
(DAP) inauzwa shilingi 80,000/=huku mkulima akichangia shilingi
52,000/=.
Kuhusu
mbolea ya kukuzia (UREA) mfuko unauzwa shilingi 72,000/= na mkulima
anachangia shilingi 52,000/= huku serikali ikilipia zinazobaki na kwa
mbegu bora mfuko unauzwa shilingi 40,000/= huku mkulima akichangia
20,000/= na serikali zinazobakia.
Kwa
upande wake Afisa Mtendaji wa kijiji cha Lugagara Bi Taifa Mahundi
katika risala yake alisema wakulima wana changamoto kubwa ya upungufu
wa vocha za ruzuku hivyo akaiomba serikali kuongeza mgao kwa kijiji.
Mkuu
wa mkoa akijibu hoja hiyo aliwafahamisha wananchi kuwa vocha
zinazotolewa ni vigumu kufanana na idadi ya wakulima kwani hiyo ni
ruzuku itolewayo na serikali kuwasaidia wakulima kujenga uwezo wa
kujitegemea.
Katika
msimu huu wa kilimo mkoa wa Ruvuma umepatiwa vocha za ruzuku ya
pembejeo za kilimo 192,000 ambapo kwa mwaka uliopita ulipatiwa vocha
204,000 hivyo kuwa na upungufu wa vocha 12,000/=.
Mkoa
wa Ruvuma ni kati ya mikoa sita maarufu kwa uzalishaji wa mahindi
nchini ambapo mikoa mingine ni Iringa, Mbeya, Rukwa, Kigoma na
Morogoro.
No comments:
Post a Comment